1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FINAL YA KLABU BINGWA AFRIKA

24 Oktoba 2005

Bundesliga-Munich yarejea kileleni;Ligi mashuhuri za Afrika na Nairobi marathon.

Nahodha wa timu ya Taifa ya Ujerumani iliotawazwa mabingwa wa dunia 1990, mjini Roma, Lothar Matthaus, ameteuliwa na FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni, kuzichagua timu zitakavyopambana katika makundi tofauti kwa kinyan’ganyiro cha Kombe lijalo la dunia.Kura yenyewe itapigwa desemba 9 mjini Leipzig.Ujerumani itaandaa kombe la dunia mwakani kuanzia Juni 9 na finali Julai 9.Matthaus, mwenye umri wa miaka 44 ni kocha wa timu ya taifa ya Hungary ,lakini kwavile Hungary haitashiriki katika Kombe hilo la dunia, Lothar Matthaus,atakuwa nyuma ya timu ya Ujerumani.

Katika Bundesliga-ligi ya Ujerumani, wiki baada ya kupoteza uongozi,mabingwa Bayern Munich wamerudi kileleni.Munich jumamosi iliikomea Duisburg mabao 4:0.Ilikua duru ya kuipendeza Munich,kwani mahasimu wao wakubwa Werder Bremen waliteleza pointi kwa kutoka sare 0-0 na Hannover na Hamburg ilitoka pia suluhu na Borussia Mönchengladbach bao 1:1 hapo jana.

Mkiani mwa Ligi,Eintracht Frankfurt iliichezea FC Cologne, kindumbwendumbwe na kuizaba mabao 6-3.Hii imechochea mtafaruku mjini Co,logne huku maswali yakiulizwa ilikuaje ?

Hatima ya kocha Uwe Rapolder, inategemea wakati tu lini atatimuliwa.orodha ya Bundesliga inaoongozwa tena na Bayern Munich,ikifuatwa na Wrder Bremen ilio pointi 2 nyuma. Hamburg iko pointi 4 nyuma.Mkiani mwa Ligi, ziko timu 3-Nuremberg,Duisburg na Mainz.Cologne inaelekea kujiunga na timu hizo,kwani mahasimu wao mwishoni mwa wiki ijayo, si wengine bali mabingwa Bayern Munich.Na Munich haitataka kupoteza pointi Cologne.

Tarehe zimetangazwa za finali ya Kombe la Afrika la klabu bingwa:Duru ya kwanza ya finali hiyo kati ya Etoile Sahel ya Tunesia na Al Ahly ya Misri, itachezwa Oktoba 29 mjini Sousse,Tunesia.

Na duru ya pili na ya kuamua wapi Kombe hilo litaelekea itakua mjini Cairo,Novemba 12.Rifu katika duru hiyo ya mwisho, atakua mburundi Pare Lassina.Mshindi ataliwakilisha bara la Africa katika kombe la dunia la klabu bningwa nchini Japan hapo Desemba.

Katika Ligi ya Angola, bao la mlinzi wa timu ya taifa Lebo Lebo lilitosha kuipa ushindi wa GiraBola klabu ya Sagrada Esperanca.Mabingwa waliopita AS Aviaco ilichupa nafasi ya pili ya mngazi ya Ligi kwa ushindi wa mabao 2:1 dhidi ya Benefica Luanda.

Katika Ligi ya Ghana,kinyan’ganyiro kileleni kati ya Asante Kotoko na Hearts of oak kilendelea jana.Ushindi lakini, ulikwenda kwa Kotoko ikicheza nyumbani ikiizaba Feynoord Academy bao 1:0.Hearts of Oak ilishinda kwa mabao 3:0 dhidi ya Hearts of Lions.

Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya El Kanemi Warriors jana umeiweka Enyimba kwenye mkondo wa kutwaa ubingwa wa Nigeria.Mabingwa hao wa bara la Afrika, sasa wanaoongoza Ligi kwa pointi 6.

Ama nchini Afrika Kusini,viongozi wa Ligi, Orlando Pirates, wamepoteza rekodi yao ya kutoshindwa hadi sasa.Orlando imelazwa mwishoni mwa wiki kwa mabao 2:1 mjini Durban na Lamontville Golden Arrows.

Na huko Misri, ambako kombe lijalo la Afrika la mataifa litaaniwa Januari,mwakani, Al Ahli iliendelea kutamba ikishinda mpambano wake wa 6 mfululizo .Al Ahly hivyo, imeendeleza hadi mapambano 47 rekodi yake ya kutoshindwa kwa jumla.Al Ahly, iliishinda Gaish mabao 3-0.

Na nchini Zimbabwe viongozi wa Ligi-CAPS United walizimwa sare 0:0 na Highlanders mjini Harare hapo jana.Hivyo wameendelea kushindwa kuwika dhidi ya klabu hiyo kutoka Bulawayo.

Mkenya Samson Barmao alinyakua ushindi wake wa kwanza wa mbio za marathon katika mashindano ya 3 ya marathon ya kimataifa ya Nairobi hapo jana.

Kijana huyo mwenywe umri wa miaka 23 alimpita Kimondiu,mshindi wa kusangaza wa Chicago marathon 2001 katika kim 2 za mwisho kabla hakutia kasi kunyakua ushindi.

Upande wa wasichana, Caroline Cheptanui ndie alieibuka mshindi na hivyo, alimaliza orodha ndefu ya kushindwa katika mbio hizi.Bingwa mtetezi wa nairobi marathon wanawake, Chemokil Chilaong hakuonekana na mwishoe alimaliza wa 11 nyuma ya mchina Liu Xiao Juan.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW