Fainali za kombe la dunia zatimua vumbi Afrika kusini
12 Juni 2010Fainali za kwanza za kombe la FIFA la dunia kufanyika katika ardhi ya bara la Afrika zimeanza kwa kishindo wakati wenyeji wa mashindano hayo Afrika kusini ikiionyesha dunia sherehe za kupendeza za ufunguzi na kisha kuwapa burudani safi mashabiki wa kandanda duniani kwa kutoka sare na Mexico kwa bao 1-1.
Afrika kusini inaonekana kuwa timu dhaifu sana kuwahi kuwa mwenyeji wa kombe la dunia. Lakini walionyesha kandanda safi na kuwanyima Mexico ushindi katika mchezo wa kwanza wa kundi A. Wamexico wakiwa wanamiliki kwa kiasi kikubwa mpira uwanjani, Tshabalala alipachika bao mchezo ukiwa katika dakika ya 55. Lakini Mexico walipata bao la kusawazisha lililowekwa wavuni na Rafael Marquez katika dakika ya 79.
Katika mchezo wa pili Ufaransa ilishindwa kuonyesha ubabe wake kwa mara nyingine tena wakati walipolazimishwa sare ya bila kufungana na Uruguay katika mchezo wa kundi A. Wakati mchezo huo haukuwa kama ilivyokuwa katika fainali za kombe la dunia mwaka 2002, wakati ikiwa kama mabingwa watetezi ilikomewa bao 1-0 na Senegal na hata kushindwa kuvuka duru ya kwanza, sare hiyo pamoja na mchezo wao utapokelewa kwa furaha na mahasimu wao katika mchezo ujao Mexico.
Jioni ya leo kutakuwa na mapambano matatu. Uingereza inashuka uwanjani kuonyeshana kazi na Marekani, US Boys, wakati Nigeria ina miadi na Argentina. Ugiriki itakwaana na Korea ya kusini.
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ameiambia timu ya nchi hiyo , The Green Eagles kuwa mfanyabiasha mmoja ameahidi kitita cha dola milioni moja iwapo watashinda pambano lao dhidi ya Argentina ya Diego Armando Maradona.
Rais Goodluck amewaambia wachezaji hao katika hoteli yao mjini Johannesburg, kuwa mfanyabiashara Michael Adenuga amekubali kuwalipa kitita hicho iwapo wataigaragaza Argentina.
Rais Goodluck kisha akawaambia Super Eagles kuwa washinde kombe hilo kwa ajili ya Afrika.
Wayne Rooney mi lazima azimwe ili Marekani iweze kuwa na nafasi ya aina yoyote ya kupata ushindi dhidi ya Uingereza katika mchezo wao utakaofanyika leo, amesema kocha wa timu ya US Boys Bob Bradley.
Alipoulizwa iwapo mshambuliaji huyo nyota wa Uingereza anapaswa kuzimwa ndipo Wamarekani waweze kushinda , Bradley amesema anafikiri hivyo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / AFPE/DPAE/RTRE
Mhariri: Munira Muhammad