1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Familia ya Ukingo wa Magharibi haina matumaini ya haki

5 Desemba 2023

Moussa ana umri wa miaka minane. Katika kwa muda wa mwezi mmoja uliopita, mvulana huyu anayeishi katika Ukingo wa Magharibi, ana mchezo mpya, "Kujifanya baba hajafa." Lakini babake, Bilal Saleh, aliuawa Oktoba 28

Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wakisherehekea uvamizi wa kushtukiza wa kundi la wanamgambo la Hamas nchini Israel mnamo Oktoba 7, 2023
Wapalestina katika Ukingo wa MagharibiPicha: Jaafar Ashtiyeh/AFP/Getty Images

Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 40 alipigwa risasi kifuani alipokuwa akichuma mizeituni na familia yake karibu na nyumba yake katika kijiji cha As-Sawiyah. Saleh ni mmoja wa zaidi ya Wapalestina 250 waliouawa na wanajeshi wa Israel na walowezi katika Ukingo wa Magharibi. Hii ni kulingana na takwimu za serikali ya Palestina, tangu shambulio la Hamas mnamo Oktoba 7 lililosababisha kuzuka kwa vita vipya na Israeli. ''Alikuwa mtu wa kawaida na aliyependa sana shamba lake,'' anasema mjane wake Ikhlas huku akionesha picha katika simu yake ya Saleh akiwa shambani, akisoma Koran tukufu na akiwa na Moussa katika harusi. Mjane huyo anajitahidi sana kuangalia picha hiyo mbali na kuelezea yalioyotokea.

Video zilionesha wanaume wanaoaminika kumuuwa Saleh

Video kutoka eneo la tukio zinaonesha wanaume wanne wakiwa wamevalia nguo zilizofumwa ambazo ni maarufu miongoni mwa walowezi wa Israel, wakipiga kelele kuelekea katika eneo walilokuwa familia hiyo walipokuwa wakivuna. Mmoja alikuwa amejihami kwa bunduki. Familia hiyo inaonekana kukimbia lakini Saleh aliyekuwa amesahau simu yake alirudi kuichukuwa. Dakika chache baadaye, mlio wa risasi ulisikika. Familia hiyo ilirudi kungalia kilichotokea na kumpata Saleh akitokwa na damu kifuani. Alipelekwa hospitalini umbali wa kilomita 10 lakini akathibitishwa kufariki muda mfupi baadaye.

Mwanamume aliyekamatwa kwa mauaji aachiwa huru

Familia hiyo inasema kuwa kaka na baba yake Ikhla, waliona kupitia mitandao ya kijamii kwamba mwanamume mmoja alikamatwa kuhusiana na mauaji hayo lakini akaachiwa huru saa chache baadaye.

Maafisa wa polisi wa Israel wakifunga eneo la Israel lililovamiwaPicha: Ohad Zwigenberg/AP Photo/picture alliance

Polisi na taasisi ya wizara ya ulinzi ya Israel inayosimamia shughuli za raia katika maeneo ya Kipalestina haikujibu maombi kadhaa ya tamko kutoka kwa shirika la habari la AFP.

Soma pia: Israel yazingira maeneo ya Jerusalem Mashariki

Siku chache baadaye bila ya kufahamu kwanini, Ikhlas alitakiwa kufika katika kituo cha polisi mjini Ariel, ambapo maafisa wa polisi walimtaka aeleze alichokiona. Ikhlas ameliarifu shirika la habari la AFP kwamba katika lango, wakati mlinzi alipokuwa akikagua vitambulisho vyake, mlowezi mmoja aliwasili kwa gari katika eneo hilo na alipomuona kuwa amevalia hijabu, alishukisha kioo chake cha gari na kumtemea mate. Ikhlas amesema, '' baada ya hilo, sioni ni aina gani ya haki wanaweza kutupa.''

Soma pia: Israel yapunguza vikwazo kwa Palestina mwezi wa Ramadhan

Kundi la haki za binadamu la Israeli Yesh Din, lilimshawishi Ikhlas kuwasilisha malalamishi ijapokuwa linasema kuwa utafiti kuhusu kesi za vurugu dhidi ya walowezi kati ya mwaka 2005 na 2021, unaonesha kuwa asilimia 92 ya kesi hizo zilifutiliwa mbali na mamlaka za Israel.

Mkazi wa Ukingo wa Magharibi aleezea madhila wanayopitia

Takriban Wapalestina milioni 3 wanaishi katika Ukingo wa Magharibi ambao umekaliwa na walowezi wa Israel tangu mwaka 1967.

'' Kwa muda wa miaka 10 iliyopita, hali imezidi kuwa ngumu,'' amesema Hazem Saleh, shemejiye Bilal. " Tunashambuliwa, ardhi yetu inanyakuliwa na makazi kujengwa. Wana nguvu, wanaweza kufanya kile wanachotaka.'' ameongeza Hazem.

lakini Hazem anasema hali imekuwa ngumu zaidi tangu kundi la wanamgambo la Hamas lilipofanya mashambulizi ya kushtukiza Kusini mwa Isreal na kuwauwa takriban watu 1,200 wengi wao wakiwa raia na kuwashika mateka takriban watu 240, kwa mujibu wa maafisa wa Israel.

     

     

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW