1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Flora Nwapa: Mama wa fasihi ya kisasa ya Kiafrika

Yusra Buwayhid
28 Aprili 2020

Mwandishi wa Kinaijeria Flora Nwapa ni mwanamke wa kwanza wa Kiafrika kuchapisha kitabu kwa Kiingereza. Kazi yake ilisafisha njia kwa wanawake wengine Afrika.

Flora Nwapa: Mama wa fasihi ya kisasa ya Kiafrika

02:22

This browser does not support the video element.

Flora Nwapa aliishi miaka gani?

Flora Nwapa alizaliwa mnamo mwezi Januari mwaka 1931 katika mji wa Oguta, jimbo la Imo, Nigeria Mashariki. Aipata elimu yake ya msingi katika miji ya Oguta, Port Harcourt pamoja na Lagos. Baadae alipata elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Ibadan, Nigeria pamoja na Chuo Kikuu cha Edinburgh huko Uskochi. Nwapa alifariki kutokana na nimonia akiwa na umri wa miaka 62 mnamo mwezi Oktoba mwaka 1993.

Je, Nwapa aliandika mada gani katika riwaya zake?

Kupitia vitabu vyake, Flora Nwapa alijaribu kubadilisha jinsi wanawake wanavyoelezwa katika simulizi za waandishi wa kiume wa Kiafrika ambao kazi zao zilikuwa zimejaa aina tofauti za ubaguzi kuhusu mwanamke wa Kiafrika. Riwaya zake kama vile Efuru na Idu zilipinga taswira ya jadi inayomueleza mwanamke wa Kiafrika kama mtu anayeishi chini ya vivuli cha wanaume kwa sababu anaonekana kuwa mtiifu na asiyeweza kuchangia kwa namna yoyote.

Asili ya Afrika | Flora Nwapa

Miongoni mwa vitabu vya Nwapa, vipi ni maarufu?

Mojawapo ya riwaya maarufu zaidi ya Flora Nwapa ni Efuru. Inasimulia maisha ya mwanamke anayejiweza vya kutosha hadi kumfadhili kifedha mume wake pamoja na baba yake. Katika riwaya hiyo ya Efuru, mwanamke huyo anapinga mitizamo yote ya kijadi katika jamii za Kiafrika na kujenga picha inayoonesha kuwa mwanamke pia anaweza kutumia akili yake mwenyewe bila ya usaidizi wa mwanaume. Mwanamke huyo anafaynya maamuzi kadhaa katika maisha yake kulingana na anvyoona kwake ni sahihi, badala ya kuendekeza mitazamo ya kijadi katika jamii za Kiafrika. Vitabu vyake vingine vya riawaya ni pamoja na  Idu, Never Again, One Is Enough na Women Are Different.

Asili ya Afrika | Flora Nwapa

Flora Nwapa anakumbukwa amewacha kumbukumbu gani?

Nwapa anakumbukwa zaidi kwa kuanzisha mtindo wa kisasa wa kumueleza mwanamke katika fasihi, ambao hadi hii leo unatumiwa na waandishi wa riwaya wa kike nchini Nigeria. Nwapa alifanya hivyo kubadilisha namna mbaya mwanamke wa Kiafrika alivyokuwa akiandikwa katika uwanja wa fasihi unaoongozwa na wanaume.

Flora Nwapa: Mama wa fasihi ya kisasa ya Kiafrika

This browser does not support the audio element.

Je, Flora Nwapa alikuwa mtetezi wa wanawake?

Flora Nwapa binafsi hakutaka kutambulika kama mtetezi wa wanawake, lakini baadhi ya vitabu vyake ni maarufu kwa kuetetea haki za wanawake. Katika kazi yake, huwa anamtumia mhusika wa kike kupinga mazoea ya kitamaduni yasiyofaa ambayo wanawake wa Kiafrika hukabiliana nayo hasa akiwa mjane na akiwa amekosa watoto maisha mwake. Umahiri wake huo wa kupinga mazoea ya kitamaduni yanayomkandamiza mwanamke katika riwana zake, hadi hii leo unaendelea kuwahamasisha watetezi wa haki za wanawake nchini Nigeria.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW