Faharasa ya CPJ ya mwaka 2018
2 Novemba 2018Mshauri wa kampeni ya kinga dhidi ya ukatili unayofanyiwa waandishi habari duniani, Elisabeth Witchel amesema Somalia inaongoza kwa muda wa miaka minne mfululizo katika orodha hiyo ya nchi ambako waandishi habari wanatendewa uhalifu bila ya wahalifu hao kuadhibiwa. Nchi nyingine zilizomo katika orodha hiyo ni Afghanistan ambako mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliwalenga waandishi habari mjini Kabul na kuwaua 9 baada ya kujilipua.
Colombia pia imerejea katika faharasa hiyo baada ya wapiganaji wa msituni wanaotuhumiwa kuwa na uhusiano na wauzaji mihadarati walipowateka nyara waandishi habari wa Ecuador karibu na eneo la mpakani na kuwaua waandishi hao ndani ya Colombia. Nchi hizo mbili zilikuwa chini kwenye orodha mnamo miaka ya hivi karibuni kutokana na vitendo vya umwagaji damu kupungua.
Katika muongo mmoja uliopita, waandishi wa habari 324 wamenyamazishwa kwa njia ya mauaji duniani kote na katika asilimia 85 ya kesi hizi hakuna wahalifu waliohukumiwa. Ni ujumbe wenye nguvu kwa wale wanaotaka kuvidhibiti vyombo vya habari kwa kutumia nguvu. Zaidi ya robo tatu yaani asilimia 82 ya mauaji yamefanyika katika nchi 14 ambazo zimetajwa na tume ya CPJ kwenye orodha yake ya mwaka huu. Nchi hizo zote 14 zimejumuishwa mara kwa mara tangu shirika hilo lilipoanza kukusanya ripoti yake mnamo mwaka 2008.
Waathirika wengi ni waandishi wa habari wa ndani. Orodha hiyo inajumuisha nchi ambapo hazina utulivu kutokana na migogoro inayosababishwa na makundi ya watu wenye silaha, ukiukwaji wa haki za binadamu, pamoja na kwenye nchi ambako waandishi wa habari wanaripoti juu ya rushwa, uhalifu, siasa, biashara, na haki za binadamu wengi wao wamekuwa wanalengwa na watuhumiwa walio na uwezo wa kuzuia haki kutendekea kutokana na ushawishi wa kisiasa walionao, utajiri au wanatumia vitisho.
Katika kipindi cha miaka10 iliyopita waandishi habari wasiopungua 324 waliuliwa katika sehemu mbalimbali za dunia na katika asilimia 85 ya mikasa hiyo, wahalifu hawakuwajibishwa, hali hiyo inatoa ishara ya kuwapa kichwa wale wanaodhamiria kuchuja na kudhibiti vyombo vya habari kwa kutumia nguvu. Zaidi ya Asilimia 82 ya mikasa hiyo ilitokea katika nchi 14 zilizoorodheshwa na kamati hiyo ya kuwalinda waandishi wa habari CPJ.
Nchi hizo zote zimekuwamo katika orodha hiyo mara kadha na nusu ya hizo zimekuwamo katika orodha hiyo kila mwaka. Idadi kubwa ya waandishi habari wanaouliwa ni raia wa nchi hizo. Orodha ya CPJ inajumuisha nchi ambako ukosefu wa utulivu unaotokana na migogoro na ambako umwagaji damu unaoletwa na makundi yenye silaha umechochea hali ya kutendeka uhalifu bila ya wahalifu kuwajibishwa. Katika ripoti yake ya mwaka shirika la waandishi habari wasiokuwa na mipaka limesema, waandishi habari wanaoandika juu ya ufisadi, uhalifu, siasa, biashara na haki za binadamu wanawindwa lakini watuhumiwa wa uhalifu huo wanazo njia za kukwepa sheria kutokana na uzito wao wa kisiasa, utajiri au kutokana na kutumia vitisho.
Faharasa inayoonyesha dhulma wanayotendewa waandishi habari bila ya wahalifu kuchukuliwa hatua, huchapishwa kila mwaka kuadhimisha siku ya kimataifa leo tarahe 2 Novemba, siku ya kuhimiza juhudi za kukomesha tabia ya kutowaadhibu wanaotenda uhalifu dhidi ya waandishi habari. Kwenye orodha hiyo pia hutolewa idadi ya mauaji ambayo kesi zake hazijatatuliwa kwa kipindi cha miaka10 kwa kuzingatia idadi ya watu katika kila nchi husika. Kwa toleo hili la leo CPJ ilichunguza mauaji ya waandishi wa habari katika kila taifa yaliyofanyika kati ya Septemba 1, mwaka 2008 na Agosti 31 mwaka huu wa 2018. Nchi zilizo na matukio matano au zaidi ambayo hayajasuluhishwa kwa kipindi hicho zimejumuishwa kwenye orodha hii mpya.
Mwandishi:Zainab Aziz/CPJ's 2018 Global Impunity Index
Mhariri:Yusuf Saumu