Kupungua kwa uhai anuai kunahatarisha upatikanaji wa chakula
22 Februari 2019Ripoti hiyo ya shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo duniani FAO iliyotolewa Ijumaa inaeleza kwamba idadi kubwa ya watu wanategemea aina za vyakula vya aina moja katika mahitaji yao ya lishe. Ripoti hiyo imetaja kwamba uharibifu wa viumbe hai unachangia pakubwa matatizo katika mifumo ya uzalishaji wa chakula, kama vile mazao kuathiriwa na magonjwa, ukame, kuleta wadudu wanaoshambulia mimea, pamoja na hali mbaya ya hewa inayohusishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Huku kukiwa na aina zipatazo 6,000 za mimea zinazoweza kutumika kwa ajili ya chakula, aina zisizopungua 200 za chakula ndizo zinazoliwa zaidi na tisa kati ya hizo ndio mazao yanayozalishwa kwenye maeneo mengi zaidi duniani.
Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo la FAO Jose Graziano da Silva amesema kuendelea kupungua kwa viumbe hai kunadhoofisha kwa kiwango kikubwa uwezo wa binadamu wa kutosheleza mahitaji ya chakula kwa watu ambao wanazidi kuongezeka. Da Silva amesema watu wanapaswa kutumia uhai anuai katika mpangilio endelevu kuzikabili changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi ili waweze kuzalisha chakula bila ya kuharibu mazingira.
Mkurugenzi huyo wa shirika la kilimo na chakula la Umoja wa Mataifa amesema uhai wa viumbe mbalimbali unahatarishwa na kuchafuliwa kwa mazingira, matumizi mabaya ya ardhi, ufujaji wa maji na uvunaji wa mazao wa kupita kiasi.
Naye rais wa Rais wa umoja wa shirika la mapinduzi ya kilimo lenye makao yake mjini Nairobi bi Agnes Kalibata amesema usalama wa chakula ni jambo linalotia wasiwasi katika maeneo mengi barani Afrika.
Bi Kalibata amesema kuhakikisha upatikanaji wa chakula ni muhimu kwa sababu hayo ni mahitaji ya kimsingi, pia ni nyanja mojawapo muhimu ya uchumi. Ameongeza kusema kwamba ni vigumu kwa jamii kuwekeza katika mambo mengine ikiwa uhakika wa chakula siyo imara kwa sababu binadamu anahitaji mambo hayo matatu muhimu sana ili kuweza kuishi pamoja na kuepusha migogoro.
Shirika hilo la Umoja wa mapinduzi ya kilimo linakusudia kuboresha tija ya kilimo kwa kutumia mbinu za kuongeza mazao kwa kutumia maeneo madogo ya ardhi. Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umesema uzalishaji wa chakula unapaswa kujumuisha aina mbalimbali za viumbe vinavyoweza kuhimili hali mbaya ya hewa na magonjwa ili kukidhi mahitaji ya chakula.
Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/p.dw.com/p/3DpbY
Mhariri: Caro Robi