1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fedha bado ni kizingiti katika vita dhidi ya njaa

18 Novemba 2009

Mkutano wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani,FAO, uliojadili masuala ya kuadimika kwa chakula uliofanyika mjini Roma,Italia umekamilika bila ya kupata fedha mpya kwa minajili ya kupambana na njaa ulimwenguni.

Viongozi waliohudhuria kikao cha Roma,ItaliaPicha: AP

Kikao hicho cha siku tatu kiliwaleta pamoja viongozi wa mataifa 60 kote ulimwenguni.Hata hivyo viongozi wa kundi la mataifa tajiri duniani G8 hawakuhudhuria kikao hicho ila mwenyeji wa mkutano huo Italia pekee.Wakati huohuo takwimu za Umoja wa Mataifa zimeonyesha kuwa kiasi cha watu milioni 23 kote ulimwenguni hawana chakula cha kutosha.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula la Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO lililoandaa kikao hicho,kiasi cha dola bilioni 44 zinahitajika kuwekezwa katika sekta ya kilimo kila mwaka kwa madhumuni ya kupambana na njaa.Kiasi hicho cha fedha ni sawa na asili mia 17 ya msaada wa maendeleo badala ya kiasi kilichopo cha asimilia 5.

Mwaka huu pekee idadi ya watu wanaotatizwa na njaa imefikia bilioni moja kwasababu ya mtikisiko wa kiuchumi unaoukumba ulimwengu mzima.

Waziri Mkuu wa Italia Silvio BerlusconiPicha: AP

Viongozi hao waliohudhuria kikao hicho walishindwa kuafikiana kuhusu kiwango cha fedha kitakachotumika kuhakikisha kuwa tatizo la uhaba wa chakula linashughulikiwa.Ifahamike kuwa wawakilishi wa mundi la mataifa tajiri ulimwenguni G8 hawakuhudhuria mkutano huo wa Roma isipokuwa Italia iliyokuwa mwenyeji wa kikao iliyowakilishwa na Waziri Mkuu Silvio Berlusconi.Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la FAO Jacques Diouff hakufurahishwa na matokeo ya mkutano huo na akatilia mkazo umuhimu wa kuwashiriikisha wadau wakuu,''Mosi tunahitaji kuwashirikisha washirika wote…WTO,WHO,Benki ya Dunia na taasisi za fedha kwasababu wote wana mchango muhimu. Tuliafikiana pia kuwa kamati husika sharti iwakilishwe na wajumbe wa ngazi za juu la sivyo maamuzi hayatoweza kupitishwa.Haya ni baadhi ya masuala tuliyoyajadili'' alisema.

Kwa upande wake Shirika la kutoa misaada la Uingereza Oxfam limeafiki kuwa mkutano mmoja pekee kamwe hauwezi kupata suluhu ya matatizo yote yanayosabishwa na njaa kote ulimwenguni.Msemaji wa shirika hilo Gawain Kripke aliongeza kwamba viongozi wa mataifa tajiri kutouhudhuria mkutano huo kulitoa ishara mbaya tangu mwanzo.

Mkulima wa mpunga akiliandaa shambaPicha: AP

Rais wa Marekani Barack Obama aliye ziarani barani Asia hakuhudhuria kikao hicho.Washiriki wa kikao hicho waliahidi kutoa kiwango cha fedha kilichokuwa sawa na kile kilichotolewa mwaka 1996 ambacho kina azma ya kuipunguza idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa kwa nusu ifikapo 2015.

Tangazo rasmi la mwisho la mkutano huo vilevile lilishindwa kuweka muda maalum wa kulimaliza kabisa tatizo la njaa ulimwenguni.Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Benedict wa 16 aliyeuhutubia mkutano huo siku ya Jumatatu alisema kuwa ulafi na kutokuwa na uhakika na wala siyo ongezeko la idadi ya watu ndiyo mambo yanayosababisha njaa na umasinikini.Alieleza kuwa baadhi ya mataifa yaliyoendelea yanachangia katika ongezeko la bei za vyakula duniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon aliwaonya wajumbe waliohudhuria kikao hicho kuwa njaa inayosababisha vifo vya kiasi cha watoto alfu 17 kila siku huenda ikakithiri iwapo athari za mabadiliko ya hali ya hewa hayatotafutiwa suluhu.

Katika hotuba yake Kiongozi wa Libya Muammar Kaddafi aliulaani ukoloni uliokuwako barani Afrika na akaikosoa teknolojia ya kuhifadhi mbegu pamoja na mbinu za uzalishaji wa chakula ambazo zimetawaliwa na mataifa makubwa.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO,Jacques DiouffPicha: AP

Hata hivyo kulikuwa na taarifa nzuri katika kikao hicho.Rais wa Brasil Lula da Silva alipokea tuzo ya kufanikiwa kupambana na njaa aliyopewa na Shirika la ActionAid.Kulingana na shirika hilo Brasil ilikuwa ya 29 katika orodha ya mataifa yanayoendelea yaliyofanikiwa kupambana na utapia mlo na vifo vya watoto katika kipindi cha miaka 7.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya/RTRE

Mhariri:Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW