1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Kandanda

FIFA yatoa tiketi zaidi za Kombe la Dunia 2026

29 Mei 2026

Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani, FIFA, limetoa awamu mpya ya tiketi za Kombe la Dunia 2026 huku zaidi ya tiketi milioni tano zikiwa tayari zimeuzwa kabla ya kuanza kwa michuano hiyo.

Marekani, Washington D.C. 2025 | Donald Trump na Gianni Infantino wakitangaza ratiba ya droo ya Kombe la Dunia 2026
Rais wa Marekani Donald J. Trump na Rais wa FIFA Gianni Infantino wakionyesha tiketi ya Kombe la Dunia la FIFA 2026Picha: CNP/ADM/Capital Pictures/picture alliance

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limetoa kundi jipya la tiketi za Kombe la Dunia 2026, ikiwa zimebaki siku 14 pekee kabla ya kuanza kwa michuano hiyo nchini Marekani, Canada na Mexico.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Alhamisi, FIFA ilisema tiketi hizo zinapatikana kwa mfumo wa "atakayewahi kwanza” hadi zitakapokwisha.

FIFA ilikuwa imetangaza mwezi Aprili kuwa tiketi zingekuwa zikitolewa kwa awamu kupitia tovuti yake rasmi hadi siku ya fainali itakayochezwa Julai 19.

Rais wa FIFA, Gianni Infantino, amesema zaidi ya tiketi milioni tano tayari zimeuzwa kati ya takriban tiketi milioni saba zinazotarajiwa kupatikana kwa mashabiki.

Rekodi ya awali ya mauzo ya tiketi za Kombe la Dunia ilikuwa tiketi milioni 3.5, iliyowekwa mwaka 1994 wakati Marekani ilipoandaa mashindano hayo kwa mara ya mwisho.

Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum akitangaza mashindano ya kuonesha ustadi wa kumiliki mpira. Mexico ni mmoja wa wenyeji watatu wa mashindano ya mwaka huuPicha: Carlos Santiago/ZUMA/IMAGO

Kombe la Dunia kubwa zaidi kuwahi kufanyika

Michuano ya mwaka 2026 itakuwa Kombe la Dunia kubwa zaidi katika historia ya mashindano hayo.

Kwa mara ya kwanza, timu 48 zitashiriki badala ya 32, huku jumla ya mechi 104 zikitarajiwa kuchezwa.

Marekani itaandaa idadi kubwa ya mechi hizo, huku Canada na Mexico zikiwa waandaaji wenza.

FIFA inaamini ongezeko hilo la timu na mechi limechangia mahitaji makubwa ya tiketi kutoka kwa mashabiki duniani kote.

Bei za tiketi zazua malalamiko

Licha ya mauzo makubwa, mfumo wa uuzaji wa tiketi umekuwa ukikosolewa vikali na mashabiki pamoja na baadhi ya viongozi wa Marekani.

Majimbo ya New York na New Jersey yametangaza uchunguzi kuhusu namna FIFA ilivyoshughulikia mauzo ya tiketi, huku waendesha mashtaka wakieleza mchakato huo kuwa wa "mkanganyiko, uhaba wa bandia na bei za juu kupita kiasi.”

Picha hii iliyopigwa Septemba 10, 2025 mjini Mexico City, Mexico, inaonyesha ukurasa wa mauzo ya awali ya tiketi za Kombe la Dunia la FIFA 2026 kwenye tovuti rasmi ya FIFAPicha: Li Muzi/Xinhua/picture alliance

Mapema mwezi huu, jimbo la California pia liliwasiliana na FIFA kufuatia madai kuwa baadhi ya mashabiki walinunua tiketi katika makundi maalum ya viti ambayo baadaye yalibadilishwa.

Shirika la mashabiki wa soka barani Ulaya, Football Supporters Europe (FSE), limeelezea mfumo wa bei za tiketi za Kombe la Dunia kuwa wa "unyonyaji” na "usaliti mkubwa kwa mashabiki.”

Hata hivyo, Infantino ametetea bei hizo akisema zinatokana na mahitaji makubwa ya tiketi na zinaendana na mazingira ya soko la Marekani, ambalo litakuwa mwenyeji wa sehemu kubwa ya mashindano hayo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW