Fritz Keller ajiuzulu wadhifa wa rais wa DFB
17 Mei 2021Rais anayeondoka wa shirikisho la kandanda Ujerumani - DFB Fritz Keller amesema chama hicho lazima kibadilike, baada ya kujiuzulu rasmi leo kuhusiana na matamshi aliyoyatoa akimlinganisha naibu wake na jaji mmoja mwenye sifa mbaya wakati wa enzi ya utawala wa Kinazi. Katika taarifa ndefu aliyoitoa, Keller amesema anaachia wadhifa wake kama rais ili DFB ifanye mwanzo mpya na muhimu.
Huku akikiri kuwajibikia matamshi yake tata, rais huyo anayeondoka pia ameshutumu hali iliyopo ya ombwe la uongozi katika shirikisho hilo lililokumbwa na kashfa na kutoa wito wa kufanyika mageuzi mapana. Keller alizusha hasira na miito ya kumtaka ajiuzulu baada ya kumlinganisha makamu wa rais wa DFB Reiner Koch na Roland Freisler, aliyekuwa mkuu wa mahakama ya chama cha Nazi katika miaka 1940s, katika mkutano wa mwezi uliopita.
AFP/Reuters/DPA/AP