1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Facebook yatilia mkazo upeperushaji habari moja kwa moja

15 Mei 2019

Facebook imetangaza kutilia mkazo upeperushaji matangazo moja kwa moja ili kuzuia kuenezwa kwa habari za chuki na zinazozua hofu.

Frankreich Paris | Emmanuel Macron, Präsident & Mark Zuckerberg, CEO Facebook
Picha: Getty Images/AFP/C. Petit Tesson

Mtandao wa Facebook umetangaza kuwa utatilia mkazo uwezo wa kupeperusha matangazo moja kwa moja huku waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakijiandaa kuzindua mpango wa kimataifa wa ''Christchurch Call'' kushughulikia kuenea kwa itikadi kali katika mitandao.

Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya mtandao wa Facebook Mark Zuckerberg, amekuwa chini ya shinikizo kali tangu mwezi Machi wakati mshambuliaji alipotumia uwezo wa mtandao huo wa facebook kupeperusha matukio moja kwa moja kuonyesha mashambulizi yake dhidi ya misikiti miwili katika mji wa Christchurch nchini New zealand yaliyosababisha vifo vya watu 51.

Baadaye Ardern na Macron watatoa wito huo wa Christchurch kukabiliana na kusambaa kwa habari za chuki na zinazohusiana na masuala ya kigaidi pamoja na viongozi kutoka Uingereza, Canada, Norway, Jordan na Senegal ambao pia watakuwa mjini Paris.

Mpango huo unanuia kutoa shinikizo kwa kampuni za mitandao ya kijamii ambazo zinakabiliwa na miito zaidi kutoka kwa wanasiasa kutoka kote ulimwenguni kuzuia mitandao yao kutumiwa vibaya.

Ardern aliliambia shirika la habari la CNN kwamba ni mpango wa hatua, ni mwanzo wa jambo. Mataifa mengi tayari yametilia mkazo sheria kuanzisha faini kwa kampuni zitakazoshindwa kuondoa habari zinazotatanisha zitakapoamrishwa na maafisa wa serikali kufanya hivyo.

Ardern aliongeza kuwa lazima suluhisho lipatikane kabla ya madhara kutokea.

Kampuni za mitandao ya kijamii zinakabiliwa na miito zaidi kutoka kwa wanasiasa kutoka kote ulimwenguni kuzuia mitandao yao kutumiwa vibaya.Picha: picture alliance / empics

Mkutano huo wa kisiasa mjini Paris utaandaliwa sambamba na mpango utakaozinduliwa na Macron unaojulikana kama '' Tech for Good '' -Teknolojia kwa wema, utakaowaleta pamoja wakurugenzi 80 wa teknolojia kujadilia kuhusu jinsi ya kushirikisha teknolojia kwa faida ya kila mtu.

Wakuu wa kampuni kubwa za teknologia za Marekani, Wikipedia, Uber, Twitter, Microsoft na Google watahudhuria mkutano huo lakini Zuckerberg aliyeandaa kikao cha faragha na Macron wiki iliyopita, hatahudhuria.

Hata hivyo kampuni hiyo kubwa ya mtandao wa kijamii badala yake itawakilishwa na naibu rais wake wa masuala ya kimataifa na mawasiliano Nick Clegg aliyekuwa naibu waziri mkuu wa Uingereza.

Ardern alisema kuwa amezungumza na Zuckerberg moja kwa moja mara mbili sasa na akaunga mkono kikamilifu hatua hii.

Katika makala ya maoni katika gazeti la New York Times, Ardern alisema kuwa mashambulizi hayo dhidi ya Christchurch yalionyesha mfumo mpya wa kutishia  katika maasi yanayotokana na itikadi kali.

Ardern alisema kuwa mtandao wa kijamii wa Facebook uliondoa nakala milioni 1.5 za video katika muda wa saa 24 za mashambulizi lakini yeye binafsi alijipata miongoni mwa wale walioona video hiyo ilipocheza tena yenyewe katika mitandao yao ya kijamii.

Aliendelea kuliambia shirika hilo la CNN kwamba takriban raia elfu 8 walipiga simu kwa nambari ya dharura ya afya ya kiakili baada ya kuona video hiyo.

Katika taarifa, Facebook ilikiri kuhusu udhaifu wa mifumo yake. Naibu rais wa masuala ya maadili Rosen, alisema kuwa moja ya changamoto walizokabiliana nazo katika siku baada ya mashambulizi hayo, ni kupenya  kwa mambo tofauti katika video hiyo ya mashambulizi.

Duru za urais nchini Ufaransa zimesema kuwa wakati umewadia kwa kampuni za teknologia kujiweka katika hali ya matarajio ya  jinsi mifumo yake inavyoweza kutumika vibaya.

VYANZO: AFPE