Fletcher azungumzia misaada na jeshi la Sudan
12 Novemba 2025
"Ninakaribisha sana mazungumzo ya maana na yenye tija niliyoyafanya na Burhan, yaliyolenga kuhakikisha kwamba tunaweza kuendelea kufanya kazi kila mahali kote Sudan ili kutoa njia huru na isiyoegemea upande wowote kwa wale wote wanaohitaji sana msaada wa kimataifa," Ndivyo alivyosema Tom Fletcher katika video iliyotolewa na Baraza la Mpito la Sudan. Kauli ya afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ilikuja baada ya kukutana na Burhan huko Port Sudan.
Fletcher aliwasili Sudan Jumanne kwa ziara ya wiki moja, akiahidi kuunga mkono juhudi za amani, kuheshimu katiba ya Umoja wa Mataifa, na kushinikiza timu za Umoja wa Mataifa kupata ufikiaji na ufadhili wanaohitaji ili kuokoa maisha ya raia wa Sudan katika maeneo yote ya mapambano ya vita.
Kulingana na baraza la mpito ya Sudan linaloungwa mkono na jeshi, wakati wa mkutano huo, Burhan alisisitiza umuhimu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kuheshimu uhuru wa Sudan na maslahi ya kitaifa, kutokana na kile kilichotokea katika jiji la El-Fasher.
Fletcher pia alikutana na wanadiplomasia wa Misri kujadili njia za kuongeza misaada, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wizara ya mambo ya nje ya Cairo. Burhan pia alikutana na naibu mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP, Carl Skau, ambaye alipongeza majadiliano yao ya uaminifu na yenye tija.
Serikali ya Sudan inayoungwa mkono na jeshi iliwafukuza maafisa wawili wakuu wa WFP mwezi uliopita, ikitangaza kuwa "watu wasiostahili", licha ya shirika hilo kuonya kwamba Wasudan milioni 24 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Juhudi za utoaji misaada huenda zikasambaratika
Wakazi waliohamishwa kutoka eneo la Darfur Kaskazini nchini Sudan lililokumbwa na vita wameelezea kuwa wanahitaji kwa dharura msaada mkubwa huku shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM likionya kuwa shughuli za sasa za kibinadamu katika eneo hilo zilikuwa karibu na kusambaratika.
Batoul Mohamed, mfanyakazi wa kujitolea mwenye umri wa miaka 25 katika kambi ya wakimbizi ya Diba Nayra huko Tawila., alisisitiza kuwa vifaa bado havitoshi. "Baadhi ya watu wanasema hawajapata chakula chochote, na kwa kweli, kuna watu wengi waliokimbia makazi yao ambao wanahitaji msaada mkubwa zaidi. Tunatoa wito kwa mashirika ya kimataifa na mashirika mengine ya kibinadamu kuyasaidia mashirika ya hisani yanayotoa vyakula ili yaweze kuwahudumia idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao katika siku za hivi karibuni."
Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM lilionya jana Jumanne kwamba juhudi za kibinadamu katika eneo la Darfur Kaskazini nchini Sudan lililokumbwa na vita zinaweza kusimama kabisa kama ufadhili wa haraka na uwasilishaji salama wa vifaa vya misaada hautahakikishwa.
IOM ilisema katika taarifa kwamba licha ya mahitaji kuongezeka, shughuli za kibinadamu sasa ziko karibu kuporomoka na maghala yanakaribia kuwa matupu, misafara ya misaada inakabiliwa na ukosefu wa usalama mkubwa, na vikwazo vya kuyafikia maeneo vinaendelea kuzuia utoaji wa misaada ya kutosha.
IOM ilisema ufadhili zaidi unahitajika ili kupunguza athari za kibinadamu za vita kati ya jeshi la Sudan na wapiganaji wanamgambo wa Rapid Support Forces, RSF. Shirika hilo limeonya kuhusu janga kubwa zaidi ikiwa wito wake hautazingatiwa.