1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FINALI YA KOMBE LA KLABU BINGWA AFRIKA

28 Oktoba 2005

Jumamosi hii , mjini Sousse,Tunisia, inachezwa duru ya kwanza ya finali ya Kombe la klabu bingwa barani Afrika kati ya Etoile Sahel ya Tunisia na Al Ahly ya Misri;Bundesliga-Ligi ya Ujerummani itakuwa uwanjani huku mabingwa Bayern Munich wakimenyana na FC Cologne;Halamsahauri kuu ya olimpik Ulimwenguni (IOC) yaupinga kuingiza mchezo wa mabondia kwa wanawake katika orodha ya michezo ya Olimpik na Afrika Kusini inataka kuipiku New Zealand kuwa Taifa la kwanza kuandaa mKombe la Dunia la rugby mara 2.

Sousse,Tunesia:

Etoile Sahel ya Tunisia inacheza nyumbani jioni hii katika duru ya kwanza ya finali ya Kombe hilo ikijua kwamba lazima itambe leo nyumbani ikiwa inataka kuvaa taji hili la africa kama timu yao ya taifa.Kipa wao Austin Ejide alikwishawaonya wenzake kabla firimbi kulia jioni hii kuanzisha mpambano huu kwamba Etoile inabidi kutia magoli mengi ili kuwa na mwanya mkubwa kabla duru ya pili mjini Cairo nyumbani mwa Al Ahly hapo Nov.12..Kwahivyo, kuishangiria leo Etoile sahel, umati wa mashabiki hadi 40.000 ukitazamiwa kusheheni katika mji wa mwambao wa pwani ya Mediterranian wa Scusse.

Etoile Sahel ilicheza pia finali ya mwaka jana ya Kombe hili lakini ilipokonywa Kombe na mabingwa wa Nigeria Enyimba.Kipa Ejide, aliwakumbusha wenzake kwamba Etiole ilishindwa katika duru ya kwanza kushinda kwa uwazi zaidi wa magoli.Etoile iliishinda Enyimba kwa mabao 2:1 lakini mwiashoe, zilisimama sare na katika hukumu ya mikwaju ya penalty, Enyimba iliitoa Etoile.

Leo basi,Etoile impania kuishinda Al Ahly alao kwa mabao 2 wazi ili wakishindwa mjini Cairo,wasishindwe kwa magoli mengi.

Al Ahly wameshatawazwa mabingwa wa kombe la Afrika mara 3 na wanaingia uwanjani jumamosi hii kutetea rekodi yao ya kutofungwa kwa muda wa miezi 15 katika mechi 49 -ya leo iwe ya 50.Hakuna dalili kuwa Al Ahly itawaachia watunesia kuwatilia kitumbua chao mchanga.

Katika safu yao kuna watiaji magoli hatari:Wana Moteab alietia mabo 6 katika kinyan’ganyiro hiki na Mohamed Barakat alietia mabao 5.Kwahivyo, kipa Ejide wa Etoile Sahel, ana jukumu kubwa binafsi kulinda lango lake.

Mshindi wa duru ijayo Nov.12, ndie atakaewakilisha bara la Afrika katika finali za Kombe la dunia mjini Tokyo,japan hapo desemba.Atatarajia kuchota dala milioni kadhaa na hivyo, ni vigumu kwa Al Ahly kutowika siku hiyo nyumbani.Al Ahly itatapia alao kutoka sare leo na kumaliza udhia nyumbani Cairo.Kwa Etoile haitatosha.

Ikilinyakua Kombe hili Al Ahly kwa mara ya 4, itakua klabu ya pili baada ya Zamalek pia ya misri kufanya hivyo. Isitoshe, itakua ishara njema kwa Misri,itakayokuwa mwenyeji wa kombe la Afrika la Mataifa januari mwakani .Ili kuwasili katika finali ya leo,Al Ahly , ilishinda mechi 8 na kutoka sare mara 4 .Ilitolewa jasho tu na Raja Casablanca ambamo bao la dakika ya mwisho la Moteab liliwanusuru.

Nigeria imeahirisha finali ya leo jumamosi ya Kombe la Nigeria ili kuomboleza kifo cha abria 117 katika ndege iliopatwa na ajali mwishoni mwa wiki iliopita pamoja na kifo cha mke wa rais Obasanjo.

Finali ya leo ilikuwa iwe kati ya Enyimba FC na Lobi FC .

Senegal iliopigwa kumbo nje ya kombe lijalo la dunia,imeamua kumbakisha kocha wake wa mpito Abdoulaye Sarr hadi kumalizika Kombe la Afrika la mataifa mjini Cairo hapo Januari-Februari mwakani.Hii ni kwa muujibu wa taarifa ya kati ya wiki hii aliotoa waziri wa michezo wa senegal Amara Daouda Faye.

Sarr aliteuliwa kocha wa muda tu baada ya kutimuliwa Guy Stephen hapo Juni pale Senegal ilipomudu sare tu na Togo katika kinyan’ganyiro cha kuania nafasi za Kombe la dunia.Amara Traore makamo wa kocha Sarr, atasalia pia .

“Mkataba wa makocha hao 2 utadumu hadi mwisho wa februari hapo mwakani.”

Senegal katika Kombe hilo lijalo la Afrika la mataifa imeangukia kundi moja na Ghana,Nigeria na Zimbabwe-mojawapo ya makundi magumu.

BUNDESLIGA-LIGI YA UJERUMANI:

Mwishoni mwa wiki iliopita, Bayern Munich ilirudi kileleni mwa ngazi ya Ligi baada ya Bremen kutoka suluhu tu.Ikiwa na jumla ya pointi 25 kwa 23 za Bremen, wakati Munich jumamosi hii inamenyana na FC Cologne.Ingawa Cologne inacheza nyumbani,lakini itahitaji bahati kubwa kuepuka pigo jengine.Kwani,mwishoni mwa wiki iliopita, Cologne ilizabwa mabao 6:3 na Frankfurt na hivyo haimudu kushindwa tena,lakini kutamba mbele ya Bayern Munich pia si kazi rahisi.

Baada ya kuzabwa mabao 6:0 kati ya wiki na Frankfurt katika kombe la Taifa, makamo bingwa Schalke wana miadi jioni hii na Hamburg.Hamburg iko pointi 4 nyuma ya Munich na wamekuwa vigumu kushindwa nyumbani katika uwanja wao wa AOL Arena.Hamburg ina kasoro moja, kwavile bado inabidi kucheza bila stadi wao wa Holland Rafael van der Vaart.

Bremen iliopo nafasi ya pili nyuma yxa Bayern Munich ilihitaji mikwaju ya penalty kuitimua Wolfsburg juzi nje ya Kombe la shirikisho baada ya kubakia sare 2:2.Jioni hii lakini, inacheza na Frankfurt.

Stuttgart iliopigwa kumbo nje ya kombe la taifa na klabu ya daraja ya pili Hansa Rostock,inacheza nyumbani na Hertha Berlin wakati Borussia Dortmund ina miadi na Borussia Mönchengladbach.Kaiserslauten inacheza na Bayer Leverkusen.

Mapambano 2 yatakamilisha kalenda ya mwishoni mwa wiki hii hapo kesho:Armenia Bielefeld itacheza na Hannover na Mainz itaikaribisha nyumbani FC Nüremberg.Nürember ndio inayoburura mkia wa Ligi wakati huu.

Nje ya dimba, jaraibio la kuanzisha mabondia katika orodha ya michezo ya olimpik ya mwaka 2008 mjini Beijing limeshindwa.

Hatahivyo, Halmashauri Kuu ya olimpik Ulimwenguni (IOC) ime wacha mlango wazi juu ya uwezekano wa kuingiza ringi ya mabondia ya wanawake katika michezo ya 2012 mjini London.

Pia IOC ilimpokonya medali ya dhahabu mwanariadha wa Marekani Jerome Young, alioshinda wakati wa michezo ya olimpik ya Sydney, Australia, 2000 kwa kugunduliwa na madhambi ya doping.Young alikimbia katika timu ya kupokezana ya Marekani ya mita 400X4.2003 ilifichuliwa kwamba, Young amekutikana ametumia madawa ya kutunisha misuli na ili kuongeza kasi.

Bingwa mara 2 wa New york marathon,mkenya Margaret Okayo, alitangaza kati ya wiki kwamba hatashiriki Novemba 6 katika mbio za mwaka huu za NY marathon upande wa wanawake. Alinukuliwa kusema,

“Sikupona barabara tangu michezo ya olimpik ya mwaka jana.”

Okayo alishinda mbio za marathon za New York 2001 na 2003.Na ndie anadhibiti rekodi ya mbio hizo kwa muda wake wa masaa 2:22:31.

Tumalizie na Kombe la dunia la mchezo wa rugby:

Nahodha wa timu ya springboks ya Afrika Kusini,Francois Pienaar ana yakini kwamba faida nono za fedha zinazotokana na kuandaa kwa Kombe la dunia la rugby 20011 nchini Afrika Kusini kutatosha kulivutia shirika la kimataifa la mchezo huo kuipa kura Afrika kusini mwezi ujao.Afrika Kusini na NZ zinashindana kuania nafasi hiyo ili kila moja iwe imeanaa mara ya pili.Japan pia inaania kuandaa kwa mara ya kwanza Kombe la dunia la rugby.Shirikisho la kimataifa la mchezo wa rugby, IRB litapiga kura hapo Novemba 17 kuamua wapi Kombe la dunia litaaniwa 2011.Pienaar aliiongoza Afrika kusini kutwaa Kombe la dunia la rugby,nyumbani 1995.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW