Miezi mitatu baadae, familia Tanzania bado zinasubiri miili
28 Januari 2026
Manenos Selanyika, mwandishi wa habari mwenye umri wa miaka 40, ni miongoni mwa waliopoteza maisha katika vurugu hizo. Kwa mujibu wa majirani waliyozungumza na familia yake, Selanyika alipigwa risasi na vikosi vya usalama tarehe 30 Oktoba, alipokuwa akitafuta chakula wakati maandamano yalipokuwa yakiendelea jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, juhudi za familia yake kuuchukua mwili wake zilikwamishwa na polisi.
Familia ilimtafuta katika hospitali kadhaa bila mafanikio, na baada ya zaidi ya wiki moja bila taarifa yoyote rasmi, walilazimika kufanya mazishi ya kiishara katika kijiji cha Lambo, karibu na Mlima Kilimanjaro.
Mashirika ya haki za binadamu yanasema mamia ya familia nchini Tanzania ziko katika hali kama hiyo, huku serikali ikikabiliwa na tuhuma za kuwazika waathirika wa ghasia katika makaburi ya pamoja kwa siri—madai ambayo serikali imeyakanusha vikali.
Madai ya mauaji, ghasia na ukimya wa serikali
Vurugu hizo zilichochewa na kufungiwa kwa wagombea wa upinzani pamoja na madai ya mauaji na utekaji wa wakosoaji wa serikali. Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi wa urais kwa asilimia 98 ya kura, baada ya siku tano za ghasia ambazo upinzani unadai zilisababisha vifo vya takribani watu elfu mbili, huku huduma za mtandao zikiwa zimezimwa kote nchini.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Rais Samia aligusia vurugu za baada ya uchaguzi bila kutaja idadi ya waliouawa.
"Kwa washirika wetu katika jumuiya ya kidiplomasia na wageni wanaoishi hapa Tanzania, natoa pole zangu za dhati kwa hali ya kutokuwa na uhakika, usumbufu wa huduma, na kuzimwa kwa intaneti. Tunatambua changamoto za machafuko na vurugu zilizojitokeza siku ya uchaguzi na muda mfupi baada ya hapo. Hatua tulizochukua zilikuwa muhimu ili kulinda utaratibu wa kikatiba na kuhakikisha usalama wa wananchi wote pamoja na jumuiya ya kidiplomasia,” alisema Rais Samia.
Hata hivyo, serikali haijatoa takwimu rasmi za vifo. Shirika la habari la AFP, lililoripoti matukio haya, limesema serikali haikujibu maswali yaliyowasilishwa kuhusiana na madai hayo.
Familia zasalia gizani, waandishi wakandamizwa
Katika tukio jingine, mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Sheila Gyumi—jina ambalo si lake halisi—alisema mume wake, aliyekuwa dereva wa bodaboda, alitoweka siku ya uchaguzi alipokwenda kazini kama kawaida. Hadi sasa, familia haijui alipo, hali iliyomwacha mjane huyo akihangaika kugharamia kodi ya nyumba na ada ya shule ya mtoto wao.
Daktari mmoja katika hospitali kubwa jijini Dar es Salaam aliwahi kuiambia AFP kuwa mamia ya miili ilichukuliwa kutoka mochwari na maafisa wa usalama wakati wa kilele cha machafuko. Uchunguzi wa shirika huru la Centre for Information Resilience umeonyesha dalili za matumizi ya risasi za moto na uwezekano wa kuwepo kwa makaburi ya pamoja kupitia uchambuzi wa picha za satelaiti.
Wakati hayo yakijiri, waandishi wa habari walikabiliwa na vikwazo vikubwa. Waandishi wa kigeni walizuiwa kuripoti uchaguzi, huku waandishi wa ndani wakiamriwa kutochapisha taarifa kuhusu machafuko. Kwa mfano, mwandishi wa Millard Ayo TV, Godfrey Thomas, alishtakiwa kwa kosa la uhaini kwa kuripoti maandamano hayo.
Licha ya serikali kuahidi kufanya uchunguzi, imeendelea kupunguza uzito wa madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi. Kwa familia nyingi kama ya Manenos Selanyika, maisha yanaendelea katika maumivu ya kutokujua hatima ya wapendwa wao, huku matumaini ya kupata ukweli yakizidi kufifia.