FIFA yatikiswa na kashfa ya rushwa
27 Mei 2015Kukamatwa kwa maafisa hao waandamizi wa FIFA ambako kumelitikisa shirikisho hilo la soka ulimwenguni, kumetokana na vibali vilivyotolewa na wizara ya sheria ya Marekani, ambayo inawatuhumu kwa hila za rushwa na hongo katika kipindi cha miaka 24 iliyopita.
Kwa ujumla waliofunguliwa mashitaka ni maafisa tisa wa FIFA na wakurugenzi wakuu watano wa makampuni ya biashara. Wizara ya sheria ya Marekani imesema tayari maafisa wanne wa FIFA na makampuni mawili ya biashara wamekiri tuhuma zinazowakabili.
Msemaji wa FIFA Walter de Gregorio ambaye amezungumza na waandishi wa habari saa chache baada ya kukamatwa maafisa wa shirikisho hilo, amesema FIFA inaunga mkono hatua ya Uswisi na Marekani dhidi ya watuhumiwa, na kuongeza kuwa mkutano wa kamati kuu ya shirikisho hilo unaofanyika mjini Zurich utaendelea kama ilivyopangwa.
Amesema, ''FIFA inaunga mkono kikamilifu uchunguzi huu na itatoa ushirikiano kwa serikali ya shirikisho ya Uswisi na kwa idara ya sheria. Lakini, ingawa tunaunga mkono mchakato huo, FIFA ndio inayoathirika, ndio inayopita katika wakati mgumu. Hata hivyo, mkutano wetu utaendelea kwa sababu hauhusiani na uchunguzi huu.''
Hila za rushwa na hongo za miongo miwili
Mwanasheria Mkuu wa Marekani Loretta Lynch amesema kwa zaidi ya miongo miwili, maafisa waandamizi wa soka wametumia vibaya madaraka yao, na kujikusanyia mamilioni ya dola kupitia hongo. Wakati kamata kamata ilipokuwa ikiendelea katika makao makuu ya FIFA mjini Zurich Uswisi, msako mwingine ulikuwa ukiendelea katika ofisi za shirikisho la soka la Amerika ya Kaskazini na ya Kati-CONCACAF mjini Florida Marekani.
Wanaohusika katika kashfa hiyo ni pamoja na makamu wa rais wa FIFA Jeffrey Webb ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu ya shirikisho hilo, na rais wa Shirikisho la kandanda la Amerika ya Kati na ya Kaskazini, CONCACAF, mjumbe wa kamati kuu ya FIFA Eduardo Li, Julio Rocha ambaye ni afisa anayeshughulikia maendeleo katika FIFA, Costas Takkas ambaye ni msaidizi wa rais wa CONCACAF, na Jack Warner ambaye aliwahi kuwa rais wa FIFA na wa CONCACAF.
Blatter kugombea licha ya shinikizo
Rais wa FIFA Sepp Blatter hakuhusishwa na uchunguzi huu, na kwa hiyo anaendelea na juhudi zake kutaka kuchaguliwa kwa muhula wa tano kuliongoza shirikisho hilo, licha ya shinikizo kutoka pande mbali mbali, kumtaka aache kugombea tena wadhifa huo.
Mpinzani wake katika uchaguzi wa tarehe 29 mwezi huu, mwanamfalme wa Jordan Ali bin Al-Hussein, amesema kashifa hizi katika FIFA, ni ishara tosha kwamba mageuzi yanahitajika haraka katika uongozi wa shirikisho hilo.
Shirikisho la Soka barani UEFA limesema limefadhaishwa na matukio mjini Zurich, na huku likitarajiwa kufanya mkutano usio rasmi mjini Warsaw jioni hii, taarifa zimeibuka kwamba huenda likataka uchaguzi wa keshokutwa uahirishwe.
Maandalizi ya kombe la dunia; la mwaka 2018 nchini Urusi, na la mwaka 2022 nchini Qatar, ambayo yalizusha utata na kughubikwa na shutuma za rushwa, hayakuathiriwa na kukamatwa kwa maafisa wa FIFA na uchunguzi unaoendelea.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae/afpe
Mhariri:Yusuf Saumu