FLORIDA:Kimbunga Rita kipo karibu kupiga pwani ya Florida na Cuba.
21 Septemba 2005Utawala wa Marekani umeeleza kuwa kimbunga Rita kimezidi kujizatiti na kuelekea kuwa tufani itakayoambatana na mvua kubwa pamoja na upepo mkali na kinaelekea kushambulia Florida na maeneo ya kaskazini-magharibi mwa Cuba.
Watabiri wa hali ya hewa wameeleza kuwa wanatazamia kimbunga Rita kitaongezeka nguvu zaidi katika muda wa saa 24 zijazo,huku kikiwa kina mwelekeo wa kupiga Ghuba ya Mexico.Pia kimbunga hicho huenda kikapiga maeneo ya Lousiana ama Texas itakapofika mwishoni mwa wiki na kwa hivi sasa watu wameshaanza kuzihama nyumba zao katika mji Gelveston,Texas ulio ufukweni mwa bahari.
Rais George Bush wa Marekani alipotembelea Louisiana kwa mara ya tano tangu kimbunga Katrina kilipovuruga eneo hilo wiki tatu zilizopita,alisisitiza kuwa maandalizi ya dharura kukabiliana na athari zitakazoletwa na kimbunga Rita yanaendelea vizuri.
Utawala wa Bush ulishutumiwa kwa kutokuwa wepesi kukabiliana na maafa yaliyoletwa na kimbunga Katrina.