Frankfurt wawanyeshea Hoffenheim nyumbani
8 Februari 2021Ushindi huo umewapelekea Frankfurt kukwea hadi katika nafasi ya nne katika jedwali la Bundesliga wakiwa na pointi 36 na ni ushindi uliomfurahisha sana kocha wao Adi Hütter.
"Huu ndio wakati ambapo kila kitu kinakwenda vizuri hata jinsi mchezo wetu unavyokwenda: Hata tukiwa nyuma, tutarudi katika mchezo tu. Ushindi huu unatupa nguvu na utulivu kwa kiasi fulani, mambo ambayo tunayahitaji na inafurahisha sana kuitazama timu yetu ikicheza kwa sasa ila tutapoteza mechi tena wakati mmoja. Lakini kwa sasa ni vigumu sana kutushinda," alisema Hütter.
Hoffenheim haikuwapa wakati mgumu wapinzani wao
Naye mkufunzi wa Hoffenheim Sebastian Hoeneß alikuwa na haya baada ya timu yake kupoteza nyumbani.
"Hatujacheza vyema lakini hadi ilipofikia dakika ya 60 ambapo tayari tulikuwa chini doli moja kwa matatu na mechi ilikua ishaamuliwa wakati huo, hatukuwa vibaya sana. Lakini hatukuwapa wakati mgumu wapinzani wetu, mabao waliyofunga yalikuwa ya rahisi sana. Tunachostahili kufanya ni kuonyesha uwezo wetu ili mechi kama hizi ziende katika njia inayostahili," alisema Hoeneß.
Hapo Jumamosi Borussia Dortmund walikosa nafasi ya kutoa ushindani zaidi wa kuwania nafasi za kushiriki Champions League msimu ujao baada ya kuzidiwa nguvu na SC Freiburg walipokuwa ugenini katika uwanja wa Schwarzwald Stadion.
Na basi baada ya kipigo hicho Nahodha wa Dortmund Marco Reus alikiri hawakustahili kuishinda mechi hiyo.
Wapinzani wengine wa Dortmund walishinda mechi zao
"Tumeipoteza mechi. Katika dakika zote 90 hatukucheza vyema, Freiburg wamecheza vizuri sana. Hatukuisumbua safu ya ulinzi ya Freiburg na hatukucheza vizuri kuelekea kwene ushambuliaji, hatukufanikiwa katika hilo. Na tumevunjwa moyo sana kwa kuwa tumepoteza mwendelezo wa kushinda mechi mfululizo," alisema Reus.
Wapinzani wengine wa Dortmund katika kuwania nafasi hizo za nne bora, RB Leipzig walishinda mechi yao dhidi ya Schalke 3-0 huku Bayer Leverkusen, wao wakipata ushindi wa kishindo kwa kuwazaba VfB Stuttgart magoli 5-1. Leipzig kwa sasa wako kwenye nafasi ya pili na pointi 41 saba nyuma ya vinara Bayern Munich kisha wolfsburg ni wa tatu na pointi 38 halafu baada ya Frankfurt Bayer Leverkusen ni wa tano wakiwa na pointi 35. Peter Bosz ni kocha wa Leverkusen.
"Ushindi huu ulikuwa muhimu kwa ajili ya jedwali lakini pia nafikiri watu wameona kwamba leo timu ilikuwa na uhakika katika mchezo wake. Kuanzia mwanzo tumeweka shinikizo. Tumecheza mchezo mzuri sana, tumekuwa na nafasi nyingi sana za kufunga ila katika kipindi cha kwanza tulifunga mabao mawili tu, ilistahili kuwa magoli mengi. Ila ni matokeo ya kuridhisha kupata ushindi wa 5-2 nyumbani dhidi ya Stuttgart," alisema Bosz.