1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Francois Bayrou ndiye waziri mkuu mpya Ufaransa

13 Desemba 2024

Rais Emmanuel Macron amemtangaza Francois Bayrou kuwa waziri mkuu mpya siku chache baada ya Michel Barnier kuondolewa katika nafasi hiyo na bunge kwa kura ya kutokuwa na imani naye wiki iliyopita.

 Francois Bayrou
Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa Francois BayrouPicha: Eliot Blondet/abaca/picture alliance

Rais Emmanuel Macron amemtangaza Francois Bayrou kuwa waziri mkuu mpya siku chache baada ya Michel Barnier kuondolewa katika nafasi hiyo na bunge kwa kura ya kutokuwa na imani naye wiki iliyopita

Tangu awali mwanasiasa Francois Bayrou mwenye miaka 73 na  kiongozi wa chama cha siasa za mrengo wa kati cha Democratic Movement ndiye aliyeonekana kuwa chaguo la Rais Macron katika kuchukua nafasi ya waziri mkuu. 

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwa na waziri mkuu mpya Francois BayrouPicha: abaca/picture alliance

Bayrou ambaye ni mshirika Macron amekuwa akimuunga mkono rais huyo tangu alipoingia madarakani  mwaka 2017. Amekuwa mtu mashuhuri katika siasa za Ufaransa kwa miongo kadhaa na uzoefu wake unaonekana kuwa muhimu katika juhudi za kurejesha utulivu wa kisiasa nchini humo.

Muda mfupi baada ya kutangazwa kuchukua nafasi hiyo, ofisi ya Macron ilisema katika taarifa kwamba Bayrou sasa amepewa jukumu la kuunda serikali mpya.

Soma zaidi. Rais Macron kumtangaza waziri mkuu mpya wa Ufaransa

Lakini wananchi wa Ufaransa wameupokea vipi uteuzi huo wa Francois Bayrou.

Raia wawili wakiwa sokoni mjini walipoulizwa swali hilo walisema '' Ilipaswa kuwa mtu kutoka mrengo wa kushoto. Wafaransa walipiga kura mwezi Juni, na wengi, hata kama huwezi kuamuru hivyo, walielekea kuwa upande wa kushoto'' 

"Katika hali ya sasa, nadhani yeye ndiye mtu anayeweza kutoa jibu la kukosekana kwa utulivu huu wa kisiasa,  kwa sababu ana marafiki katika mirengo ya kushoto na kulia.Kwa hivyo ikiwa atafanikiwa hadi kwenye uchaguzi ujao, anaweza kuwa mtu mzuri."

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu wa zamani Michel Barnier alijiuzulu kufuatia kura ya bunge ya kutokuwa na imani naye iliyochochewa na migogoro ya bajeti katika bunge la kitaifa na kuiacha Ufaransa bila serikali inayofanya kazi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwa na waziri mkuu mpya Francois BayrouPicha: abaca/picture alliance

Soma zaidi. Rais Macron aahidi kumtangaza Waziri Mkuu mpya

Bayrou anatarajiwa sasa kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa vyama vya kisiasa katika siku zijazo ili kuchagua baraza jipya la mawaziri.

Ufaransa imekuwa kwenye mkwamo wa kisiasa tangu ilipofanya uchaguzi mwezi Juni na Julai na kushindwa kutoa matokeo ya wazi huku masuala kama vile hali mbaya ya kiuchumi ikiendelea kufukuta nchini humo.

Kufuatia hali hiyo upinzani nchini Ufaransa umekuwa ukimshinikiza Rais Macron ajiuzulu lakini alipohutubia taifa hivi majuzi baada ya kuondolewa kwa waziri mkuu barnier, Macron  aliapa kwamba  yeye atasalia madarakani hadi pale muhula wake utakapomalizika mwaka 2027.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW