1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fainali za kombe la dunia 2018 zakurubia kumalizika Urusi

Oumilkheir Hamidou
15 Julai 2018

Kinyang'anyiro cha kuania kombe la dunia mwaka 2018 kitakamilika leo usiku huku rais wa Urusi Vladimir Putin akitekeleza ahadi aliyotoa ya kuhakikisha kila kitu kinapita salama na kuipatia sifa nzuri kabisa Urusi

Russland Luzhniki-Stadion
Picha: Getty Images/AFP/D. Serebryakov

Hakuna anaeweza kukanusha: maandalizi ya kombe la dunia la dimba mwaka 2018 yanafana. Viwanja  kabambe vya michezo, mashabiki wacheshi, hakuna tukio lolote baya lililoripotiwa. Hofu za visa vya kibaguzi, matumizi ya nguvu na mivutano ya kidiplomasia zilizokuwa zimeenea zimetoweka  tangu michuano hiyo ilipoanza. Lilikuwa tukio la kufurahisha kwa wageni kutoka nje wageni  ambao kwa mujibu wa shirikisho la kimataifa la kabumbu FIFA walipindukia watu milioni moja.

Mashabiki kutoka kila pembe ya dunia waliteremka majiani mjini Moscow na katika miji mengine ya michuano huku mashabiki kutoka nchi za Amerika ya kusini wakimiminika kwa wingi zaidi.

Mashabiki kutoka nchi za magharibi hawakuwa wengi sana, kutokana na sababu nyingi tuu, ikiwa ni pamoja na uhusiano dhaifu wa kidiplomasia pamoja na Urusi. Lakini mashabiki wa Uingereza walikuwa miongoni mwa wazungu waliofika kwa wingi nchini michuano ya kombe la dunia ilipoelekea awamu ya mwisho, walipoamini timu yao ina nafasi ya kutimka hadi mwisho.

 Sifa kem kem kwa Maandalizi na mapokezi mazuri

Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenyekiti wa FIFA InfantinoPicha: picture alliance / dpa

Wakitishwa na ripoti eti wangeandamwa na makundi ya wafanyafujo, wote wamejionea sura tofauti kabisa ya Urusi na wengi wao wataondoka wakiwa na maoni sawa na yale ya kocha wao: "Maaandalizi ya mashindano yalifana kupita kiasi, tumepokelewa vizuri katika kila mji wa  Urusi tuliokwenda" amesema Gareth Southgate baada ya timu yake kushindwa mbili bila na Ubeligiji katika kinyang'anyiro cha kuania nafasi ya tatu mjini Saint Petersburg.

Mwenyekiti wa shirikisho la kabumbu ulimwenguni-FIFA, Gianni Infantino amefika hadi ya kusema "mashindano ya kombe la dunia mwaka 2018 yamefana kupita yote mengine".

"Sote tunavutiwa na kuipenda Urusi, tumegundua nchi ambayo hatukuwa tukiijua" alisema Gianni Infantino alipokuwa ziarani Kremlin .Yote hayo ni malengo aliyokuwa amejiwekea tangu mwanzo rais Vladimir Putin  "Ameongeza kusema.

Maajabu ya mpira wa duara yameshuhudiwa

Maelfu ya mashabiki walijazana viwanjaniPicha: DW/E. Barysheva

Licha ya sifa za maandalizi mazuri kupita kiasi na mapokezi mazuri, magoli hayakuwa mengi ikilinganishwa na fainali za kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil. Magoli 163 yamepachikwa  kabla ya fainali leo jioni ikilinganishwa na jumla ya magoli 171 mwaka 2014. Pambano moja tu lakini ndilo lililomalizika bila ya goli, nalo ni lile kati ya Ufaransa na Danemark.

Hofu za awali kuhusu kuanzishwa marifu wanaofuatilizia michuano kupitia kanda ya video zimedhihirika hazikuwa na msingi.

Kilichosisimua zaidi  ni jinsi Croatia ilivyofanikiwa kuingia fainali na pia jinsi vilabu vilivyokuwa vikipigiwa upatu  mfano wa Ujerumani, Uhispania na Argentina vilivyopigwa kumbo hali inayodhihirisha jinsi dimba linavyoweza kuzusha maajabu.

Maajabu yanasubiriwa magharibi ya leo pambano la fainali kati ya Ufaransa na Croatia litakapomalizika mjini Moscow. Ufaransa inapania kunyakua nyota ya pili baada ya ile ya mwaka 1998 huku Croatia ikijiandaa kunyakua nyota yake ya kwanza katika historia yake ya dimba la kimataifa. Pindi wakishinda  watawapa matumaini timu ndogo ndogo zinazojiandaa kwa kombe la dunia la mwaka 2022 nchini Qatar.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri:Bruce Amani

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW