1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Facebook yaondoa akaunti za bandia za Urusi

31 Oktoba 2019

Mtandao maarufu wa kijamii wa Facebook umeondoa akaunti tatu za mitandao  nchini Urusi, kurasa na makundi, kama sehemu ya mkakati wake unoendelea wa kukabiliana na akaunti bandia zinazotumika kuwahadaa watumiaji.

Symbolbild Facebook Verschlüsselung
Picha: REUTERS

Kampuni ya Facebook imesema kwenye taarifa yake kwamba ingawa watu wanaohusika na mitandao hiyo walijaribu kuficha utambulisho wao na namna wanazivyoratibu kurasa hizo lakini uchunguzi uliofanywa na Facebook umehusisha kampeni za mitandao hiyo na watu wenye mahusiano na mfadhili ambaye ni raia wa Urusi Yevgeniy Prigozhin ambaye huko nyuma aliwahi kushitakiwa na wizara ya sheria ya Marekani.

Prigozhin ni mlengwa muhimu anayeshukiwa kwa kufadhili taasisi ya uchunguzi wa wakala wa utafiti wa intaneti ama Internet Research Agency ambayo ilikuwa na jukumu mahsusi katika mkakati wa Urusi wa kuingilia uchaguzi wa Marekani mnamo mwaka 2016. Prigozhin pia anatajwa kuwa mtu wa karibu wa rais wa Urusi, Vladimir Putin.  

Wizara ya sheria ya Marekani mnamo mwezi Septemba ilisema kwamba kundi la Prigozhin pia lilijaribu kuingilia kwenye chaguzi za katikati ya muhula za mwaka jana, lakini jaribio lake hilo halikufanikiwa.

Akaunti 12 za mtandao wa kijamii wa instagram pia zimeondolewaPicha: Reuters/D. Ruvic

Kampuni ya Facebook ambayo ni mtandao mkubwa kabisa wa kijamii ulimwenguni tayari umeondoa jumla ya akaunti 66 bandia, kurasa 83 na makundi 11 pamoja na akaunti 12 za mtandao wa Instagram, ukiilenga Madagascar, Jamhuri ya Afrika ya Kati, msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Cote d'Ivore, Cameroon, Sudan na Libya.

Kwa ujumla, akaunti milioni 1.1 zilifuata moja ama kurasa zote miongoni mwa hizo zilizoondolewa huku takriban watu 1,750 walizifuatilia ama kujiunga na moja ya makundi hayo. Zaidi ya watu 32,200 pia wanatajwa kuwa walikuwa wafuasi wa moja ya akaunti hizo za Instagram.

Facebook imesema imegundua mitandao miwili kati ya mitatu ilitumika katika uchunguzi wa ndani dhidi ya  watu wenye mahusiano na Urusi walioshukiwa na kile walichokitaja "kuratibu tabia zenye mwelekeo mbaya barani Afrika." 

Kugunduliwa kwa matandao wa tatu kulitokana na uchunguzi ulioibuliwa na dokezo lilitosambazwa na shirika la ufuatiliaji kwenye masuala ya intaneti la Stanford Internet Observatory. Kulingana na shirika hilo kila mtandao ulisambaza maudhui kadhaa ambayo ni pamoja na sera za nje za Urusi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW