Finali ya Klabu bingwa Afrika
11 Novemba 2005Timu 6 zinazoweza kutawazwa mabingwa wa dunia Juni mwakani nchini Ujerumani,Ufaransa na Ujerumani,Argentina na Uingereza ,Holland na Itali zinaingia uwanjani juammosi hii kupimana nguvu:
Ujerumani ni wenyeji na wanaamini kama 1974 walipoandaa Kombe la dunia ,watalibakisha Kombe nyumbani.Ujerumani lakini imekuwa ikipepesuka hivi karibuni ikilazwa na Uturuki na kushindwa hata kutamba na China.Ufaransa ni mabingwa wa 1998 na Kombe likicheza mpakani mwao, wanahisi hawako mbali nalo.Kocha wa Ufaransa Raymond Domenech anakiongoza kikosi cha Ufaransa katika Stade de France,nje ya Paris baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Costa Rica ,atataka kumuonesha Jürgen klinsmann kwamba timu yake yaweza kuwika hata nchini Ujerumani Juni mwakani.Klinsmann akimrudisha uwanjani nahodha wake Michael ballack,ameshawaonya wachezaji wake kwamba, hataki chochote kasoro ya ushindi.Ufaransa kwa dimba la jioni hii, imemrudisha Necolas Anelka baada ya kupita miaka 3 na nusu.Wengine wanaoweza kuwa hatari katila lango la Ujerumani ni Djibril Cisse,Thierry Henry na David Trezegue. Kuna wasi wasi hatahivyo, kwamba wimbi la machafuko katika vitongoji vya miji ya Ufaransa, huenda likafunika kivuli chake baada ya firimbi ya mwisho ya mpambano huu huko St.Denis, nje ya Paris.
Mpambano mwengine wa kukodolewa macho jumamosi hii ni ule mjini Amsterdam,kati ya wenyeji Holland na Itali-mabingwa mara tatu wa dunia.H olland ndio iliocheza finali ya Kombe la dunia na Ujerumani,1974 na inaamini itacheza tena ikitegemea mizinga yake usoni kama Roy Makaay.
Itali chini ya kocha Marcello Lipi inakusudia kutamba mbele ya timu ya kocha Marco van basten ili jumatano ijayo iwaooneshe Tembo wa Ivory Coast katika miadi yao ya kirafiki,kilichomtoa kanga manyoya.Kwani,Itali itacheza na Corte d’Ivoire,mjini Geneva,Uswisi.Tembo wanajiandaa kwa Kombe la Afrika la mataifa litakaloanza Januari 20 mjini Cairo,Misri,mapema mwakani.
Changamoto nyengine ya kupania kwa kombe la dunia ni kati ya mabingwa wa zamani wa dunia kutoka Amerika Kusini-Argentina wa 1966 uwanjani Wembley-Uingereza.Timu hizi mbili zikikutana zamani,daima ukichomoza uhasama wao katika vita vya Folkland.Uwanjani hivi sasa ni nani tu bora katika medani ya dimba.Kocha Eriksson ana shida ya kuchagua ni beki gani mshahara aliebora-kwa changamoto ya jioni hii baina ya Rio Ferdinard,sol Campbell na John Terry.Kuna wanaodai Terry ana nafasi bora.Kocha wa Argentina Jose Pekermann huenda akamteresha uwanjani chipukizi mpya -Miartin Demichelis anaeichezea Bayern munich,mabingwa wa Ujerumani.
Kati ya mapambano yote ya jioni hii, ni mmoja tu unaoania tiketi ya mwisho ya 31 kwa kombe lijalo la dunia:Australia na mabingwa wa kwanza kabisa wa dunia-Uruguay.Baada ya mabishano marefu kati ya timu hizi mbili, sasa zinaamua ubishi wao uwanjani katika duru ya kwanza kati ya 2 za kuaamua ni nani kati yao atakuja mwakani Ujerumani.Uruguay katika mpambano uliopita ililaza Argentina na kuweka miadi na Australia katika changamoto ya timu za maeneo tofauti kuania tiketi ya Kombe la dunia.Australia inaamini ikiongozwa na kocha wa Holland, Guus Hiddink alieiongoza Korea ya Kusini hadi nusu-finali ya kombe lililopita la dunia, itawika leo mjini Montevideo.Wauru wana fikra nyengine kabisa.
FINALI YA KOMBE LA KLABU BINGWA BARANI AFRIKA:
Asie na mwana eleke jiwe ,kwani jioni hii Al Ahly ya Misri imepania kuichezesha etoile Sahel ya Tunesia, kindumbwe-ndumbwe mjini cairo na kutoroka na Kombe la klabu bingwa barani Afrika.
Rauni ya kwanza ya finali hii ambayo mshindi ataiwakilisha afrika katika Kombe la dunia la klabu bingwa mjini Tokyo,Jpana desemba mwaka huu, ilimalizika suluhu 0:0 mjini Souse,Tunesia.Ni matokeo muafaka kwa Al Ahly ili kuimaliza leo Etoile mjini Cairo.ufunguo wa Al Ahly usoni anao Mohammed Barakat,mchezaji wao wa kiungo na ndie wanaemtazamia mashabiki wa Al Ahly kuufumania na mapema mlango wa watunesia.Ilikua barakat alietia mabao 3 katika nusu-finali na klabu ya pili ya Misri-Zamalek ili kukutana na Etoile katika finali hii.
Kwa Al Ahly, Kombe litakua tu linarudi nyumbani, kwani wamekwishalitwaa mara tatu:1982,1987 na 2001 na waliibuka makamo-bingwa 1983.
Upande wa Etoile, kuna mastadi wachache wa kinigeria ambao waweza kuvunuja matumaini ya Al Ahly kuwika nyumbani na kuondoka na Kombe hili uwanjani.Wao ni Austin Ejide na Emeka Oapara.Isitoshe, Etoile nusra itoroke na Kombe mwaka jana ilipopigwa kumbo na Enyimba na kuipokonywa Kombe katika changamoto ya mikwaju ya adhabu-penalty.Lakini, tusisahau kwamba, Al Ahly ni timu iliosahau kushindwa na mwishoni mwa wiki iliopita tu iliicharaza Al Ittihadi mabao 6:0 na kufanya urodha ya ushindib wake 51 katika muda wa zaidi ya mwaka.Etoile wataweza kuvunja leo rekodi hiyo ?
Tumalizie kwa ringi ya mabondia:
Mbabe mpya wa wezani wa juu ulimwenguni wa shirika la WBC anaetazamiwa kutawazwa kitini ni Hasim Rahman.Bila kuvurumisha konde,Hasim anajaza pengo lililoachwa na mbabe Vitali Klitchko –muukrain aliepiga kambi yake Ujerumani.Klitchko alitangaza kati ya wiki kulivua taji lake na kustaafu kutoka ringini.Klitcho alilazimka kuvunja changamaoto yake ya kupambana leo na rahman kutokana na kuumia goti wakati wa mazowezi huko Los Angeles.
Klitchko mwenye umri wa miaka 34, alivunja pia mpambano wa awali na Hasim Rahman mapema mwaka huu wakati ule akinun’gunika akiumwa na mgongo na maumivu pajani.Hasim Rahman kutoka Baltimore alikwishavaa taji hili la ubingwa wa dunia la WBC kwa kumdengua mbabe Lennox Lewis katika rauni ya 5 mjini Johannesberg, Afrika Kusini,Januari, 2001.
Alilipoteza taji lake hilo katika mpambano wa marudio mwaka huo huo mjini Las Vegas.