1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Felix Tshisekedi atangazwa mshindi wa urais DR Congo

Daniel Gakuba
10 Januari 2019

Felix Tshisekedin ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Desemba 30 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ikiashiria ubadilishanaji madaraka wa amani kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo.

Kongo Kinshasa Felix Tshisekedi nach der Stimmabgabe
Picha: Reuters/K. Katombe

Tume ya taifa ya uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, CENI, imetangaza ushindi wa Tshisekedi  alfajir ya leo Alhamis, na ushindi huo umekuwa wa kushtukiza kwa wengi ambao walishuku kuwa matokeo hayo yangebadilishwa ili mgombea wa muungano wa vyama tawala, Emmanuel Ramazani Shadary awe ndie mshindi. Shadary alikuwa mgombea aliyeteuliwa mahsusi na rais anayeondoka madarakani, Joseph Kabila.

Takwimu zilizotangazwa na CENI zimeeleza kuwa Tshisekedi amepata kura milioni 7, sawa na asilimia 38 ya kura zote zilizopigwa, akifuatiwa na mgombea mwingine wa upinzani, Martin Fayulu aliyeungwa mkono na watu milioni 6.3, naye Shadary wa muungano wa vyama tawala akaja katika nafasi ya 3 akiwa na kura milioni 4.3. Wagombea wengine waliambulia kura kiduchu.

Tshisekedi atoa heshima kwa Kabila

Baada ya kutangazwa mshindi, Felix Tshisekedi amesema anatoa heshima zake kwa Rais Joseph Kabila, ambaye amesema anamchukulia kama mshirika muhimu kisiasa.

Lakini, aliyekuja katika nafasi ya pili, Martin Fayulu, ameyapinga matokeo yaliyotangazwa, akisema hayana uhusiano wowote na ukweli uliokuwa katika masanduku ya kura. Katika mahojiano na Radio ya Kimataifa ya Ufaransa, RFI, mwanasiasa huyo amewataka waangalizi wa uchaguzi kuchapisha alichokiita 'matokeo ya kweli'', akisema kilichotangazwa na CENI ni mapinduzi kupitia uchaguzi. Mapema wiki hii, Fayulu alikuwa amesema kuwa ikiwa tume itatangaza matokeo tofauti na waliyo nayo, yumkini akimaanisha yanayompa yeye ushindi, muungano unaomuunga mkono ungetangaza matokeo yake wenyewe, ambayo alidai yasingekuwa na mjadala wowote.

Martin Fayulu, amekuja katika nafasi ya pili licha ya kuongoza katika utafiti wa maoniPicha: DW/S. Mwanamilongo

Mwandishi wa idhaa hii katika mji mkuu, Kinshasa, Saleh Mwanamilongo amesema shamra shamra zilianza mara moja katika jiji hilo, ambako Tshisekedi anao ufuasi mkubwa. Hali kama hiyo ya furaha pia imeripotiwa mjini Goma, Mashariki mwa nchi, ambako watu wengi pia wanaunga mkono upinzani.

Changamoto lukuki

Uchaguzi wa Desemba 30 ulifanyika ukiwa umecheleweshwa kwa miaka miwili, kufuatia hatua ya Rais Joseph Kabila kung'ang'ania madarakani, baada ya kumaliza mihula yake miwili inayoruhusiwa kikatiba. Ulikumbwa pia na changamoto kadhaa, zikiwemo kuungua moto kwa ghala la vifaa vya uchaguzi mjini Kinshasa, mashambulizi ya wanamgambo, na mripuko wa ugonjwa hatari wa Ebola.

Mgombea aliyeteuliwa na Rais Joseph Kabila, Emmanuel Ramazani Shadary ameambulia nafasi ya tatuPicha: REUTERS

Changamoto hizo zilisababisha kuahirishwa kwa uchaguzi katika maeneo matatu ya nchi, zikiwemo wilaya za Beni na Butembo katika mkoa wa Kivu Kaskazini, ambako mgombea wa upinzani Martin Fayulu alikuwa na ufuasi mkubwa.

Wakati matokeoa yalipokuwa yakisubiriwa, wagombea wawili wakuu wa upinzani waliliambia shirika la habari la DPA kwamba hawakuwa na imani kwamba uchaguzi huu unaweza kuwa huru wala wa haki, kutokana na historia ya Congo iliyojaa makovu ya mizozo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, ape

Mhariri: Rashid Chilumba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW