Dola bilioni 1 zakusanywa kulikarabati kanisa la Notre Dame
17 Aprili 2019Wataalam wa ujenzi wamepeleka winchi kubwa na mbao katika eneo la tukio. Maafisa wa zima moto nao bado wanachunguza hasara iliyopatikana na kuona kama nguzo haijaathirika kufuatia janga la moto la jumatatu lililopelekea mnara wa kanisa kuporomoka na kuharibu paa la kanisa hilo mashuhuri Notre dame.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amezidisha shinikizo alipotangaza muda wa miaka mitano kukamilisha shughuli za kulikarabati kanisa hilo kuu mashuhuri kabisa ulimwenguni lililojengwa karne ya 12.
Rais Macron anaongoza kikao maalum cha baraza la mawaziri hii leo kuzungumzia msiba wa Notre Dame ambao wataalam wanaamini ni ajali iliyosababishwa na kazi za ukarabati.
Kengele zitahanikiza kutoka makanisa yote makuu ya Ufaransa leo usiku kwa hishma ya kanisa hilo kuu mashuhuri.
Maajabu ni kwamba hakuna aliyeuwawa kutokana na janga hilo la moto baada ya maafisa wa zima moto kuwahamisha haraka haraka waumini waliokuwa wakihudhuria misa.
Watu wasiopungua 30 wameshahojiwa na polisi kuhusiana na kadhia hiyo ambayo mwendesha mashitaka wa Paris anasema ni tete na itahitaji muda mrefu
Euro milioni 880 zimeshakusanywa muda mfupi tu tangu janga la moto liliporipuka
Mjumbe maalum wa rais anaeshughulikia turathi za kitamaduni Stephane Bern amekiambia kituo cha matangazo cha France Info zaidi ya Euro milioni 880 (kiwangoa mbacho ni sawa na Dala milioni 995 zimeshakusanywa kwa siku moja na nusu tu tangu janga la moto liliporipuka.
Wafadhili wanatokea kila pembe ya dunia tangu karibu mpaka mbali, matajiri na maskini,kuanzia waachamungu wa kikatoliki na wasio wakatoliki.
Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa Francis aliyezungumza kwa simu na rais Macrion jana jioni,amewatolea wito walimwengu wawajibike katika kulijenga upya kanisa kuu la notre dame.
Wakati huo huo muda wa miaka mitano uliowekwa na rais Macron kukaamilisha shughuli za kulikarabati kanisa Notre dame na ambao unasadifu wakati mmoja na michezo ya Olympiki ya mwaka 2024 ya mjini Paris unatajwa na wengi kuwa hauwezekani.