1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
BiasharaKimataifa

Francoise Bettencourt Meyers: Mwanamke tajiri zaidi duniani

12 Januari 2024

Bilionea wa urembo nchini Ufaransa, Francoise Bettencourt Meyers ni mwanamke wa kwanza kufikia utajiri wa dola bilioni 100 za Kimarekani. Lakini mwanamke huyu ni nani na amekuwaje mwanamke tajiri kabisa ulimwenguni?

Mrithi wa L'Oreal Francoise Bettencourt Meyers ndiyo mwanamke wa kwanza kumiliki utajiri wa dola bilioni 100.
Francoise Bettencourt Meyers ni mwenyekiti wa kampuni miliki ya familia yake, Tethys, ambayo inamiliki theluthi moja ya hisa za L'Oreal.Picha: Bernard Patrick/abaca/picture alliance

Pesa huzaa pesa. Hakuna mtu anayeweza kuuthibitisha msemo huu zaidi ya bilionea wa Kifaransa, Francoise Bettencourt Meyers, ambaye kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba alivunja ukomo wa bilionea 100 za Kimarekani na kuwa mwanamke wa kwanza kabisa kuwahi kumiliki utajiri huo mkubwa, kwa mujibu wa Faharasa ya Mabilionea ya Bloomberg. Mwaka 2023, aliongeza dola bilioni 28.6 kwenye mabilioni aliyokwishakuwa nayo.

Hata kama kufikia tarehe 4 Januari 2024 alikuwa ameshuka hadi bilioni 96.2, bado Bettencourt Meyers ndiye mwanamke tajiri mkubwa kabisa duniani, na anashika nafasi ya 13 ya mabilionea wote, kwa mujibu wa hisabu za Bloomberg. Jarida la Forbes, ambalo pia hukusanya orodha ya mabilionea, linamuweka kwenye nafasi ya 15. Kwa hisabu yoyote ile, yeye ni mmoja kati ya wanawake wachache waliomo kwenye orodha hiyo.

Ni vipi Bettencourt Meyers aligeuka tajiri?

Bettencourt Meyers mwenye umri wa miaka 70 ni mjukuu wa muanzilishi wa kampuni ya L'Oreal. Mama yake, Liliane Bettencourt, alikuwa ndiye mwanamke tajiri kabisa ulimwenguni hadi anakufa mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 94, na kumuachia binti yake utajiri wa dola bilioni 40, sehemu kubwa ikiwa kwenye hisa katika kampuni hiyo ya L'Oreal.

Mwana na mwana, kila mmoja wao mwanamke tajiri zaidi duniani wakati wa enzi zao.Picha: Mousse/abaca/picture alliance

Bettencourt Meyers mwenye umri wa miaka 70 sio tu mjukuu wa mwanzilishi wa L'Oreal, Eugene Schuleller, bali - kama alivyo mama yake - naye ni mtoto pekee. Hiyo inamaanisha kuwa hisa zote za mama yake zilikuwa zake. Sasa anamiliki asilimia 34.7 za hisa za kampuni hiyo ya vipodozi na urembo.

Yeye ni kizazi cha tatu kwa familia kujihusisha na kampuni hiyo na ni makamu mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi yenye wajumbe 16. Wanawe wawili wa kiume, ambao ni sehemu ya kizazi cha nne, wamo pia kwenye bodi hiyo.

Soma pia: Oxfam: Mabilionea watajirika maradufu wakati wa Covid-19

Bettencourt Meyers amepokea magawio makubwa ya kampuni hiyo kwa mfumo wa fedha taslimu kwa miaka mingi, lakini kitu cha thamani kubwa kabisa anachomiliki ni mtaji wa L'Oreal.

L'Oreal ndiyo kampuni kubwa zaidi ya urembo duniani

Kampuni hiyo ya Kifaransa iliyoanzishwa mwaka 1909 ndiyo mtengenezaji mkubwa kabisa wa vipodozi na urembo duniani kwa sasa. Inamiliki bidhaa za Lancome, Kiehl's, Maybelline na Garnier. Imewaajiri zaidi ya watu 85,000 duniani. Mwaka 22, iliripoti kuwa na mapato ya zaidi ya dola bilioni 38.

Lakini si kwamba daima imekuwa ikitengeneza faida. Kwa miaka mingi, bei ya hisa zake ilikuwa imekwama. Lakini tangu mwaka 2011, hisa za kampuni hiyo zimekuwa zikipanda. Mwaka 2012, zilifikia euro 100, na tangu hapo zimekuwa zikipanda, hata wakati wa janga la UVIKO-19.

L'Oreal ilianzishwa mnamo 1909 na bado inamilikiwa na familia ya mwanzilishiPicha: Bildagentur-online/Schoening/picture alliance

Kufikia tarehe 19 Desemba mwaka jana, hisa zake zilifikia thamani ya euro 460 na kuipa kampuni hiyo mtaji wa zaidi ya euro bilioni 240. Hili ndilo jambo lililomgeuza Bettencourt Meyers kupindukia kiwango cha dola bilioni 100.

Hata hivyo, Bettencourt Meyers siye mtu tajiri mkubwa kuliko wote nchini mwake, Ufaransa. Nafasi hiyo inashikiliwa na Bernard Arnault, mmiliki wa kundi la makampuni ya mambo ya anasa, LVMH, ambaye kuna wakati alikuwa pia tajiri mkubwa kabisa duniani. Kwa sasa utajiri wake ni dola bilioni 179, kwa mujibu wa Bloomberg.

Safari ngumu kuelekea juu
Kwa Bettencourt Meyers, haikuwa rahisi, kupanda kileleni moja kwa moja. Wakati mwingine, kuwa tu mrithi haitoshi. Kwa miaka mingi, ameepuka jamii ya tabaka la juu, amenadika vitabu, na kujitahidi kujiepusha kuonekana hadharani.

Soma pia:Ripoti ya Oxfam: Wanawake hufanya kazi bure wakati mabilionea wakiongeza utajiri 

Licha ya hayo, alikuwa na uhusiano mbaya na mama yake. Mambo yalizidi kupamba moto katika mzozo wa hadharani wa familia yao, na kupamba vichwa vya habari duniani kote na kusababisha moja ya kashfa kubwa nchini Ufaransa. Ilikuwa ya kushangaza sana, kiasi cha kuitwa tu "L'affaire Bettencourt" na hivi karibuni iligeuzwa kuwa tamthilia ya sehemu tatu katika chaneli ya Netflix.

Kuanzia mwaka wa 2007, Bettencourt Meyers aliwashutumu watu kadhaa kwa kutumia vibaya afya ya akili ya mama yake inayozorota, shutuma ambazo wakati fulani zilimjumuisha hata aliyekuwa Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy. Mama na binti walisuluhisha ugomvi wao nje ya mahakama, na Bettencourt - pamoja na pesa zake, uwekezaji na mali - aliwekwa chini ya ulezi wa kisheria wa familia yake.

Baada ya moto mkali kuliunguza Kanisa la Notre Dame mwaka 2019, Bettencourt Meyers na L'Oreal waliripotiwa kutoa euro milioni 200 kwa ukarabati wake.Picha: Thierry Mallet/AP Images/picture alliance

Kutafuta urari sahihi

Wakati wa vita hivyo virefu vya kisheria, Bettencourt Meyers alisimama kidete na kutunza mali nyingi za mama yake. Leo, inaonekana ameweka kando mkasa huo wa mahusiano ya umma.

Tangu kifo cha mamake, Bettencourt Meyers amekuwa akisimamia kikamilifu na amejiingiza katika orodha mbalimbali za mabilionea mwenyewe tangu 2018. Katika miaka michache iliyopita, ameshuhudia utajiri wake wa kurithi wa dola bilioni 40 ukiongezeka zaidi ya mara mbili, kutokana na ongezeko la hisa ambalo halijawahi kutokea L'Oreal. Lakini kama kawaida kwenye soko la hisa, kile kinachopanda kinaweza kushuka.

Kando na hisa za L'Oreal, yeye na familia wamewekeza katika miradi mingine kupitia kampuni yao ya uwekezaji inayomilikiwa na familia, Tethys.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW