1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FDP yaidhinisha makubaliano ya serikali ya muungano

Sylvia Mwehozi
6 Desemba 2021

Chama cha Ujerumani kinachopigia debe mazingra rafiki ya biashara cha FDP, kimeidhinisha kwa wingi makubaliano ya serikali ya muungano yaliyofikiwa baina yake na chama cha Social Democrats SPD na kile cha kijani. 

FDP Parteitag (Aufmacher)
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Katika mkutano maalumu wa FDP uliofanyika kwa njia ya vidio mjini Berlin, asilimia 92 ya wajumbe wa mkutano huo walipiga kura ya kuunga mkono makubaliano ya uundwaji wa serikali ya muungano. Uamuzi huo unamfanya kaimu makamu Kansela na waziri wa fedha Olaf Scholz, hatua moja mbele ya kuchukua hatamu ya Ukansela kutoka kwa Angela Merkel.

Kiongozi wa FDP Christian Lindner, ambaye anatazamiwa kuchukua wadhifa wa waziri wa fedha katika serikali ijayo, amejaribu kuondoa wasiwasi wa chama hicho kuegemea katika mrengo wa kihafidhina zaidi, akisema makubaliano ya muungano yanasukuma sera za msimamo wa kati. Ameongeza kwamba makubaliano hayo yataisogeza nchi mbele zaidi.

"Hatimaye, sasa tuna mkataba wa muungano. Nina hakika kwamba hautambuliki na mipaka tuliyowekeana. Badala yake, makubaliano haya ya muungano yana sifa ya ukweli kwamba tumepanuka na kupeana sifa. Yanaelezea sera mpya kwa nchi yetu."

Kabla ya kura ya Jumapili, kiongozi huyo alisema kuwa anashawishika nchi itanufaika na serikali ya muungano ijyao. Chama cha Social Democrats SPD, FDP na kile cha kijani vimekuwa katika mazungumzo kwa miezi miwili baada ya SPD kuibuka mshindi katika uchaguzi wa mwezi Septemba.

Olaf Scholz anayetarajiwa kuchukua mikoba ya Kansela wa UjerumaniPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kuidhinishwa kwa makubaliano hayo na wanachama wa FDP kulitarajiwa kwa kiasi kikubwa kwani chama hicho, ambacho kitakuwa kidogo zaidi katika muungano huo, kilijadiliana vyema na kupata wizara kadhaa muhimu.

Siku ya Jumamosi wajumbe wa SPD nao waliidhinisha kwa wingi makubaliano hayo kwa asilimia 98. Chama cha kijani bado kipo katika mchakato wa kupiga kura kwa ajili ya kupitisha makubaliano hayo.

Makubaliano hayo yenye kurasa 177 yanabainisha malengo ya serikali mpya ya Ujerumani katika ngazi ya shirikisho itakayojumuisha vyama vitatu vya SPD, FDP na chama cha kijani. Ikiwa vyama vyote vitatu vitakubaliana na mpango huo, makubaliano yatasainiwa rasmi na kumruhusu Scholz kutafuta kupitishwa rasmi katika bunge la Bundestag siku ya Jumatano.

Serikali mpya ya muungano ya SPD, Kijani na FDP imepachikwa jina la 'Taa za barabarani' kutokana na rangi za vyama hivyo, yaani nyekundu, njano na kijani.

Muungano huo mpya utachukua nafasi ya muungano mkuu wa vyama vya kihafidhina vya Christian Democratic Union (CDU) na SPD - kambi mbili kubwa zaidi za vyama bungeni, ambazo zimetawala siasa za Ujerumani tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW