FIFA yatangaza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi
1 Juni 2013Hata hivyo baadhi wanasisitiza kuwa FIFA haifanyi ya kutosha. Rais wa shirikisho hilo Sepp Blatter, hata hivyo ametoshelezwa na hatua hizo kufuatia kashfa zilizoshuhudiwa katika miaka kadhaa ya nyuma. Akizungumza katika kikao cha wajumbe wa FIFA mjini Port Louis, Mauritania, Blatter amesema kuwa ana furaha FIFA hatimaye imejinyanyua baaada ya kukabiliwa na changamoto chungu nzima.
Lakini mkuu wa jopo la mageuzi linalolishauri shirikisho la FIFA amesema bado kuna mengi ya kufanywa. Profesa huyo Mswisi Mark Pieth amesema FIFA ni lazima itangaze hadharani mishahara na marupurupu ya maafisa wake wanaopata donge nono na kuweka kiwango cha juu cha umri na muhula wa kuhudumu kwa maafisa wake wakuu. Pia, wachunguzi huru hawajajumuishwa katika kamati kuu ya FIFA inayofanya maamuzi.
Hatua kali dhidi ya ubaguzi wa rangi
FIFA imechukua hatua kuhusiana na ubaguzi wa rangi, na sasa timu zitakabiliwa na adhabu kali kwa kupatikana na hatia ya tukio baya la kibaguzi, ikiwa ni pamoja na kupokonywa pointi na kushushwa daraja.
Hatua hizo zimeidhinishwa kwa wingi na zinafuatia matatizo ya karibuni nchini Italia na England. Kulingana na sheria hizo mpya, makosa makubwa au ya kurudiwa yatakayofanywa na klabu au mashabiki wake yatasababisha pia kupigwa marufuku timu kushiriki katika vinyang'anyiro fulani ikiwa ni pamoja na ligi ya mabingwa Ulaya – Champions League.
Mwanamke wa kwanza achaguliwa
Katika suala jingine, Lydia Nsekera wa Burundi amepigiwa kura ya kujiunga na kamati kuu ya FIFA kama mwanamke wa kwanza kuwahi kuwa mwanachama wa kudumu kwa muhula wa miaka minne, wakati wanawake wengine wawili wakiwekwa katika kamati hiyo kwa mwaka mmoja. Nsekera alihudumu katika bodi hiyo kwa kipindi cha muda mwaka uliopita.
Kamati kuu imepanuliwa hadi wanachama 27. Rais wa shirikisho la soka Marekani Sunil Gulati ameanza muhula wake katika kamati hiyo hapo jana. Gulati amechukua nafasi ya Chuck Blazer ambaye alihudumu kwenye kamati hiyo tangu mwaka wa 1997 na akasimamishwa uwanachama mapema mwezi Mei baada ya kutuhumiwa kwa madai ya ubadhirifu wa takribani dola milioni 21.
Mwandishi: Bruce Amani/
Mhariri: Sekione Kitojo