Fayulu kuwasilisha pingamizi dhidi ya matokeo ya uchaguzi
12 Januari 2019Wakati huo huo , wakati muungano wake wa upinzani umesisitiza kwamba alipata asilimia 61 ya kura kwa mujibu wa uchunguzi wa waangalizi wa kanisa katoliki lenye ushawishi mkubwa .
Fayulu alizungumza na mamia kwa maelfu ya waungaji wake mkono ambao walikusanyika katika mji mkuu Kinshasa, kupinga kile walichokiita "ushindi wa wananchi ulioibiwa."
Polisi wengi walionekana wakishika doria katika mji huo mkuu. Mfanyabiashara na mwanaharakati anayefanya kampeni dhidi ya rushwa iliyokithiri nchini Congo, Fayulu amemshutumu rais anayeondoka madarakani Joseph Kabila kwa kufanya makubaliano ya chini kwa chini na mshindi aliyetangazwa , kiongozi wa upinzani ambaye hajajihusisha sana na siasa Felix Tshisekedi.
Kanisa katoliki , mamlaka adimu ambayo Wakongo wengi wanaliamini, limesema wachunguzi wake 40,000 wa uchaguzi wamempata mshindi tofauti kutoka matokeo rasmi lakini halikutoa maelezo zaidi.
Uchunguzi wa kanisa hilo umegundua Tshisekedi alipata asilimia 18 ya kura , juu kidogo ya mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary, muungano wa Fayulu umesisitiza.
Matokeo yachapishwe
Fayulu ametoa wito kwamba tume ya uchaguzi ya Congo ichapishe maelezo ya matokeo, kituo kwa kituo, na kusema atawasilisha mashauri mahakamani leo Jumamosi asubuhi (12.01.2019) kupinga matokeo hayo. Aliwatupia busu watu waliokusanyika. "Wale ambao wamekuwa wajinga kuchapisha matokeo bandia, tutapambana nao," alisema.
Wacongo wanakabiliwa na hali isiyokuwa ya kawaida ya uchaguzi unaodaiwa kuwa umechakachuliwa kuelekea upinzani baada ya mgombea aliyependelewa na Kabila , Shadary , kufanya vibaya katika uchaguzi.
Tume ya uchaguzi mapema siku ya Alhamis ilitangaza kwamba Tshisekedi alishinda kwa asilimia 38 ya kura wakati Fayulu alipata asilimia 34.
"Mabadiliko hayawezi kujadiliwa nyuma ya pazia na madaraka yanakuja tu kutokana na sanduku la kura, hakuna njia nyingine," amesema muungaji mkono wa Fayulu Jean Otaba , mwenye umri wa miaka 28. "Unaweza kuona hakuna sherehe kubwa licha ya tangazo hilo. Hii ni kwasababu sio kweli.
wakati huo huo vyama vinavyomuunga mkono rais anayeondoka madarakani nchini Congo Joseph Kabila vimeshinda wingi katika uchaguzi uliocheleweshwa wa bunge, kwa mujibu wa ukusanyaji wa hesabu uliofanywa na shirika la habari la AFP leo.
Vyama vinavyomuunga mkono Kabila vimevuka kiwango cha viti 250 kinachotakiwa kuwa na wingi bungeni katika bunge la taifa lenye viti 500, kwa mujibu wa matokeo yaliyowekwa pamoja na tume huru ya taifa ya uchaguzi CENI.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape