1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Familia za waliokuwa watumwa Nigeria zapinga ubaguzi

2 Julai 2020

Kizazi cha watumwa nchini Nigeria kinatarajia kuwa maandamano ya kutetea maisha ya watu weusi ''Black Lives Matter'' yatakomesha ubaguzi dhidi yao. Nchini humo kizazi za watumwa hakiruhusiwi kuchukuwa nafasi za uongozi.

Kumbukumbu ya George Floyd
Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com/A. Vaishnav

Barack Obama alipochaguliwa kuwa rais wa kwanza mweusi kuiongoza Marekani mwaka 2008, Antony Uzoije alishuhudia kupungua kwa unyanyapaa kwenye kizazi cha watumwa, jamii alikotokea huko kusini mashariki mwa Nigeria.

Uzoije, kutoka jamii ya Ogbaru kwenye jimbo la Anambra, anategemea kwamba maandamano ya hivi sasa ya ''Black Lives Matter'' kote duniani kufuatia wimbi la hasira lililochochewa na mauaji ya Mmarekani Mweusi, George Floyd mwezi uliopita akiwa mikononi mwa polisi wa Minneapolis, Marekani yataleta mageuzi pia kwa watu wa kabila la Igbo, mojawapo ya makundi makubwa ya kikabila barani Afrika, ambao walibaguliwa wakati wa biashara ya watumwa.

Ubaguzi bado upo miongoni mwa Waafrika wenyewe

Watu wa kabila la Igbo wanakadiriwa kuwa baina ya asilimia 10 hadi 20, sawa na milioni kadhaa ya watu, ni kutoka kizazi cha watumwa na wanakumbwa na ubaguzi, jambo ambalo lilisababisha machafuko ya miaka ya hivi karibuni kwenye baadhi ya maeneo ya Nigeria. Sheria na tamaduni haziwaruhusu kushika nafasi za uongozi wa jadi au kuwaoa watu kutoka jamii za walio huru.

''Watu walianza kuona kwamba ikiwa mzungu anaruhusu Obama kuwa rais, vipi kutomruhusu ndugu yako mweusi kuchukuwa nafasi fulani ya uongozi'', aliuliza Anthony Uzoije, mwenye umri wa miaka 67. Wakati watu hapa wanaona kwamba kuna usawa baina ya mzungu na mtu mweusi huko Marekani, itachangia pia kubadili hisia zao kuhusu jinsi wanavyowatendea ndugu zao weusi.

Picha: picture-alliance/dpa/H. Dridi

Utawala wa ukoloni kutoka Uigereza ulikomesha utumwa nchini Nigeria mapema katika ya karne ya 20 na kuumaliza mnamo miaka ya 1940 na 1950, lakini vizazi vya watumwa viliendelea kunyanyapaliwa kama babu zao. Ubaguzi unaendelea sio tu dhidi ya kizazi cha watumwa kusini mashariki mwa Nigeria, lakini pia kwenye nchi nyingine barani Afrika zikiwemo Ghana, Senegal na Benin.

Sheria hazifanyi kazi

Licha ya kwamba hakuna takwimu kuhusu idadi ya watumwa nchini Nigeria na kwengineko Afrika, lakini jamii hufahamu historia na ukoo wa kila familia na ni vigumu kuficha. Sheria za kupingana na ubaguzi zipo nchini Nigeria na mwaka 1956, wabunge walipitisha sheria inayopinga ubaguzi dhidi ya kizazi cha watumwa.

Lakini sheria hizo ni vigumu kuzitekeleza hasa zaidi kwenye jamii ambako watu hawafuati katiba na wanatekeleza zaidi kanuni na desturi za jadi. Oge Maduagwu, mwenye umri wa miaka 44, miaka mitatu iliyopita alitembelea jamii tofauti za kusini mashariki mwa Nigeria ili kutetea usawa wa haki za vizazi vya watumwa. Kutokana na vuguvugu la maandamano ya Maisha ya Mtu Mweusi ni Muhimu, anategemea kwamba wahusika wa ubaguzi nchini Nigeria na kwingineko barani Afrika watabadili misimamo yao na kutakuweko na idadi kubwa ya Waafrika ambao wataendesha vita vya kupambana na ubaguzi katika nchi zao wenyewe.

Kampeni ya Maduagwu ilianza kutokana na kutokuweko na ndoa za watu kutoka vizazi vya watumwa. Yeye mwenyewe sio kutoka jamii hiyo, lakini alishuhudia ubaguzi mkubwa kwenye miji ya Oguta na Imo katika jimbo la kusini mashariki mwa Nigeria. Na kuamua kukomesha hali hiyo, wakati rafiki yake alipokatazwa kuolewa na mpenzi wake kwa sababu anatoka jamii ya watumwa. Mwanaharakati huyo tayari amefanikiwa kuwashawishi baadhi ya viongozi wa jadi ambao walitangaza kukomesha ubaguzi dhidi ya vizazi vya watumwa.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo

Mhariri: Grace Patricia Kabogo