1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G20: Mkutano wa kilele kujadili mazingira na Covid-19

Daniel Gakuba
30 Oktoba 2021

Viongozi wa nchi zilizostawi kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi - G20 wako mjini Roma Italia, kuhudhuria mkutano wao wa kilele, ambao ni wa kwanza wa uso kwa uso tangu kutokea mripuko wa virusi vya corona.

G20 Gipfel in Rom
Viongozi wa G20 wakiwa kwenye meza ya mazungumzo mjini RomaPicha: Andrew Medichini/AP/picture alliance

Waziri Mkuu wa Italia, Mario Draghi ameufungua mkutano wa kilele wa siku mbili wa viongozi wa kundi la nchi zilizostawi kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi za G20, huku ajenda za mabadiliko ya tabia nchi na janga la COVID-19 zikitarajiwa kutawala kwenye mkutano huo.

Soma zaidi: Mawaziri wa fedha na afya wa G20 wakutana mjini Roma

Draghi ametaka kuongezwa kwa kasi ya chanjo kupelekwa kwenye nchi masikini, akisema pengo la chanjo ya virusi vya corona lililopo duniani halikubaliki. Amesema asilimia 3 tu ya watu kwenye nchi masikini duniani ndiyo wamechanjwa, huku asilimia 70 ya watu wa nchi tajiri wakiwa wamepata angalau dozi moja ya chanjo.

Waziri Mkuu wa Italia Mario Draghi akimpokea Kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: Alberto Pizzoli/AFP/Getty Images

Urusi, China zataka chanjo zao zitambuliwe

Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa China, Xi Jinping ambao wameshiriki kwa njia ya vidio, wametaka chanjo zilizotengenezwa nchini mwao zikubaliwe na mataifa ya magharibi, wakati huo huo Urusi na China pia zikiahidi kuzitambua zile zilizotengenezwa katika mataifa hayo.

Hadi sasa, chanjo ya Sputnik V ya Urusi haitambuliwi katika nchi za magharibi, lakini chanjo mbili zinazotengenezwa China, Sinovac Biotech na Sinopharm, ziko kwenye orodha ya dharura ya Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO.

Urusi inataka chanjo yake ya Sputnik V itambuliwe kimataifaPicha: Semyon Antonov/TASS/dpa/picture alliance

Awali, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amezitaka nchi zenye uchumi mkubwa za G20 kuhakikisha ulimwengu wote umepata chanjo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2022, na kuongeza kuwa kipaumbele cha kwanza cha G20 kinapaswa kuendelea na usambazaji haraka wa chanjo ulio sawa na wa kimataifa.

Soma zaidi:Umoja wa Ulaya kutoa dozi milioni 1 za chanjo dhidi ya virusi vya Corona kwa nchi masikini

Wakati huo huo, Ufaransa imesema viongozi wa Umoja wa Ulaya watakutana na viongozi wa Afrika pembezoni mwa mkutano wa G20, katika juhudi za kulisaidia zaidi bara hilo kutokana na janga la COVID-19. Mkutano huo usio rasmi ambao umeandaliwa na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, utafanyika Jumamosi jioni.

Watetezi wa Mazingira wamefika mjini Roma kuwashinikiza viongozi wa G20 kuzingatia hatua za kuokoa mazingira ya duniaPicha: Marina Strauss/DW

Mabadiliko ya tabianchi miongoni mwa vipaumbele

Viongozi wanaojumuika katika mkutano huo wanakabiliwa na shinikizo la kutafuta suluhisho linalofaa kushughulikia kadhia ya mabadiliko ya tabianchi, kuelekea mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuongezeka kwa joto duniani, utakaofanyika mjini Glasgow, Scotland kuanzia Jumapili.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye pia yuko mjini Rome, ameonya kuwa mkutano huo unaweza kuambulia patupu, ikiwa nchi wachafuzi wakubwa wa mazingira hazitaweza kuondoa tofauti miongoni mwao, na kati ya nchi hizo na zile zinazoendelea.

Mpango wa nyuklia wa Iran utajadiliwa pembezoni mwa mkutano huu wa kilele wa G20Picha: Iranian Presidency Office/AP Photo/picture alliance

Mpango wa nyuklia wafanyiwa mapitio

Mzozo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran umejadiliwa pembezoni mwa mkutano wa huu wa kilele wa G20, kati ya Rais Joe Biden wa Marekani, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson.

Maafisa wa nchi hizo wamewaambia waandishi wa habari kuwa kikao hicho kimeitishwa na Ujerumani, kwa lengo la kuzipitia mada muhimu kabla ya mazungumzo yanayotarajiwa kuanza baadaye.

Papa Francis aalikwa kuizuru India

Katika taarifa nyingine, waziri mkuu wa India, Narendra Modi ametumia fursa ya ziara yake mjini Roma kumualika kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis kuizuru India. Mwaliko huo ameutoa baada ya kukutana na Papa Francis kwa mara ya kwanza.

Soma zaidi: G20: Merkel atoa wito wa mshikamano wa kimataifa dhidi ya corona

India nchi yenye waumini wengi wa Kihindu, ina takriban Wakristo milioni 28. Kabla ya mkutano wa viongozi hao wawili, redio ya Kanisa Katoliki iliripoti kuwa maombi ya awali yaliyotolewa na Vatican kutaka Papa aizuru India, yalikataliwa na nchi hiyo.

afpe, rtre, ape

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW