1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fatah na Hamas wazungumzia umoja

6 Mei 2014

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Wapalestina amekuwa na mazungumzo yaliotajwa kuwa mazuri na kiongozi wa Hamas Khaled Meshaal katika mkutano wa kwanza tokea makundi yao hasimu yaliposaini makubaliano ya kuungana.

Rais Mahmoud Abbas (kulia) na Kiongozi wa Hamas Khaled Meshaal (kushioto) mjini Doha. (05.05.2014)
Rais Mahmoud Abbas (kulia) na Kiongozi wa Hamas Khaled Meshaal (kushioto) mjini Doha. (05.05.2014)Picha: reuters

Afisa mwandamizi wa Wapalestina ameliambia shirika la habari la AFP mjini Ramallah kwamba mkutano huo ulianza saa saba mchana muda mfupi baada ya Rais Abbas kuwa na mazungumzo na Emir Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani wa Qatar mjini Doha leo hii.

Taarifa iliotolewa na kundi la Hamas imesema Abbas na Meshaal wamekuwa na mkutano wa muda mrefu mchana huu mjini Doha kujadili matukio ya Wapalestina yaliyotokea hivi karibuni kabisa ikiwa ni pamoja na makubaliano ya usuluhishi na kuweka mazingira mazuri ya kuyafanikisha.

Taarifa hiyo imeongeza kusema kwamba mkutano huo ulikuwa mzuri ambapo viongozi wote wawili wameelezea umakini wa utashi wao wa kuanza ukurasa mpya chini ya msingi wa ushirikiano wa kitaifa.

Kiongozi huyo wa Hamas anayeishi uhamishoni amekuwa akikaa Doha kwa zaidi ya miaka miwili baada ya kuondoka katika makao yake ya awali nchini Jordan kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria.

Uhasama wa muda mrefu

Mara ya mwisho viongozi hao walikutana ana kwa ana mjini Cairo Misri hapo mwezi wa Januari mwaka 2013.

Mkuu wa serikali ya Hamas Ismail Haniyeh (kulia) na afisa mwandamizi wa Fatah Azzam Al-Ahmed (kushoto) wakati walipotangaza makubaliano yao ya usuluhishi Gaza City.Picha: Reuters

Kundi la Fatah la Abbas ambalo ndilo lenye kukidhibiti Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO kwa miaka mingi limekuwa katika uhasama mkubwa na kundi la Hamas la Meshaal tokea kundi hilo la itikadi kali za Kiislamu lilipouchukuwa kwa nguvu Ukanda wa Gaza hapo mwaka 2007 na kuvifanya vikosi vya Abbas vibakie Ukingo wa Magharibi tu.

Juhudi za usuluhishi za hapo awali zimeshindwa lakini hapo tarehe 23 Aprili chama cha PLO na Hamas vilitangaza kufikia makubaliano ambayo kwayo watashirikiana kuunda serikali mpya itakayoongozwa na watu watakaokuwa huru kisiasa.

Hamas imesema huenda ikawajumuisha wanajeshi wapatao 3,000 wa vikosi vya usalama vya Mamlaka ya Wapalestina kusaidia shuguli za ulinzi huko Gaza ikiwa kama ni hatua za muda.

Hatua za muda

Katibu wa serikali wa kundi la Hamas Abdul Salam Siyyam amesema katika taarifa hapo jana kwamba kuna kifungu chenye kuzungumzia hali ya usalama ikiwa ni pamoja na mipango ya utawala kwa wanajeshi 3,000 wa taasisi za usalama huko Ramallah kufanya kazi kama sehemu ya shughuli za usalama katika Ukanda wa Gaza. Amesema hatua hiyo itakuwa kwa ajili ya kipindi cha mpito bila ya kusema itakuwa kwa muda gani.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (kulia) na Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas (kushoto).Picha: picture-alliance/dpa

Habari za kufikiwa kwa makubaliano kati ya pande hizo mbili mwezi wa Aprili zilichemsha ghadhabu kutoka Israel ambayo imesema haitozungumza na serikali yoyote ya Wapalestijna inayoungwa mkono na Hamas jambo ambalo limekomelea msumari wa mwisho kwenye jeneza la duru ya mwisho ya mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na Marekani.

Abbas amesema makubaliano ya kuungana na Hamas hayatomzuwiya kufanya mazungumzo zaidi na Israel katika kipindi cha usoni.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP/dpa

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman