1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Filamu ya maisha ya Harry na Meghan yawapa kiwewe waingereza

9 Desemba 2022

Magazeti chungunzima Uingereza yawashambulia Harry na Meghan kwa madai ya kumchafua Malkia Elizabeth wa Pili kwa kusema uwongo na kutumia lugha chafu dhidi ya Malkia huyo katika filamu yao inayotia fora Netflix

UK Harry und Meghan
Picha: Jacob King/AP Photo/picture alliance

Vyombo vya habari ndani ya Uingereza hivi sasa vimejikita katika kuikosoa filamu inayohusu maisha ya mwanamfamle Harry na mkewe Meghan iliyoanza kuoneshwa wiki hii katika mtandao mkubwa wa filamu duniani, Netflix.

Vyombo vya habari vya Uingereza vinawashutumu wanandoa hao kwa kusema uongo na kutumia lugha mbaya dhidi ya Malkia Elizabeth wa Pili kwenye filamu hiyo inayoonesha uhalisia wa maisha yao.

Katika sehemu tatu za mwanzo za filamu hiyo zilizotoka Alhamisi, familia ya kifalme ya Uingereza kwa kiasi kikubwa haikumulikwa badala yake kilichoonekana zaidi ni maisha ya utotoni ya Harry na chuki aliyokuwa nayo kuelekea vyombo vya habari ambavyo anavilaumu kuwa chanzo cha kifo cha mama yake, Diana.

Picha: Alessandro Abbonizio/AFP

Lakini mwanamfalme Harry hakusita kuishutumu familia hiyo kwa ubaguzi wa rangi na wanandoa hao wanajiandaa wiki ijayo kutowa sehemu nyingine ya filamu hiyo ambayo huenda ikayaibua mengi zaidi.

Kadhia hii imehanikiza kwenye kurasa za mbele za magazeti yaliyochapishwa leo Ijumaa yakibeba vichwa vya habari ambavyo kwa kiasi kikubwa vinawakosoa wanandoa hao, Harry na Meghan.

Mfano ni gazeti maarufu la udaku, The Sun, ambalo limeandika habari hiyo kwa kutanguliza kichwa cha habari kinachosema ''Harry the Nasty'', yaani ''Harry Muharibifu''.

Picha: 2022 Prince Harry and Meghan, The Duke and Duchess of Sussex

Gazeti hilo limekwenda mbali zaidi kwenye makala yake na kuandika kwamba wanandoa hao wameichafua sifa iliyoachwa na Malkia na wamemuacha Mfalme Charles wa Tatu ambaye ni baba yake Harry pamoja na nduguye mwanamfalme William katika hali ya majonzi.

Na pia gazeti hilo limeandika kwamba wameichafua sifa ya nchi nzima bila ya sababu, kwa kuuita ya ubaguzi.

Gazeti hilo pamoja na mengine mengi yameandika kutokana na tukio moja tu la filamu hiyo nzima ambako alionekana Meghan akiimba muziki wakati akikumbuka mara ya kwanza aliyokutana na Malkia Elizabeth wa Pili.

Picha: dpa

Gazeti hilo likahoji kutokana na tukio hilo: "je, ni kwa umbali gani Meghan anaweza kuichafua familia hiyo zaidi ya hapo?" Liliongeza kusema kwamba Meghan alitia chumvi kuibeza familia hiyo ya kifalme.

Gazeti la Daily Mail, ambalo linaegemea sana mrengo wa kulia  na ambalo mara nyingi limejikuta limekuwa likilumbana na wanandoa hao, lilitoka na kichwa cha habari kinachosema Kasri laghadhabishwa na matusi dhidi ya urithi wa Malkia.

Gazeti hilo limeandika habari hiyo karibu kwenye kurasa 20. dani ya maelezo yake mmoja wa waandishi wake aligusia suala la madai yaliyotolewa na wanandoa hao kwamba kujiondowa Uingereza Umoja wa Ulaya yaani Brexit kumechochea ubaguzi ndani ya nchi hiyo na kuchangia hatimaye mgawanyiko wa familia hiyo, mwandishi huyo akisema ni tusi kubwa sana na la upotoshaji.

Picha: Paul Grover/Daily Telegraph/empics/picture alliance

Kisa hiki cha Harry na Meghan hakikuishia tu magazetini, bali jana Alhamisi mbunge wa chama cha Conservative Bob Seely alisema anapanga kupeleka hoja ya kisheria ya kuwavua wanandoa hao vyeo vyao vya kifalme.

Gazeti la mrengo wa kushoto la The Guardian, hata hivyo, limeonesha kuegemea upande wa wanandoa hao likiwaunga mkono na kujikita zaidi kuhusu ukosoaji uliotolewa na Harry  kwamba familia hiyo ya kifalme haikumlinda Meghan dhidi ya ubaguzi wa rangi ulionekana kumuandama kwenye ripoti za vyombo vya habari.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW