Frankfurt yapoteza fursa ya kusonga nafasi ya pili
5 Februari 2018Frankfurt sasa wamesalia katika nafasi ya sita wakati Augsburg wamepanda hadi nafasi ya saba, ikiwa ni nafasi moja tu nje ya eneo la kutafuta tikiti za moja kwa moja kucheza michuano ya Ulaya. Michael Gregoritsch ni mmoja wa wafungaji wa mabao ya Augsburg "Nadhani ilikuwa kazi ngumu sana leo. Nadhani tulistahili kabisa ushindi huo na nadhani idadi ya mabao pia iko sawa. Hatukuwapa nafasi yoyote ya kupua. Nadhani leo ulikuwa mchezo wa hali ya juu toka mwanzo na ilikuwa muhimu kuongeza kasi na ndio maana nadhani mambo yalikuwa mazuri".
Nambari mbili kutoka mkiani Hamburg sasa wamecheza mechi nane bila kupata ushindi, baada ya kutoka sare ya kufungana bao moja kwa moja na Hanover. Hamburg ambayo ndio timu pekee ya Bundesliga ambayo haijawahi kushushwa daraja sasa inajikuta katika hali mbaya kabisa. Jens Todt ni mkurugenzi wa spoti wa Hamburg "Nadhani umuhimu wa mechi haukufanya kazi ya wachezaji kuwa rahisi. Wengi walikuwa na uchovu miguuni. Timu yetu ilijaribu kila kitu lakini haukuwa mchuano rahisi. Na kisha hatukutumia vizuri nafasi za wazi za kufunga. Hata hivyo tulirudi tena mchezoni na hio ni habari nzuri. Bila shaka pointi moja haitoshi lakini tutaendelea kupambana".
Siku ya Jumamosi Bayern Munich waliendeleza uongozi wao kileleni baada ya kuichapa Mainz mabao mawili kwa sifuri. Ushindi huo una maana Bayern wameweka pengo la pointi 18 dhidi yao na nambari mbili Bayer Leverkusen na RB Leipzig. Mats hummels aliuzungumzia ushindi huo "Kwa miaka tisa nimekuwa nacheza dhidi ya Mainz, na sijawahi kuona mchezo ambao unapata ushindi kwa urahisi. Kuna msisimko mkubwa sana hapa, wa hisia na mpinzani mwenye shauku. Mchezo kama huu unafurahisha sana. Pamoja na hayo nimefurahi kwamba tumeweza kutoka na ushindi"
Leipzig walipata ushindi wa dakika za mwisho mwisho dhidi ya Borussia Moenchengladbach na kurejea katika kundi la timu nne za kwanza. Leverkusen walitokwa jasho katika sare yao ya sifuri kwa sifuri na Freiburg. Heiko Herrrlich ni mkufunzi wa Leverkusen "Tumeridhika sana na pointi moja. Tulijaribu kila kitu na tukashindwa kufunga bao kwa sababu ya ukuta uliowekwa. Tuliumiliki sana mpira na tukawa na nafasi kadhaa za kufunga mabao ambazo hatukuzitumia. Lakini hata hivyo nimeridhika sana"
Hata hivyo Leverkusen wanabakia katika nafasi ya pili baada ya Schalke kwa mara nyingine kupoteza pointi. Schalke ilichapwa mabao mawili kwa moja na Werder Bremen
Katika sehemu ya msimamo wa ligi, Wolfsburg walitoka sare ya bao moja kwa moja na VfB Stuttgart. Hoffenheim ilitoka sare ya bao moja kwa moja na Hertha Berlin. Siku ya Ijumaa, Borussia Dortmund ilipata ushindi muhimu wa mabao matatu kwa mawili dhidi ya wenyeji Cologne.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Gakuba, Daniel