G-20 na Afrika na kashfa za rais Jacob Zuma Magazetini
2 Juni 2017Tunaanza na mkutano wa kilele wa mataifa 20 yanayo na yaliyoendelea ulimwenguni-kundi linalojulikana kama G-20, mkutano utakaoitishwa msimu wa kiangazi mwaka huu katika mji wa kaskazini wa Ujerumani Hamburg. Ujerumani ndio mwenyekiti wa kundi hilo la G-20 mwaka huu na imepania kulipa kipa umbele bara la Afrika katika ajenga ya mazungumzo. Gazeti la der Tagesspiegel linazitaja mada muhimu katika mkutano huo wa kiilele kuwa ni pamoja na msimamo finyu wa rais mpya wa Marekani kuelekea biashara ya kimataifa misaada ya dharura kwa Afrika na jinsi maradhi ya kuambukiza yanavyoweza kuutikisa uchumi wa dunia."Kuna cha kutafakari" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la der Tagesspiegel linaloendelea kuandika: Kimsingi Ujerumani ambayo ndio mwenyekiti wa mwaka huu wa G-20 imedhamiria kuutumia wadhifa huo kuwatanabahisha walimwengu kuhusu bara la Afrika. Serikali kuu ya Ujerumani inataka kuwa mstari wa mbele katika kulijumuisha bara la Afrika katika uwanja wa uchumi wa utandawazi. Kwasababu, gazeti linaendelea kuandika , hata kama bara hilo bado halijaendelea vizuri lakini lina uwezo kupitia nafasi bara hilo inayoishikilia kama msafirishaji mkubwa wa mali ghafri, kama soko na pia kama eneo la uzalishaji.
Nchi za Ulaya ,wakoloni wa zamani hazitaki kuachwa nyuma
Wengi wa wanaowekeza barani Afrika wanatokea katika kundi la mataifa 20 yaliyo na yanayoendelea kiuchumi-G-20, linaandika der Tagesspiegel linaloitaja hasa China kuwa mwekezaji mkubwa , lengo likiwa kufaidia zaidi na mali ghafi. Gazeti linazitaja pia, India, Brazil na Uturuki zinazoliangalia bara la Afrika kama fursa nzuri ya uwekezaji na fursa pia ya kujipatia mali ghafi. Kila mmoja anataka kujipendekeza barani Afrika na nchi za Ulaya, wakoloni wa zamani wa bara hilo hawataki pia akuchwa nyuma linamaliza kuandika gazeti la der Tagesspiegel.
Rais Zuma eti afikiria kuhamia uhamishoni Dubai
Visa na mikasa ya rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma vinaendelea kugonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani . Wiki hii barua pepe za rais Zuma zilfichuliwa na zinazungumzia visa vya rushwa vinavyomhusisha rais Zuma, visa vilivyozidisha ghadhabu ya wananchi nchini humo. Gazeti la die Tageszeitung linazungumzia pia kuhusu azma ya rais Zuma kukimbilia uhamishino nchini Dubai. Licha ya mikasa yote hiyo kura ya kutokuwa na imani na rais Zuma imeshindwa kupata uungaji mkono wa walio wengi miongoni mwa chama cha African National Congress -ANC. Gazeti la Süddeutsche limeandika ripoti yenye kichwa cha maneno "Dubai au mtalaka wake", Rais wa Afrika kusini anajitafutia kinga dhidi ya tuhuma za rushwa. Kitakachomsaidia ni kuhamia uhamishoni na pia kama mtalaka wake Nkosazana Dlamini-Zuma atachaguliwa kuwa rais. Gazeti limenukuu barua rais Zuma aliyowaandikia viongozi wa Dubai akisifu jinsi aliyopokelewa alipoitembelea nchi hiyo ya ghuba hivi karibuni na kuwaarifu azma yake ya kutaka kuishi katika falme za nchi za kiarabu-au Emirati. Kama masheikh hao watayapokea pia kwa moyo mkunjufu maombi hayo, hakuna ajuaye, linaandika gazeti hilo linalomaliza kwa kuandika kwa sasa hakuna yeyote anaependelea kuonekana pamoja na rais huyo wa Afrika kusini anaezongwa na kadhia 786 za rushwa.
Mwafrika wa kanza kuchaguliwa kuongoza shirika la WHO
Ripoti yetu ya mwisho inamhusu Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus aliyechaguliwa kuwa mkurugenzi mpya wa shirika la Afya la umoja wa Mataifa-WHO. Raia huyo wa Ethiopia ni mwafrika wa kwanza kukabidhiwa uongozi wa shirika hilo la umoja wa mataifa lililoundwa takriban miaka 70 iliyopita. Gazeti la Berliner Zeitung linakumbusha jinsi Tedros alivyofiwa na kakaake kwa maradhi ya surua akiwa na umri wa miaka mitano tu-kisa ambacho Tedros alihisi si cha haki. Alijua maradhi hayo katika sehemu nyengine za dunia yanatibika. "Sitotulia si mpaka tunahakikisha huduma jumla za afya kwa wote amenukuliwa Tedros akisema baada ya kuchaguliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa WHO.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Khelef