1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Frank Habineza- sauti adimu ya ukosoaji Rwanda

Sekione Kitojo
1 Agosti 2017

Zikisalia siku tatu kabla ya uchaguzi wa rais nchini Rwanda, vyama tisa vinashiriki na rais Paul Kagame wa chama cha RPF anatarajiwa kushinda.Chama cha Green Party cha Frank Habineza ndio chama pekee halisi cha upinzani.

Ruanda Frank Habineza
Kiongozi wa chama cha Green nchini Rwanda Frank HabinezaPicha: DW/J. Johannsen

Frank Habineza anagombea kiti  cha  urais  kwa  mara  ya kwanza  baada  ya  miaka  minane  ya  mapambano  kuweza kukiandikisha  chama  chake  na  kupata  nafasi ya  kuingizwa  katika makaratasi  ya  kupigia  kura. 

Frank Habineza  ni mwanaharakati  wa  kulinda  mazingira anayewania  kuwa  rais  wa  Rwanda.  Habineza  mwenye  umri  wa miaka  40  kiongozi  wa  chama  cha  Green Party  amekabiliana  na vitisho  vya  kuuwawa  na  ameshuhudia  waungaji  wake  mkono wakipigwa, wakifungwa  jela na  kulazimishwa  kuikimbia nchini  hiyo na  kwenda  kuishi  uhamishoni  katika  wakati  akijaribu  kuingia katika  uwanja  wa  kisiasa  nchini  rwanda  ambao  una udhibiti mkubwa.

Habineza (kulia) akiwa na wakili wake Antoinette Mukamusoni wakiwa mahakamani nchini Rwanda , mwaka 2015.Picha: DW/J. Johannsen

"Imekuwa  ni  safari  ngumu , na  pia  safari ya  hatari," ameliambia shirika  la  habari  la  Ufaransa  AFP  katika  mahojiano  katika  ofisi yake katika  mji  mkuu  Kigali, ambako  walinzi  wake wanalinda doria.

Alizaliwa  uhamishoni  nchini  Uganda , baba  yake  akiwa  ni  Mhutu na  mama  yake  Mtutsi, alirejea  nchini  Rwanda na  kusomea masuala  ya  utawala. Pia  alianza  kuwa mwanaharakati  wa  asasi za  kijamii , akifanya  kampeni  ya  ulinzi  wa  mazingira.

Habineza  alikuwa  mwanachama  wa  chama  btawala  cha Rwandan Patriotic Front RPF lakini  alijitoa  na  kujiunga  na  siasa za  upinzani  mwaka  2009  ili  kuweza  kuwa  na  chama  mbadala kwa  chama  tawala  ambacho  kinatawala  kwa  mkono  wa  chuma.

Mkutano wa kampeni wa chama tawala cha RPF , kinachoongozwa na rais Paul KagamePicha: Picture alliance/Zumapress/G. Dusabe

Mkono wa  chuma

Rais  Paul Kagame  amekuwa  akishutumiwa  kwa  kuzuwia  uhuru wa  kutoa  mawazo  na  kuzuwia  vyama  vya  upinzani. Mbali  na chama  cha  Habineza  cha  Green Party , vyama  vyote vya upinzani  vilivyosajiliwa  vinamuunga  mkono  Kagame.

"Tulipoanzisha  chama  tulipigwa katika  baadhi  ya  mikutano  yetu na  watu  ambao  walikuwa  na  silaha, watu  waliwekwa  korokoroni, walifungwa , wengine walikimbilia  uhamishoni," amesema  Habineza.

Chama  chake  kilizuiliwa  usajili  kabla  ya  uchaguzi  wa  mwaka 2010, na  muda  mfupi  kabla  ya  uchaguzi  mwili  wa  makamu  wa rais  wa  chama  cha  Green  Andre  Rwisereka  ulipatikana  ukiwa umeharibika  kabisa.

Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Picture alliance/AP Photo/E. Murinzi

Habineza , ambae  anasema  binafsi  pia  alipokea  vitisho vya kuuwawa , aliamua kukimbilia  Sweden mwezi  mmoja  baadaye ambako  familia  yake  hatimaye  ilipata  uraia.

Upinzani wabinywa Rwanda

Mwaka  2012  aliamua  kurejea  nchini  Rwanda. Amesema kumuacha  mkewe na  watoto , ikiwa  ni  pamoja  na  mtoto  wake wa  kiume  wa   mwaka  mmoja, ilikuwa  kitu  kigumu  sana  ambacho amewahi  kufanya.

Chama  chake  hatimaye  kilifanikiwa  kusajiliwa  mwaka  2013, mwezi  mmoja  tu  kabla  ya  uchaguzi  wa  bunge, ambapo Habineza aliamua  kutoshiriki  kutokana  na  ukosefu wa  muda  wa matayarisho.

Raia wa Rwanda wakiandamana mjini Madrid wakionesha mikono yenye damu kuashiria ukatili unaofanya na serikali ya Rwanda.Picha: AP

Mwaka  2015 alikuwa  mgombea  pekee  kushiriki  katika  kura  ya maoni  ya  mageuzi  ya  katiba  inayomruhusu Kagame  kuwania muhula  wa  tatu madarakani. Habineza  alirejesha  uraia  wa Sweden  ili  kuweza kushiriki  katika  uchaguzi  wa  mwaka  huu 2017 na  ameendelea  kukabiliana  na  vikwazo  chungu nzima katika kila  hatua.

Mwaka  2016  aliotolewa  kutoka  katika  jengo  la  ofisi  yake  na nyumbani  kwake  bila  kupewa taarifa ,  na  kufanya  kampeni  pia imekuwa  taabu  kwake.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afp

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW