Fatah na Hamas yatesa wapinzani wao
15 Novemba 2008Wafungwa hao wanashikiliwa kwenye magereza ya Mamlaka ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi.Imebainika kwamba makundi hayo hasimu makuu ya kisiasa ya Kipalestina yanaendelea kutesa na kukandamiza wapinzani wao.
Kundi la Hamas ambalo linadhibiti Ukanda wa Gaza limedai kuachilwa kwa wafungwa hao kama sharti la kuhudhuria mazungumzo hayo ambayo yalikuwa yamepangwa kufanyika mjini Cairo nchini ya upatanishi wa Misri.Hivi karibuni Hamas iliwaachilia huru wafungwa wa kisiasa 80 wa kundi la Fatah kutoka kwenye magereza ya Gaza na ilidai Mamlaka ya Wapalestina ichukuwe hatua kama hiyo.
Kwa mujibu wa mashirika ya haki za binaadamu mahasimu hao wakuu wa kisiasa wanaendelea kuwafunga , kuwatesa,kuwakandamiza na kuwadhulumu wapinzani wao wa kisiasa wakati mapambano ya kuwania madaraka katika maeneo mawili makuu ya Wapalestina ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi yakiendelea kupamba moto.
Watatezi wa haki za binaadamu wanasema sehemu kubwa ya mahabusu wa Hamas katika Ukingo wa Magharibi hawana uhusiano na tawi la kijeshi la kundi hilo au harakati zake za kukusanya michango na kwamba sehemu kubwa ya kamata kamata inayofanywa na makundi hayo mawili ni ya kisiasa na haihusiani kabisa na usalama wala uhalifu.
Shawan Jabarin wa shirika la haki za binaadamu la Kipalestia Al Haq lenye makao yake mjini Ramallah amesema katika kipindi cha miezi miwili iliopita wameshuhudia kampeni ya kiwango kikubwa huko Ukingo wa Magharibi ya kuwakandamiza watu wanaosemekana kuwa wamo kwenye kundi la Hamas.
Naye Raji Sourani mkuregenzi wa Kituo cha Haki za Binaadamu cha Wapalestina kinachoheshimiwa kimataifa kikiwa na makao makuu yake mjini Gaza anasema hatua ya Hamas ya kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa ni hatua kwenye muelekeo sahihi na ameitaka Mamlaka ya Wapalestina kuiga hatua hiyo.
Hata hivyo anaendelea kuwa na wasi wasi juu ya udhibiti wa Hamas kwa mahkama na bunge kunakozuwiya kuwepo kwa mfumo wa sheria wa haki.
Sourani ameliambia shirika la habari la IPS kwamba kuendelea kwa makundi hayo kufanyiana vitendo vya dhuluma pia kunafanya iwe vigumu zaidi kwa makundi hayo ya Kipalestina kuwa na msimamo wa pamoja wa kisiasa.
Shirika la Al Haq linakadiria asilimia 20-30 ya wafungwa wanaoshikiliwa na makundi hayo wamekabiliwa na mateso ya aina mbali mbali ikiwa ni pamoja na vipigo vibaya na kwamba katika kesi nyingi mahkama imeamuru kuachiliwa kwa mahabusu hao lakini mashirika ya kijasusi yamepuzilia mbali amri hizo.
Waandishi wa habari wanaojihusisha na upande mmoja wa upinzani wamekuwa pia wakiandamwa na wengi wao hivi sasa wanahofu kuelezea upinzani wao.
Mahabusu kadhaa wamekufa wakiwa wanashikiliwa huko Gaza na Ukingo wa Magharibi.
Kamati ya Wapalestina ilioanzishwa na makundi ya haki za binaadamu na wa wabunge kufuatilia kamata kamata ya kisiasa imeshindwa kufanya kazi licha ya kwamba ilikuwa na baraka za Rais Abbas lakini mashirika yake ya ujasusi ambayo anayadhibiti yaligoma kutowa ushirikiano wake.
Tatizo hilo linafanywa kuwa gumu zaidi kutokana na mifumo ya sheria za jinai huko Gaza na Ukingo wa Magahribi kuwa na kasoro kubwa sana pamoja na hatua ya Israel kuharibu vituo vya usalama na vile vya kushikilia wahalifu vya Wapalestina.