1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoQatar

Götze, Moukoko na Füllkrug kwenda Qatar

Josephat Charo
10 Novemba 2022

Kocha Hansi Flick amekitaja kikosi chake kitakachokwenda Qatar kushiriki kombe la dunia la kandanda 2022 kwa matumaini ya kufanya vyema na kurejea kwa nguvu katika soka la dunia.

Bundesliga Dortmund Schalke Moukoko Tor
Picha: David Inderlied/dpa/picture alliance

Mshambuliaji wa klabu ya Borussia Dortmund, kinda Youssoufa Moukoko na mshambuliaji mwenzake wa klabu ya Werder Bremen Niclas Füllkrug wameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya soka ya Ujerumani Die Mannschaft kushiriki mashindano ya kombe la dunia Qatar. Mfungaji bao la pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Argentina katika fainali ya kombe la dunia 2014 huko Maracana, Brazil dhidi ya Argentina, Mario Goetze pia ameitwa tena katika kikosi kuiwakilisha Ujerumani.

Nahodha wa Dortmund Marco Reus na beki wa kati Mats Hummesla hawamo miongoni mwa wachezaji 26 waliotajwa na kocha Hansi Füllkrug kwa ajili ya mashindano hayo yanayoanza Novemba 20 hadi Desemba 18.

Moukoko, anayetimiza umri wa miaka 18 wiki ijayo, na Füllkrug, walitarajiwa kuitwa katka kikosi cha Ujerumani kwa sababu Timo Werner na Lukas Nmecha wameumia. Moukoko na Füllkrug wamekuwa katika fomu nzuri wakifunga mabao mengi na wanatarajiwa kuipa timu ya Ujerumani fursa kadhaa katika safu ya ushambuliaji wakati washindi hao mara nne wa kombe la dunia wakipania kurejea tena kwa nguvu kubwa katika soka la ulimwengu baada ya kupata matokeo mabaya katika kombe la dunia 2018 nchini Urusi ambapo walipigwa kumbo na kutolewa wakati wa mechi za makundi.

Niclas FüllkrugPicha: Maik Hölter/Team 2/IMAGO

Götze alitia kimyani bao la ushindi wakati wa fainali ya kombe la dunia 2014 dhidi ya Argentina na sasa anarejea katika timu ya taifa kwa mara ya kwanza tangu 2017 baada ya kuonyesha kiwango kizuri cha mchezo msimu huu wa sitini wa Bundesliga na klabu ya Eintracht Frankfurt.

Washindi wengine wa kombe la dunia 2014 ni mlindalango na nahodha Manuel Neuer na mchezaji mwenzake kiungo mshambuliaji wa klabu ya Bayern Munich, Thomas Müller ambao wote watacheza katika mashindano ya kombe la dunia kwa mara ya nne.

Miamba wa Bundesliga Bayern pia wametoa viungo wenye uwezo mkubwa Joshua Kimmich na Leon Goretzka, mchezaji nyota anayeinukia kwa kasi Jamal Musiala na washambuliaji Serge Gnabry na Leroy Sane.

Marco Reus anakosa kwa mara ya tatu mashindao makubwa ya kombe la dunia kutokana na jeraha alilolipata hivi majuzi na klabu yake ya Dortmund na mchezaji mwenzake Mats Hummels pia ameachwa nje ya kikosi kwa sababu kocha Flick anawapenelea wachezaji wengine katika nafasi ya mabeki wa kati katika safu ya ulinzi.

Ujerumani itaondoka kwa mazoezi mafupi nchini Oman Jumatatu huku ikitarajiwa kucheza mechi ya kupimana nguvu dhidi ya Oman Jumatano ijayo kabla kuelekea katika kambi yao huko Qatar siku itakayofuata ya Alhamisi. Mechi ya kwanza ya kikosi cha Die Mannscahft ni Novemba 23 dhidi ya Japan, huku Uhispania na Costa Rica zikiwa wapinzani wengine katika mechi za kundi E.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW