Fillon ashinda uchaguzi wa mchujo Ufaransa
28 Novemba 2016Katika wakati ambapo wafuasi wa mrengo wa kushoto walioko madarakani wanazidi kuzozana,waziri mkuu wa zamani wa Nicolas Sarkozy (2007-2012) anaweza kupambana na mgombea wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia,Front National-FN,Marine Le Pen duru ya pili ya uchaguzi wa rais itakapoitishwa May 7 mwakani. Na hata kama Donald Trump amezusha maajabu kwa kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa rais wa Marekani,taasisi za utafiti wa maoni ya wananchi zinaondowa uwezekano kwa Marine Le Pen kuweza kuingia katika kasri la Elysée.
Mwongozo wake unaotajwa kuwa"mkali" unaonyesha kuwavutia walio wengi."Tunahitaji mageuzi ya kina" alisema Francois Fillon jana usiku akizungukwa na vigogo wote wa kihafidhina. Gazeti la mrengo wa kushoto Liberation,katika toleo lake la leo,linautaja ushindi wa Fillon kuwa ni wenye kuelemea mno upande wa kulia. Kwa mujibu wa mtaalam wa masuala ya kisiasa Jean Yves Camus,mwongozo wa Francolis Fillon utabidi ufanyiwe marekebisho kidogo ikiwa atataka kweli kuwaleta pamoja wafaransa wote na kuepusha mfarakano hasa katika sekta ya mageuzi ya kijamii na kiuchumi.
Wafuasi wa siasa za wastani wanataka wapaatiwe ufafanuzi kuhusiana na sera za kijamii pia.
Francois Fillon atamshinda Marine Le Pen uchaguzi wa rais utakapoitishwa mwakani
Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Front ational kinautaja mwongozo wa Francois Fillon kuwa ni wa enzi za kale.
Kwa mujibu wa utafiti wa hivi punde,Francois Fillon atampita Marine Le Pen duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais itakapoitishwa April 23 mwakani kwa kujikingia asili mia 26 dhidi ya 24,na kumuacha nyuma kabisa rais Francois Hollande au waziri mkuu wake Manuel Valls,wote wawili wa kutoka chama cha kisoshialisti,ambao wanasemekana watapata asili mia 9 ya kura.
Sera za Francois Fillon kuelekea Urusi na Umoja wa Ulaya zinatia wasi wasi
Mrengo wa kushoto wanamtupia jicho Francois Hollande ambae hadhi na umaaarufu wake unazidi kuporomoka na kukosolewa mpaka na wafuasi wake mwenyewe. Anatarajiwa kutangaza kati kati ya mwezi unaokuja wa decemba kama atagombea mhula wa pili wa miaka mitano,lakini waziri wake mkuu Manuel Valls haondowi uwezekano wa kushindana nae,uchaguzi wa mchujo utakapoitishwa.
Uwezekano wa ushindi wa Francois Fillon katika uchaguzi wa rais wa Ufaransa mwezi May mwakani unazusha baadhi ya hofu nchini Ujerumani na hasa msimamo wake kuelekea Urusi. Na katika masuala ya Ulaya pia,msimamo wa Fillon kuhusu kuundwa serikali ya nchi za kanda ya Euro hauwavutii viongozi wa mjini Berlin.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/
Mhariri:Yusuf Saumu