1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G20 ndiye msimamizi mkuu wa uchumi wa dunia

25 Septemba 2009

Viongozi wa mataifa tajiri na yale yanayoinukia wameafikiana kuwa kundi la G20 ndilo litakalokuwa msimamizi mkuu wa masuala ya uchumi wa ulimwengu.Kikao hicho cha Pittsburgh,Pennsylvania kimeingia siku yake ya pili.

Nembo ya Kikao cha Pittsburgh

Ajenda kuu ya mkutano huo wa kilele wa uchumi ni kuzitathmini njia za kuuzuwia mtikisiko wa kiuchumi ulioanza kudhihirika mwaka uliopita kushuhudiwa tena.Ikumbukwe kuwa kikao hicho cha kilele kinafanyika ikiwa ni mwaka mmoja tangu hilo litokee.

Viongozi hao wa mataifa 20 tajiri na yale yanayoinukia waliafikiana kulitumia kundi hilo kuwa msimamizi mkuu wa masuala ya uchumi wa ulimwengu. Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Barack Obama kuaandaa kikao hicho cha kilele kwa madhumuni ya kutathmini mbinu zitakazozuwia uwezekano wa mtikisiko wa kiuchumi kutokea tena.

China na India kuwa na usemi

Kwa mujibu wa taarifa yao ya pamoja kudni la G20 ndilo litakalokuwa msimamizi mkuu wa masuala ya uchumi wa ulimwengu na litausambaza ushawishi wake kwa mataifa yanayoinukia kama vile China na India.

Tangazo hilo limetolewa baada ya viongozi hao kuafikiana kuwa na mfumo unaoweka mbinyo zaidi katika sekta ya fedha ili kuepuka mtikisiko wa uchumi kutokea tena kama ilivyoshuhudiwa mwaka uliopita.Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anaziunga mkono kauli hizo''Mtazamo wangu ni ikiwa tunafuata mkondo ulio sahihi . Hili ni jambo linaloweza kutokaea wakati wowotena ndiyo maana kwa upande wetu tungetaka kuchukua hatua ili kuzuwia isitokee tena ."

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwasili kikaoniPicha: AP

Kulingana na rasimu ya taarifa yao iliyowafikia shirika la habari la AFP,viongozi wa G20 wana azma ya kutoa kauli ya pamoja ya kuziondoa bonasi za wafanyakazi wa mabenki wa ngazi za juu vilevile kuziruhusu serikali kuendelea na harakati za kuunyanyua uchumi mpaka pale itakapobainika kuwa umeimarika.

Kundi la G8 la mataifa tajiri pekee ulimwenguni limekuwa likiichukua nafasi hiyo ya usimamizi wa masuala ya uchumi wa ulimwengu tangu mwaka 1975 katika ngazi tofauti na limekuwa likifanya mikutano maalum kila mwaka kuyajadili masuala hayo.Kundi hilo linayajumuisha mataifa ya Uingereza,Ujerumani,Ufaransa,Urusi,Japan,Canada,Italia na Marekani.

Sauti za wanyonge zisikike

Viongozi wa mataifa yanayoinukia nao pia walitaka sauti zao zisikike katika maamuzi ya kundi hilo la G20.Viongozi wa ulimwenguni wameahidi kufanya mabadiliko ya jumla katika Shirika la Fedha Ulimwenguni la IMF na imejitokeza haja ya kulishughulikia suala la kuusawazisha mchango wa mataifa yanayoinukia wakati wa kupitisha maamuzi ya pamoja.Kiongozi wa Benki ya Dunia Robert Zoellick anasisitiza kuwa mataifa masikini yana uwezo mkubwa ambao haujapewa nafasi''Mataifa yanayoendelea yana uwezo mkubwa wa kuwa soko jipya ila tatizo ni ufadhili na mikakati.Ikiwa tutawafadhili bila shaka tutaunda soko linalohitajika.

Hakuna ridhaa ya wote

Hata hivyo baadhi ya mataifa ya Ulaya hayajafurahishwa na wazo hilo kwani ushawishi wao utapungua katika taasisi hiyo.Makubaliano yoyote yatakayofikiwa katika kikao cha Pittsburgh kuhusu mchango wa mataifa yanayoinukia yana uzito kwani shirika la fedha la IMF litayaidhinisha katika kikao chake kijacho.Shirika hilo linajiandaa kufanya kikao cha kila mwaka cha siku mbili ifikapo tarehe 6 mwezi ujao wa Oktoba mjini Istanbul,Uturuki.

Kikao hicho cha G20 kinafanyika ikiwa ni miezi sita tangu viongozi wa kundi hilo kukutana mjini London kwa minajili ya kuandaa mbinu za kushirikiana kupambana na mtikisiko wa kiuchumi.Mkutano huu una azma ya kuzitathmini harakati hizo na ahadi zilizotolewa mpaka sasa.Rais wa Benki ya Dunia Robert Zoellick ameonya kuwa ''Mkutano wa London ulifanikiwa ila wasiwasi wangu kwa sasa ni kuwa uchumi unakua kwa kasi ndogo jambo ambalo huenda likawafanya watu kupitisha maamuzi ya binafsi ambayo yatasababisha matatizo kwani uchumi bado haujaimarika.''

Wanaharakati wanaoupinga mfumo wa ubepari wanalipinga kundi hilo kwa madai kwamba linaunga mkono utandawazi na sera za biashara huria.Viongozi hao pia wameahidi kuongeza juhudi ili kuyahitimisha ifikapo mwaka 2010 mazungumzo ya biashara ya Doha yaliyosuasua kwa kipindi cha miaka minane.

Wakereketwa nao hawakuachwa nyuma kwani walipambana na polisi waliowafyatulia mabomu ya gesi ya machozi ilikuwatawanya.Kulingana na polisi watu 15 walikamatwa wakati wa purukushani hizo. Taarifa ya pamoja kuhusu maazimio ya kikao cha Pittsburgh inatarajiwa kutangazwa baadaye hii leo.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya-AFPE/RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman




Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW