Finali ya Bundesliga
21 Mei 2009Kesho jumamosi, asie na mwana aeleke jiwe na asie na mguu atie gongo-mkutano uwanjani :Historia itaandikwa kesho katika dimba la Ujerumani na ni siku kweli ya historia,Ujerumani ikiadhimisha mwaka wa 60 tangu kuundwa kwake:
Timu 4 zina nafasi ya kutawazwa mabingwa kesho:VFL Wolfsburg yenye pointi 66 ndio wenye nafasi wazi zaidi ya kutwaa taji la bundesliga na itahitaji kutoka sare tu nyumbani katika mpambano wake na Weder Bremen iliohoi baada ya kupokonywa juzi Kombe la ulaya la UEFA na Shakhtar Donetsk ya Ukraine.
Wolfsburg kutoka kaskazini mwa Ujerumani wako pointi 2 na mabao 7 mbele kuliko mabingwa wa Ujerumanikutoka kusini mwa Ujerumani-Bayern Munich.Wakitoka suluhu tu na Bremen itatosha kuvalishwa taji.Mabingwa Munich wanakabiliwa na kinyanganyiro cha mshindi azowa kila kitu katika mpambano wao na Stuttgart nyumbani.
Stuttgart wana pia pointi 64 kama Munich na ushindi kwao utawapiga kumbo Bayern Munich na kuwaweka wao nafasi ya pili nyuma ya Wolfsburg pamoja na kuwahakikishia tiketi ya kucheza msimu ujao katika champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya.
Na hii ni kinyume na timu itakayoangukia nafasi ya 3 hapo itakayobidi kwanza kukata upya tiketi yake . Hata timu iliopo nafasi ya 4 katika ngazi ya Ligi-Hertha Berlin ,bado ina nafasi alao karatasini klutawazwa pia mabingwa:Berlin ina pointi 63 na inahitaji ushindi huko Karlsruhe,timu inayoburura mkia wa Ligi na itia mabao 24.
Hata ikiwa hakuna anaeamini kwamba ,Berlin itatawazwa mabingwa msimu huu, ushindi kesho dhidi ya karlsruhe,utawakatia tiketi ya champions League ama kwa kuangukia nafasi ya pili endapo Munich na Stuttgart wakitoka sare au kama timu ya nafasi ya 3 iwapo Munich au stuttgart ikishinda.
Kocha wa Wolfsburg,Felix Magath , ambae hapo kabla alikuwa kocha wa Werder Bremen na Bayern Munich, amesema kila kitu kinawezekana katika mpambano kati ya timu yake na Bremen.Magath atawategemea tena majogoo wake 2 kuwika usoni:mbrazil Grafite na Mbosnia Edin Dzeko ambao kwa pamoja msimu huu, wameshatia mabao 51.Wanaisaka rekodi iliowekwa na Gerd Mueller na meneja wa sasa wa B.Munich Uli Hoeness ya mabao 53.
1986, Bremen iliingia finali ya Bundesliga ikiwa na pointi 2 zaidi kuliko Bayern Munich kama Wolfsburg kesho.Lakini, ikashindwa mechi yao ya mwisho na Stuttgart wakati Munich ilishinda mpambano wake na ikatwaa taji kwa tofauti ya magoli.
Mwaka 2000 ,Bayer Leverkusen walijikuta katika hali sawa na hiyo wanaongoza:Lakini walipoteza mechi yao ya mwisho wakati Bayern Munich iliilaza Bremen na kuvaa taji kwa tofauti ya magoli.Stuttgart iliwahi nayo kunufaika na hali kama hiyo 1994.Walicheza mechi ya mwisho ya msimu wakiwa pointi 2 nyuma ya Frankfurt lakini, ilipolia firimbi ya mwisho,ilłikua Stuttgart ilitoroka na taji.
Sijui maajabu gani yatazuka kesho:ni Wolfsburg,Munich,Stuttgart au Hertha Berlin itaibuka mabingwa wa Bundesliga ?
Tusiandike mate na wino upo.
Muandishi:Ramadhan Ali /DPAE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman