1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FARC watangaza kusitisha vita Colombia

Admin.WagnerD18 Desemba 2014

Kundi kubwa zaidi la waasi nchini Colombia la FARC limetangaza usitishaji mapigano wa upande mmoja usiyo na kikomo, katika mgogoro huo wa miaka 50, kufuatia duru nyingine ya mazungumzo ya amani.

Kolumbien ELN Rebellen Guerilla
Picha: STR/AFP/Getty Images

Kundi la Revolutionery Armed Forces of Colombia FARC, lilitoa tangazo la kusitisha mapigano kwa muda usiyo na kikomo nchini Cuba mwishoni mwa duru nyingine ya mazungumzo ya amani yanayolenga kumaliza uasi wa muda mrefu zaidi katika bara la Amerika ya Kusini.

"Kwa kuwa tunaamini kwamba tumeanzisha njia halisi kuelekea amani pamoja na mchakato wake, tumeazimia kutangaza usitishaji mapigano wa upande mmoja na kukomesha uhasama wote kwa muda usiyojulikana, ambao unapaswa kupelekea mapatano ya kusitisha vita," alisema Ivan Marquez, mwakilishi wa FARC katika mazungumzo ya mjini Havana.

Kamanda wa FARC Ivan Marquez akitangaza usitishaji mapigano wa upande mmoja mjini Havana, Cuba.Picha: Yamil Lage/AFP/Getty Images

CELAC,CICR, ICRC kusimamia mchakato

Alisema ili hatua hiyo ifanikiwe kikamilifu, wanategemea usimamizi wa muungano wa mataifa ya Amerika Kusini, Jumuiya ya mataifa ya Amerika na Caribbean, Shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundi na ngao pana ya amani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya kundi hilo, usitishaji huo mapigano utaanza kutekelezwa dakika moja baada ya saa sita usiku Jumamosi hii ya tarehe 20 Desemba.

Waasi hao wamekuwa wakitoa wito wa usitishaji mapigano wa pande mbili kama sehemu ya mchakato wa amani unaoendelea, lakini rais Santos, ambaye ametoa kipaumbele kwa mazungumzo ya amani amekataa matakwa hayo, akisema waasi wanaweza kutumia fursa ya makubaliano kujipanga upya na kurefusha zaidi mgogoro.

Mtego kwa serikali ya Juan Manuel

Hata hivyo, tangazo la jana la FARC litaiwekea shinikizo serikali ya Colombia kuchukuwa hatua sawa, alisema mtaalamu wa siasa Jorge Restrepo, anaeongoza kituo cha uchambuzi wa migogoro cha Colombia. Ingawa FARC wamekuwa wakitangaza usitishaji mapigano kuelekea siku kuu ya Krismasi, hii itakuwa mara ya kwanza wamekubali kuweka chini silaha kwa muda usiyo na kikomo tangu miaka ya 1980.

Mazungumzo hayo yalikuwa yamekwama kufuatia mgogoro uliyosababishwa na kutekwa kwa jenerali wa jeshi Ruben Dario Alzate Novemba 16. FARC ilitetea hatua yake ya kumteka Jenerali huyo kama kitendo halali cha kivita, lakini ilimuachia Novemba 30 ili kuunusuru mchakato wa amani.

Jenerali Ruben Dario Alzate ambaye kutekwa kwake na FARC kulivuruga mchakato wa amani.Picha: picture alliance/ZUMA Press/Jhon Paz

Kama moja ya masharti ya kuanzisha upya majadiliano, pande mbili zilikubaliana kuweka mfumo wa kudumu wa kutatua migogoro inayojitokeza usoni, ambao utasimamiwa na Cuba na Norway, mataifa mawili yanaoongoza juhudi za amani.

Mazungumzo ya matumaini zaidi

Mazungumzo hayo yaliyodumu miaka miwili katika mji mkuu wa Cuba Havana, ndiyo juhudi ya matumaini zaidi kukomesha mgogoro huo wa miongo mitano, ambao umeshindwa kutatuliwa na juhudi zote za nyuma.

Mpaka sasa majadiliano yamezaa makubaliano kuhusu mageuzi ya sera ya ardhi, mapambano dhidi ya usafirishaji madawa ambao umechochea mgogoro huo, na ushirikishwaji wa waasi kisiasa.

Mgogoro huo umesababisha vifo vya zaidi ya watu 220,000 and zaidi ya milioni 5.3 wameyakimbia makaazi yao tangu FARC ilipoanzishwa kufuatia uasi wa wakulima mwaka 1964.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,ape
Mhariri: Saumu Yusuf

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW