1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA yakumbwa na kashfa nzito

Admin.WagnerD18 Desemba 2014

Kamati ya uongozi wa shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA inakabiliwa na mgogoro mpya kufuatia kujiuzulu kwa Michael Garcia, akipinga kuchakachuliwa kwa ripoti yake ya rushwa katika zabuni za kobe la Dunia.

FIFA-Logo
Picha: picture-alliance/dpa/Steffen Schmidt

Uamuzi wa ghafla wa Garcia kujiuzulu siku ya Jumatano huenda ukazidisha shinikizo ndani ya kamati ya uongozi ya rais wa FIFA Sepp Blatter kuchapisha ripoti ya wakili huyo Mmarakeni yenye kurasa 430, inayotathmini kura zilizozipatia ushindi wa kuandaa kombe la dunia, nchi za Urusi kwa mwaka 2018 na Qatar mwaka 2022.

Akiwa ameshtushwa na kujiuzulu kwa Garcia, Blatter aliliambia shirika la habari la Associated Press kuwa jambo hilo moja ya mada za mkutano wa siku mbili wa bodi ya uongozi wa FIFA, uliyofanyika Alhamisi na Ijuma. Wajumbe 27 wa Bodi hiyo wamegawanyika juu ya ama kutangaza sehemu au ripoti kamili ya Garcia, jambo lililosababisha watatu kati yao kushtakiwa kwa mienendo inayokiuka maadili.

Aliekuwa Emir wa Qatar Sheikh Hamad Khalifa al-Thani na naibu waziri mkuu wa Urusi Igor Shuvalov wakibeba kombe la Dunia nyuma ya rais wa FIFA Sepp Blatter baada ya nchi zao kutangazwa washindi wa zabuni za uandaaji wa mwaka 2018 na 2022.Picha: AFP/Getty Images/F. Coffrini

Uozo ndani ya FIFA

Sifa ya FIFA ilipata pigo jingine baada ya Garcia kusema kuwa hakuna kamati huru ya uongozi, mchunguzi, au kamati ya upatanishi inayoweza kubadilisha utamaduni wa shirikisho hilo. Blatter alieleza kushangazwa na uamuzi huo wa Garcia, lakini alisema kazi ya kamati ya maadili itaendelea na kuwa sehemu muhimu ya mkutano huo wa bodi ya uongozi.

Mchunguzi huyo Garcia alijiuzulu siku moja baada ya FIFA kutupilia mbali rufaa yake dhidi ya mukhtasari wa uchunguzi wake uliyotangazwa na shirikisho hilo, kuhusu utoaji wa zabuni za maandalizi ya kombe la dunia mwaka 2018 na 2022.

Katika taarifa, Garcia alisema kulikuwa na ombwe la uongozi katika FIFA, na kwamba alikuwa amepoteza imani na Hans-Joachim Eckert, mwenyekiti wa chemba ya maamuzi ya idara ya maadili, na kwamba jukumu lake katika mchakato huo lilikuwa limefika mwisho.

Urusi, Qatar zasafishwa na FIFA

Urusi ilishinda zabuni ya kuandaa mashindano ya kombe la dunia mwaka 2018, huku Qatar ikishinda uwenyeji wa mashindano ya mwaka 2022. Lakini kufuatia madai ya rushwa, Garcia alipewa jukumu la kuchunguza na kuripoti juu ya mchakato wa maombi ya zabuni hizo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Garcia aliyoitoa siku ya Jumatano, ripoti yake ilibaini masuala mazito na mapana kuhusiana na mchakato wa maombi. Lakini mukhtasari wa Eckert wa ripoti hiyo uliyochapishwa mwezi Novemba, ulizisafisha Urusi na Qatar kutokana na makosa yoyote.

Garcia aliukatia rufaa mara moja mukhtasari uliyotolewa na Eckert, akisema ripoti yake imewasilishwa isivyo. Lakini rufaa yake ilielezwa kama isiyokubalika na FIFA, kwa hoja kwamba mukhtasari huo uliyotangazwa hauhusishi maamuzi, na kwa hivyo hauna nguvu ya kisheria na wala hauwezi kukatiwa rufaa.

Michael Garcia akiwa na mwenyekiti wa Chemba ya maamuzi ya kamati ya maadili ya FIFA Hans.Joanchim Eckert.Picha: picture-alliance/epa/W. Bieri

Mapambano yanaendelea

Mtendaji kutoka Ujerumani Theo Zwanziger anapanga jaribio lingine kuichapisha kikamilifu ripoti ya Garcia, na pia kwenye ajenda ya mkutano wa Marrakeshi kunajadiliwa sheria za kazi nchini Qatar.

"Fifa katika zahma," liliandika gazeti la Uingereza la The Guardian katika toleo lake la jana Alhamisi, huku Sueddeutsche Zeitung la Ujerumani likiitaja hatua ya Garcia kuwa kilele cha muda cha malumbano yaliokuwa yanatokota kwa muda mrefu."

Rais wa shirikisho la mpira wa miguu barani Ulaya UEFA Michel Platini, ambaye anamtaka Blatter aachie ngazi kama mkuu wa FIFA mwakani, aliitaja hatua ya kujiuzulu kwa Garcia kama upungufu mpya. Afisa mtendaji wa zamani wa FIFA Jerome Champagne, ambaye anapanga kupambana na Blatter katika kinyanganyiro cha urais wa shirikisho hilo aliitaja kama hatua ya kurudi nyuma.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,ape.
Mhariri: Saumu Yusuf

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW