Frankfurt nafasi ya tatu baada ya kuichapa Cologne
15 Februari 2021Eintracht Frankfurt imeimarisha matumaini yake ya kujikatia tiketi ya kucheza kandanda la Ligi ya Mabingwa msimu ujao kwa kupanda katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa liigi, kufuatia ushindi wa 2 – 0 dhidi ya Cologne jana. Ulikuwa ni ushindi wa saba katika mechi nane za mwaka huu wa 2021 na kurefusha rekodi yake ya kutopoteza katika mechi kumi za ligi.
Nayo Nambari nne kwenye ligi Wolfsburg ilikamatwa kwa sare tasa nyumbani dhidi ya Borussia Moenchengladbach. Frankfurt iko mbele ya Wolfsburg kwa tofauti ya magoli.
Timu nyingine inayotafuta ligi ya mabingwa ni Borussia Dortmund, na mwishoni mwa wiki, fomu yake mbovu iliendelea baada ya kutekwa kwa mabao 2 - 2 na Hoffenheim. Ni matokeo ya kutia wasiwasi kwa Dortmund kwa sababu ya ushindani uliopo na nahodha wake Marco Reus anafahamu hilo
Nitasema tena, sote ni binaadamu na kama hauna hisia ya mafanikio katika mchezo, huwa haina umuhimu kwa mtu yeyote, lakini jukumu la kwanza ni kujaribu kupambana katika kila mpambano na kupata ujasiri kutokana na hilo. Mechi ingeenda upande mwingine lakini hatujaridhika..
Frankfurt na Wolfsburg zina pointi 39 kila mmoja na pengo la pointi tatu mbele ya Bayer Leverkusen ambayo iko nafasi ya tano, wakati Borussia Mönchengladbach iko nafasi ya saba lakini ina pointi sawa na Dortmund katika nafasi ya sita zikiwa na 33. Mainz ambayo ni ya pili kutoka mkiani ilitoka nyuma mabao mawili na kulazimisha sare ya 2 – 2 na Leverkusen
"Ufafanuzi ni kuwa tulicheza vibaya mchezo wote, hata kabla ya kuwa kifua mbele 2 - 0. Tayari katika kipindi cha kwanza hatukucheza vizuri na nilisema hilo katika muda wa mapumziko. Tulikuwa hovyo kabisa katika umiliki wa mpira. Kwa hivyo haukuwa mchezo wetu bora lakini kama bado uznaongoza 2 - 0 katika dakika ya 85 basi haupaswi kuusalimisha."
Timu pekee inayoonekana kwa sasa kuiwekea mbinyo Bayern Munich, ni RB Leipzig ambayo ilipata ushindi wa 2 – 1 na kupunguza mwanya kati yake na vigogo Bayern kufikia pointi nne. Ijapokuwa Bayern wanashuka dimbani leo kupambana na Arminia Bielefeld. Julian Nagelsmann ni mwalimu wa Leipzig
Nadhani kwa jumla mchezo ulikuwa mzuri. Kulikuwa na watu kadhaa kwenye klabu ambao walikuwa na uwoga kuhusu jinsi vijana wangeuchukulia mchezo dhidi ya Augsburg. Niliwaambia wawe watulivu, vijana wanasikiliza na unaweza kuona hilo. Waliingia mchezoni wakiwa sawa, na nguvu na kujilinda vyema.
Hata hivyo ni habari kuhusu mmoja wa wachezaji wake ndizo zilizogonga vichwa vya habari. Bayern imetangaza jana kuwa beki wa Leipzig Mfaransa Dayot Upamecano atajiunga na miamba hiyo msimu ujao kwa mkataba wa miaka mitano, baada ya mabingwa hao watetezi kukubali kulipa kitita cha euro milioni 42.5 cha kumuachilia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22.
AFP, Reuters, DPA, AP