1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FINALI YA KOMBE LA CAF KESHO KATI YA ASANTE KOTOKO NA HEARTS OF OAK.NIGERIA NA MVUTANO WAKE NA FIFA NA MICHEAL SCHUMACHE ACHANGIA DALA MILIONI 10 KWA MAAFA YA ASIA.

Ramadhan Ali6 Januari 2005

FINALI YA KOMBE LA CAF KESHO KATI YA KLABU 2 ZA GHANA (KOTOKO NA HEARTS OF OAK) HUKO KUMASI

MVUTANO KATI YA FIFA NA SERIKALI YA NIGERIA

RAIS WA FIFA BLATTER KUZURU AFRIKA KUSINI WIKI IJAYO

NA KWANINI BINGWA WA MBIO ZA MAGARI MICHAEL SCHUHMACHER AMECHANGIA DALA MILIONI 10 KWA MAAFA YA MAFURIKO HUKO ASIA ?

MTANZANIA –KUIBUKA BINGWA WA DANSA YA BARAFUNI UJERUMANI ?

Kesho jumapili ni finali ya Kombe la shirikisho la dimba la Afrika (CAF) baina ya klabu mbili za nchi moja:Ghana.Asante Kotoko inaumana mjini Kumasi na mahasimu wao wakubwa Hearts of Oak.

Duru ya kwanza ya finali hii ilichezwa mjini Accra mwishoni mwa wiki iliopita na kumalizika suluhu bao 1:1.

Kesho ikiwa ‘mcheza kwao hutunzwa’ basi Asante kotoko likiwa ni jogoo la nyumbani,halitaliachia lile la shamba Hearts of Oak kuwika mjini.

Hii ni finali ya kwanza kabisa chini ya mfumo mpya .

Rais wa FIFA-shirikisho la dimba duniani-FIFA-Sepp Blatter akipanga wiki ijayo kuzuru Afrika Kusini-mwenyeji wa Kombe la kwanza la dunia barani Afrika, mvutano ulipambamoto kati ya wiki hii kati ya FIFA na Nigeria :

Kwanza, FIFA iliipa Nigeria hadi jana ijumaa muda kufuta hatua zake za kuwatimua viongozi kadhaa wa Shirikisho la dimba la Nigeria (NFA) alizochukua waziri wa michezo Musa mohammed au si hivyo,Nigeria ifungiwe kucheza dimba kimataifa.

Wiki mbili nyuma, waziri wa michezo Mohammed aliwatimua Katibu mkuu wa NFA Taiwo Ogunjobi na akamteua nahodha wa zamani wa timu ya Taifa Segun Odegbami kujaza nafasi yake.Pia waziri huyo alimteua Salisu Abubakar kuwa mwenyekiti wa halmashauri mpya inayoongoza Ligi ya Nigeria.

FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni,likajibisha kwa kusema uteuzi huo si sawa na haulingani na kifungu cha 17 cha kanuni za FIFA-iliandika FIFA katika barua yake iliochapishwa kwa vyombo vya habari mjini Lagos, juzi jumatano.FIFA ikaipa Nigeria muda hadi Januari 7-yaani jana kurekebisha mambo au la ifungiwe.Miongoni mwa hatua hizo ni kufungiwa Nigeria kucheza mechi zote za kimataifa.FIFA imesema uamuzi uliokatwa na serikali ya Nigeria ni sawa na kujiingiza serikali katika maswali ya dimba na ni kinyume na mazungumzo yaliofanywa mjini Zurich makao makuu ya FIFA.

Juzi jumatano, serikali ya Nigeria, iliidhinisha kufutwa kwa sheria in ayoingilia uhuru wa chama cha mpira cha Nigeria (NFA).Ni sheria ile ile ambayo FIFA ikiibisha.waziri wa michezo Musa Mohammed mwishoni mwa kikao cha baraza la mawaziri huko Abuja imefuta sheria hiyo.Chini ya sheria ya zamani iliofutwa ilikua serikali yenye haki ya kumteua Katibu mkuu wa chama cha mpira cha Nigeria.FIFA kwahivyo, imeitikiwa dai lake lililotaka sheria hiyo ifanyiwe mageuzi na sasa yaonesha mlango ni wazi kwa Nigeria kuania tiketi zake 2 za kuja mwaka ujao Ujerumani kwa Kombe la dunia na kwenda Cairo,Januari mwakani kwa Kombe la Afrika la Mataifa.

KOMBE LA AFRIKA LA MATAIFA LITACHEZWA JANUARI 20,2005 MISRI:

Finali za kombe lijalo la Afrika la mataifa zitaanza Januari 10 na finali itakua Februari 20 mjini Cairo,Misri.Hii ilitangazwa wiki hii na CAF-shirikisho la dimba la Afrika.tangu dimba la ufunguzi hata finali zitachezwa katika Uwanja mkuu wa Taifa mjini Cairo unaochukua mashabiki 80.000.Viwanja vyengine vitakavyochezewa Kombe hilo ambalo mwaka jana lilichezwa Tunisia, havikutangazwa bado,lakini inatarajiwa vitakua mjini Alexandria,port Said na Aswan.

Tarehe za kombe hilo la Afrika,litakalofungua pazia kwa kombe la dunia Juni mwakani hapa Ujerumani, zinaweza kuzusha mfarakano na klabu za Ulaya zitakazobidi kuwaachia wachezaji wao stadi kushiriki katika Kombe hilo na timu zao za Taifa.

Rais wa CAF,mkameroun,Issa Hayatou amekataa kabisa vilio vya hapo kabla kutoka klabu za Ulaya na mameneja wao kuahirisha Kombe la afrika hadi kwanza msimu wa dimba barani Ulaya umemalizika.

Kura ya jinsi timu hizo zitakavyopambana hapo januari,itapigwa hapo Oktoba 20 mjini Cairo, makao makuu ya CAF na hii itakua wiki 2 baada ya kinyan’ganyiro cha kuania tikiti za finali kumalizika.Kinyan’ganyiro hicho kilichosita wakati huu,kitaanza upya hapo machi.

Kwa mara ya kwanza kinyan’ganyiro cha kuania tikiti za kombe lijalo la Afrika kimeambatishwa pamoja na tikiti 5 za afrika kwa Kombe la dunia hapa ujerumani.Mshindi kutoka kila kundi kati ya hayo 5,ataiwakilisha Afrika katika Kombe la dunia Ujerumani.Timu 3 za usoni kutoka kila kundi lakini,zitaenda Cairo kwa Kombe la Afrika.

Misri inaingia moja kwa moja katika Kombe hili kama mwenyeji.

FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni,limejitolea nalo kuchangia dala milioni 3 katika mfuko wa kuwasaidia wahanga wa maafa ya zilzala na mafuriko huko Asia.Inapanga kutumia fedha hizo kujenga upya zana za dimba zilizoathiriwa na msiba wa Tsunami.

FIFA na shirikisho la dimba la Asia –AFC- limetoa mwito kwa wachezaji wa mpira wa zamani kusaidia nao katika juhudi za kueneza misaada .

Nae bingwa mara 7 wa mbio za magari duniani,mjerumani michael Schumacher,alichangia wiki hii dala milioni 10 kwa wahanga wa maafa hayo.Alisema alihuzunishwa mno na msiba huo ambao pia ulimuathiri sana kwa kuwa hata bodi-gadi wake,watoto wake 2 na mkew wa bodi-gadi wake huyo ni miongoni mwa maalfu walipoteza maisha.

Schumacher alisema mlinzi wake huyo-Burkhard Cramer,aliekua na umri wa miaka 44 alifariki katika kisiwa cha Thailand cha Pukhet.

Idadi ya waliofariki katika msiba huu uliozuka desemba 26 umechukua maisha ya zaidi ya watu

1.56000.

Michael Schumacher,alichangia pia dala milioni 1 kwa waliokumbwa na maafa ya mafuriko kandoni mwa mto Elbe mashariki mwa Ujerumani hapo 2002 na kwa shirika la UNESCO la UM.

Hatahivyo, Michael Schumacher,amewahi kukosolewa pamoja na baadhi ya wanaspoti maarufu wa Ujerumani kama vile Boris Becker, kuamua kuishi n’gambo na kukwepa kwa njia hiyo kulipa kodi za mapato katika hazina ya Ujerumani.

Stadi wa zamani wa timu ya Taifa ya Ufaransa alieibuka bingwa wa dunia na bingwa wa Ulaya na Ufaransa na klabu-bingwa ya Ulaya na dunia na Bayern Munich Bixente Lizarazu ameamua kurejea kuichezea Bayern Munich.Lizarazu,beki wa shoto aliacha Munich kuhamia Olympique Marseille, miezi 6 iliopita na kati ya wiki hii ametangaza anarejea Münich.Alijiunga na Marseille, kwa mkataba wa miaka 2.kwanini anaiacha mkono marseille,haikufahamika.,

Mwishoe, kisa cha mchezaji wa dansa ya barafuni wa asili ya Tanzania mwishoni mwa wiki hii kutawazwa bingwa wa Ujerumani:

Robin Szolkowy baba yake asili yake ni tanzania na pamoja na msichana Aljona Sawtschenko-wote kutoka mji wa Ujerumani mashariki wa Chemnitz,wanapania mwishoni mwa wiki hii kutawazwa mabingwa wa Ujerumani katika mashindano ya barafuni.Wakidansa na kuteleza barafuni kwa wimbo maarufu kutoka ile filamu ‘Casablanca’ Robin mwenye umri wa miaka 25 na mwenzake Aljona Sawtschenko, wanataraji kuwafurahisha mahakimu na kuibuka washindi.Wote wawili wakiibuka washindi, wanatazamia kuiwakilisha Ujerumani katika taji la ubingwa wa Ulaya baadae mwezi huu huko Turin,Itali.wakiwika huko watakata tiketi yao ya kushiriki katika mashindano ya barafuni huko Moscow,mwishoni mwa mwezi machi.

Robin Szolkowy akiwa na rangi nyeusi na mwenzakcha aina pekee katika mashindano haya huko Oberstdorf.

Na kwa taarifa hiyo, ndio sina budi kuishia hapo kwa leo kutoka ukaguzi huu wa matokeo muhimu ya michezo wiki hii.