FIFA: Ujerumani bado ni timu bora
16 Oktoba 2017Timu hizo zitakazowekwa katika chungu kimoja katika upangaji wa timu zitakazoshiriki katika makundi ya fainali za kombe la dunia mwakani , pamoja na michuano ya mchujo ya kombe la mataifa ya bara la Ulaya.
Mabingwa wa dunia Ujerumani , Brazil , Ureno , Argentina, Ubelgiji , Poland na Ufaransa zinajiunga na Urusi kuwa timu zitakazowekwa katika chungu cha kwanza katika upangaji wa timu hapo Desemba mosi kwa ajili ya fainali za mwaka 2018.
Katika upangaji wa makundi kwa ajili ya michuano ya kufuzu kucheza katika fainali za kombe la mataifa ya Ulaya hapo kesho Jumanne, Uswisi, Italia, Croatia na Denmark zitakuwa miongoni mwa timu za juu, wakati Ireland ya kaskazini , Sweden , Ireland na Ugiriki ni timu za chungu cha pili.
Timu bora 6 hazijabadilika
Katika orodha ya FIFA ya timu bora , timu 6 za juu hazijabadilika, wakati Ufaransa imepanda nafasi moja hadi ya saba na Uhispania imepanda nafasi tatu hadi nafasi ya nane lakini hazimo katika chungu namba moja.
Chile, ambayo imeshindwa kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia , imebakia kiuwa katika nafasi ya tisa wakati Peru imeingia katika kumi bora kwa mara ya kwanza, ikipanda nafasi mbili hadi ya kumi. Peru imefanikiwa kuingia katika mchezo wa mchujo wa mabara dhidi ya New Zealand ikiwa katika nafasi ya 122 katika juhudi zao za kufikia fainali za kombe la dunia.
Kwingineko Uingereza imepanda nafasi tatu hadi 12 wakati timu nyingine zilizopiga hatua ni pamoja na Denmark iliyopanda nafasi saba hadi ya 19, Scotland ikiwa katika nafasi ya 29, Austria , 39. Wenyeji wa kombe la dunia Urusi iko katika nafasi ya 65.
Kwa upande wa Afrika Tunisia inaongoza bara hilo nafasi iliyoshika miaka 15 iliyopita kwa kukaribia kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia mwakani. Ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Guinea wa Tai wa Carthage ni mafanikio makubwa kwa kocha Nabil Maaloul. Misri iliyokata tikiti yake katika fainali za kombe la dunia kwa kuishinda Congo Brazzaville mwishoni mwa juma lililopita , imeporomoka nafasi moja na kushika nafasi ya pili wakati Morocco imepanda nafasi tatu na kushika nafasi ya saba. Senegal ni ya tatu, (32)ikifuantiwa na jamhuri ya kidemokrasi ya Congo,(35) , Nigeria ni ya tano (41), Cameroon ni ya 6, (42), Morocco ya 7, (48), Ghana ni ya nane (52), Burkina Faso ni ya 9 , (55) na Cote d'ivoire ni ya 10 (61).
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae / ape
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman