1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fillipo Grandi asema Afghanistan haijasahaulika

16 Machi 2022

Mkuu wa shirika la wakimbizi la UN Filippo Grandi asema kuna umasikini na matatizo mengi Afghanistan lakini haijasahaulika

Schweiz | PK Filippo Grandi und Martin Griffiths
Picha: Martial Trezzini/KEYSTONE/picture alliance

Mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa kuhusu wakimbizi Fillipo Grandi amewaambia waafghanistan kwamba hawajasahaulika licha ya ulimwengu kushuhudia vita vinavyoendelea nchini Ukraine vinavyosababisha mgogoro wa kibinadamu barani Ulaya.

Fillipo Grandi ametowa ujumbe ambao waafghanistan wengi ndio waliotaka kuusikia hivi sasa.Mkuu huyo wa shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi amesema licha ya vita vya Urusi nchini Ukraine kushuhudiwa na kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu barani Ulaya ambao haujawahi kuonekana tangu kumalizika vita vya pili vya dunia,bado waafghanistan hawajasahaulika.

 Ni ujumbe ambao waafghanistan waliuhitaji sana katika wakati ambapo wanataka uthabiti wa nchi yao ambayo imezidi kutumbukia kwenye umasikini baada ya kundi la Taliban kutwaa madaraka mnamo mwezi Agosti. Kamishna mkuu huyo wa Umoja wa mataifa kuhusu wakimbizi amesema hatua zimepigwa.

Picha: Wakil Kohsar/AFP/Getty Images

"Nafikiri naweza kusema kwamba hatua zimepigwa lakini ikiwa hatua hizo zimeanza kuonekana matokeo yake ndani ya nchi,nafikiri ni mapema mno kusema, Kuna mgogoro mkubwa hapa wa kibinadamu,mateso ni mengi,njaa na matatizo makubwa ambayo yatahitaji muda mwingi kabla ya sera nzuri kuanza kufanya kazi.''

 Katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la Associated Press Grandi amesema baadhi ya watu wanashangaa kipindi ilichofanyanyika ziara hiyo,lakini akasema hata wakati ambapo macho ya ulimwengu yameleekezwa kwengine,mgogoro wa Afghanistan ni mkubwa sana.

Picha: Airman Edgar Grimaldo/U.S. Air/Planet Pix via ZUMA Press Wire/picture alliance

Ni mwaka jana tu ambapo ulimwengu ulikuwa ukiitazama nchi hiyo namna vijana wa kiume wa Kiafghani wakiparamia ndege ya Marekani iliyokuwa ikiondoka,kupata fursa ya kuikimbia nchi yao baadhi wakianguka na kufariki. Hivi sasa Jumuiya ya Kimataifa iliyopatwa na mshangao inatazama namna ambavyo wimbi la wakimbizi linamiminika kutoka nchini Ukraine,ambalo linatajwa kufikia watu milioni 3 hadi jana Jumanne. Grandi anasema

"Nataraji kwamba Jumuiya ya Kimataifa itaziona hatua zilizopigwa sasa na nia njema iliyopo kwasababu wanatakiwa pia kuchukua hatua  kuelekea kundi la Taliban,bila hivyo- hii nia njema haitokuwa na tija.''

Jana mjini Kabul Grandi alikutana na viongozi wa Taliban na alipangiwa kusafiri katika mikoa ya Kandahar ulioko Kusini na Nangarhar ulioko mashariki mwa nchi hiyo kabla ya kuondoka kesho alhamisi. Alikiri kwamba ameona hatua zimepigwa tangu ziara yake ya mwisho iliyofanyika mwezi Septemba.

Amesema Viongozi wa Taliban wanaanzisha mifumo na kujenga mikakati kuhusu namna ya kuyakabili masuala muhimu wakati kundi hilo likibadili mwelekeo wake wa vita iliokuwa nao na kujielekeza katika uongozi na kuendesha masuala ya kila siku ya kiserikali.Jana ripoti iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika kuratibu msaada wa kiutu ilionesha kwamba asilimia 98 ya Waafghanistan milioni 38 hawana chakula cha kutosha.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW