1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fahamu zaidi kuhusu mateka wa Israel chini ya Hamas

Angela Mdungu
28 Novemba 2023

Wapiganaji wa Hamas wamewaachilia mateka kadhaa, wakiwa hasa wanawake na watoto chini ya makubaliano ya kusimamisha mapigano.

Israel | mkusanyiko wa kushinikiza kuachiwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas
Familia za mateka wanaoshikiliwa na Hamas wakifarijiana katika mkusanyiko wa kushinikiza serikali kuchukua hatua kabla ya makubaliano ya kuachiwa mateka na wafungwa kati ya Israel na HamasPicha: Mahmoud Illean/AP Photo/picture alliance

Waliwaachia huru pia wafanyakazi kwenye mashamba raia wa Thailand sambamba na wengine kadhaa wa Ufilipino baada ya mapigano kusitishwa  katika ukanda wa Gaza kwa mara ya kwanza ndani ya wiki saba.

Wapiganaji wa Hamas waliwachukua mateka karibu watu 240 na kuwauwa waengine 1,200 wakati walipoivamia Israel Oktoba 7, kwa mujibu wa serikali ya Israel.

Mateka hao walikuwa ni kutoka katika jumuiya mbalimbali na vijiji vya ujamaa na ngome za jeshi kusini mwa Israel pamoja na watu waliokuwa wakihudhuria tamasha la muziki.

Kando ya raia wa Israel,  serikali ya nchi hiyo imesema kuwa zaidi ya nusu ya mateka waliokamatwawalikuwa na uraia pacha au wa nchi nyingine kutoka karibu mataifa 40 yakiwemo Marekani, Thailand, Uingereza, Ufaransa, Argentina Ujerumani, Chile, Uhispania, na Ureno.

Soma pia:Israel na Hamas wakubaliana kuongeza muda wa kusitisha mapigano

Kulingana na vyombo vya habari vya Israel na serikali, karibu mateka 40 walikuwa ni watoto akiwemo mtoto wa miezi 10. Wengine waliotekwa nyara walikuwa wanajeshi na walemavu.

Kabla ya makubaliano ya kusitisha mapigano, Oktoba 20, Hamas iliwaachilia mateka wanne ambao ni Judith Raanan, raia wa Marekani Judith Raanan, 59, na binti yake Natalie  Raanan, mwenye miaka 17  kwa kile kundi hilo lilichokiita kuwa ni ''sababu za kiutu".

Wanawake wawili wa Kiisraeli Nurit Cooper mwenye miaka 79 na Yocheved Lifshitz, 85 waliachiliwa Oktoba 23.

Mateka aliekombolewa na vikosi vya Israel

Vikosi vya Israel vilimkomboa mateka mmoja  ambaye pia ni mwanajeshi  Ori Megidish, katika operesheni ya kijeshi ndani ya Gaza Oktoba 30.

Mapema mwanzoni mwa mwezi Novemba jeshi la nchi hiyo lilisema kuwa limeipata miili ya mateka wawili katika mji wa Gaza akiwemo mwanajeshi Noa Marciano mwenye miaka 19.

Helkopta iliowabeba mateka wa Israel waliokuwa wakishikiliwa na HamasPicha: Ohad Zwigenberg/AP/picture alliance

Kundi la Hamas limesema kuwa limewaficha mateka kwenye sehemu salama na katika mahandaki katika ukanda wa Gaza.

Israel imedai wapiganaji hao wana mtandao mkubwa wa mahandaki chini ya ardhi ambako linahifadhi silaha, vituo vya operesheni zake na linayatumia mahandaki hayo kama njia za wapiganaji wake.

Soma pia:Usitishaji vita waibua matumaini ya mateka zaidi kuachiwa

Lifshitz, kikongwe wa miaka an 85- aliyeachiliwa huru na Hamas anasema baada ya kutekwa alipelekwa katika handaki chini ya ardhi mahali alipopafananisha na mtandao wa buibui.

Israel imesema kuwa ilipata ushahidi kuwa baadhi ya mateka walifichwa ndani ya au chini ya hospitali ya  Shifa Oktoba 7.

Mfumo unaotumika kuwashikilia mateka

Akizungumzia mazingira ya mateka, Lifschitz alisema kuwa waliomteka nyara waliwatenganisha mateka katika makundi madogo madogo.

Anasema yeye na wenzake kadhaa walilala kwenye magodoro sakafuni katika mahandaki.

Aliendelea kusema kuwa madaktari walitoa huduma na Hamas ilihakikisha kuwa mazingira ni safi.

Makubaliano ya kusitisha vita Israel-Hamas kurefushwa?

02:12

This browser does not support the video element.

Soma pia:Mateka wengine 13 wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Hamas kuachiwa huru

Katika picha ya video iliyotolewa na Hamas mwezi Oktoba ilimuonesha mateka raia wa Ufaransa mwenye miaka 21 akitibiwa majeraha yake na mhudumu wa afya.

Wanafamilia na maelfu ya watu wamekuwa wakiishinikiza serikali ya Israel kutoa kipaumbele katika suala zima la kuwakomboa mateka, kwa hofu kuwa wanaweza wakauwawa kwa mashambulizi ya kulipa kisasi katika ukanda wa Gaza.

Wamekuwa pia wakisafiri huku na kule duniani kuangazia hatma ya mateka.

Baada ya awamu mbili za mateka kuachiliwa  huru, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alirudia msimamo wake wa kuwakomboa na kuwarejesha nyumbani mateka wote.

Kwa familia za mateka ambao wameshaachiliwa huru  kulikuwa na furaha iliyogubikwa na wasiwasi kwa wale ambao bado wamesalia Gaza.