1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona yaongeza migogoro duniani

17 Juni 2021

Viwango vya migogoro kote duniani vimeongezeka tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona. Hii ni kulingana na ripoti ya kila mwaka ya faharasi ya amani duniani iliyochapishwa Alhamisi na taasisi ya uchumi na amani.

Corona-Situation in Taiwan
Picha: Ceng Shou Yi/picture alliance

Ripoti hiyo, inayotathmini hali ya mwaka 2020, inaonyesha kwamba mizozo imeongezeka ulimwenguni kwa mara ya tisa katika muda wa miaka 12. Mwanzilishi wa taasisi hiyo, Steve Killelea, amesema kuwa janga hilo limechangia hali hiyo. Killelea amesema kuwa ijapokuwa viwango jumla vya migogoro na ugaidi vilipungua katika mwaka 2020, hali ya kuyumba kisiasa na maandamano ya vurugu yameongezeka. Amesema kuwa athari ya kiuchumi inayotokana na janga hilo itasababisha hali ya kutokuwa na uhakika hasa katika mataifa ambayo tayari yamekuwa yakikabiliwa na changamoto kabla ya janga hilo. Killelea pia ameongeza kuwa kuimarika kiuchumi hakutakuwa kwa usawa hali ambayo huenda ikasababisha migawanyiko zaidi.

Kwa ujumla, faharasi ya amani duniani imerekodi zaidi ya matukio elfu 5 ya ghasia zinazohusiana na janga la virusi vya corona kati ya mwezi Januari mwaka 2020 na Aprili mwaka huu. Mataifa 25 yalishuhudia idadi kubwa ya maandamano ya vurugu huku mataifa manane pekee yakiimarika katika orodha hiyo. Hali ilikuwa mbaya zaidi katika mataifa ya Belarus, Myanmar na Urusi ambapo mamlaka za nchi hizo zilifanya msako wa kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji.

Msako wa kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji MyanmarPicha: AP/picture alliance

Sababu nyingine zilizochangia kuongezeka kwa ghasia

Machafuko ya kijamii pia yaliongezeka kwa kiwango kikubwa nchini Marekani wakati wa kipindi hicho kilichofanyiwa tathmini lakini sio tu kwasababu ya janga la virusi vya corona lakini kwa sehemu kutokana na harakati za vuguvugu lililokuwa linakuwa kwa kasi la Black Lives Matter pamoja na kuvamiwa kwa majengo ya bunge ya Marekani mjini Washington mnamo mwezi Januari.

Kwa upande mwingine, kiwango cha mauaji, vifo kutokana na ugaidi na mtazamo wa uhalifu kilipungua sana katika maeneo mengi duniani ingawa hali hiyo ilitofautiana sana kutoka eneo moja hadi lingine. Nchini Afghanistan, Brazil, Afrika Kusini na Mexico, kwa mfano, zaidi ya nusu ya idadi ya watu waliendelea kutaja ghasia kama tishio kubwa zaidi kwa usalama wao katika maisha yao ya kila siku. Taasisi hiyo ya uchumi na amani inasema kuwa faharasi ya amani dunia inashughulikia asilimia 99.7 ya idadi ya watu duniani na inatathmini hali ilivyo kwa kutumia viashiria 23 vya ubora na upimaji vilivyoorodheshwa katika maeneo matatu ambayo ni migogoro inayoendelea, usalama na shughuli za kijeshi.

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW