1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fainali kabla ya fainali; Nani mkali PSG ama Bayern?

28 Aprili 2026

PSG na Bayern wanakutana Paris kwa pambano la kusisimua, huku Atletico na Arsenal wakijiandaa kwa vita kali Madrid. Ni safari ya hadithi mpya kuelekea fainali ya Ulaya.

Champions League 2025/26 | Viertelfinale | Bayern München vs. Real Madrid | Olise erzielt das 4:3
Picha: Tom Weller/dpa/picture alliance

Nusu fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inang'oa nanga usiku wa leo, ikifungua ukurasa mpya wa hadithi mbili tofauti lakini zenye msisimko mkubwa barani Ulaya. Mabingwa watetezi Paris Saint‑Germain wanawakaribisha Bayern Munich jijini Paris, kisha kesho Jumatano Atletico Madrid watawakaribisha Arsenal katika dimba la Metropolitano. 

Usiku wa leo macho yote yatakuwa Parc des Princes, ambako PSG wanaikaribisha Bayern Munich katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali. Kocha Luis Enrique anaingia kwenye mchezo huu akiwa na kikosi kamili na ari ya hali ya juu baada ya timu yake kushinda mechi nane kati ya tisa zilizopita.

Mabingwa hao watetezi wameonyesha ubora mkubwa Ulaya msimu huu, wakiitoa Monaco, Chelsea na Liverpool katika hatua za mtoano. Kocha Enrique anaamini timu yake iko katika kiwango cha juu zaidi, akisisitiza kuwa "hakuna timu iliyo bora kuiliko hasa kwa kile walichokionyesha kufikia sasa.”

"Ukifika hatua hii, mambo madogo yatakuwa muhimu, na lazima uwe tayari kwa hali yoyote itakayokukumba. Tunastahili kuwa hapa, na tuna imani, lakini wakati huo huo tunaelewa ugumu wa kucheza dhidi ya Bayern.” Alisema Enrique.

Upande wa Bayern Munich, wanakuja wakiwa na rekodi ya kuvutia, baada ya kutwaa ubingwa wa Bundesliga na kulenga kutwaa mataji matatu msimu huu. Hata hivyo, Kompany hatakuwepo benchi kutokana na adhabu ya kusimamishwa mechi moja. Bayern wanajiamini zaidi baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya PSG katika hatua ya makundi mapema msimu huu.

"Kwa hiyo, ninakaa wapi? Mahali fulani uwanjani, ingawa labda si mbali sana na wao, lakini bado sijazoea uwanja huu. Najua suluhisho liko wapi kwa mtu ambaye hawezi kuwepo. Lakini tuna utaratibu, uko wazi. Najua ni muda gani ninaweza kuruhusiwa kufanya nini, na jinsi ninavyoweza kuisaidia timu. Lakini najua kwamba nimesimamishwa.” Alisema Kompany.

Miamba ya soka Ulaya kupambana katika ligi ya mabingwa.Picha: Adrian Dennis/AFP

Wachezaji muhimu watachukua nafasi kubwa katika mchezo huu, akiwemo mshambuliaji hatari Harry Kane ambaye tayari amefunga mabao 53 msimu huu, pamoja na winga Michael Olise. PSG nao wanategemea ubunifu wa viungo wao na mshikamano wa kikosi chao kuhakikisha wanapata matokeo chanya nyumbani.

Vipi Arsenal na Athletico Madrid?

Kesho Jumatano, macho yatahamia Madrid ambako Atletico Madrid watakuwa wenyeji wa Arsenal katika nusu fainali ya pili. Kocha Diego Simeone anatafuta kurejesha heshima ya timu yake baada ya kupoteza fainali ya Copa del Rey.

Atletico hawajawahi kushinda taji hili kubwa la Ulaya, lakini wanapata motisha kutoka kwa mashabiki wao wenye shauku kubwa. Mshambuliaji Julian Alvarez amesisitiza kuwa timu iko tayari kupambana kwa nguvu zote ili kufikia fainali. Wachezaji wengine kama Antoine Griezmann wanatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mchezo huo muhimu.

Kwa upande wa Arsenal, safari yao ya Ulaya imejaa matumaini mapya. Kocha Mikel Arteta anatafuta kuiongoza timu yake kufika fainali kwa mara ya pili katika historia ya klabu. Kiungo Declan Rice amewataka wachezaji wenzake kukumbatia uzito wa historia na kupambana bila woga, akisema uzoefu wa misimu ya karibuni umewajenga kisaikolojia.

Hata hivyo, kuna wasiwasi kuhusu ubora wa Eberechi Eze na Kai Havertz baada ya kupata majeraha katika mchezo uliopita. Eze, ambaye amekuwa chanzo cha ubunifu msimu huu, anaweza kuwa pigo kubwa iwapo hatakuwa tayari.

Kwa ujumla, nusu fainali za mwaka huu zimejaa msisimko, ushindani na hadithi za kipekee, huku kila timu ikipigania nafasi ya kucheza fainali na kuandika historia mpya katika soka la Ulaya. Mashabiki duniani kote wanasubiri kwa hamu kuona nani ataibuka mshindi na kusonga mbele kuelekea taji la heshima zaidi barani Ulaya.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW