G20: Viongozi wakubaliana kuhusu tabianchi
29 Juni 2019Baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu, kundi la mataifa 20 yanayoongoza kiuchumi duniani lilikubaliana Jumamosi kutokubaliana juu ya kupambana dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, huku Marekani ikikataa kutoa ahadi ya kutekeleza makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi yaliofikiwa 2015 mjini Paris.
Akizungumza mwishoni mwa mkutano wa kilele mjini Osaka, waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe alisema viongozi wamepata msimamo wa pamoja kuhusu mabadiliko ya tabianchi licha ya tofauti kubwa katika mitizamo ya wanachama.
"Tutakuwa na maandishi yanayofanana na ya Argentina. Tangazo la A 19+1," kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliwaambia waandishi habari kandoni mwa mkutano huo wa G20.
Kama ilivyokuwa kwenye mkutano wa mjini Buenos Aires, tangazo hilo jipya linasema kwamba Marekani imekariri uamuzi wake wa kujitoa kwenye makubaliano ya Paris "kwa sababu hayawanufaishi wafanyakazi na walipakodi wa Marekani."
Waraka huo ulisema mataifa yaliosaini makubaliano ya Paris "yataangazia mikakati na njia pana za teknolojia safi, ikiwemo miji ya kisasa, mifumo ya ekolojia na mikakati ya kijamii, suluhisho za kiasili na maarifa ya kiasili na kienyeji," ilisoma taarifa ya mwisho.
uwezekano wa lengo la kuondoa gesi chafu ifikapo 2050
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisifu makubaliano hayo, akiwaambia waandishi habari nchini Japan kwamba "mchakato huu hauwezi kurudishwa nyuma."
Merkel aliongeza kuwa baadhi ya viongozi waliokuwepo Osaka tayari wameonyesha kuwa wako tayari kuongeza ahadi zao kupunguza gesi chafu kwa kulenga kuondoa kabisaa utoaji wa gesi hiyo ifikapo mwaka 2050.
"Kwa matazamo wetu, mabadiliko ya tabianchi yataamua hatma ya mwanadamu, hivyo ni muhimu kwamba kizazi chetu kinafanya chaguo zilizosahihi," alisema waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi katika mkutano wa waandishi habari pamoja na mwenzake wa Ufaransa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kufuatia mazungumzo juu ya mabadiliko ya tabianchi.
Sera ya biashara ya haki inahitajika
Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe alisema viongozi 20 kwenye mkutano wa kilele wa G20 pia walithibitisha haja ya sera ya biashara huru, ya haki na isiyobagua.
"Uchumi wa dunia unaendelea kukabiliwa na hatari za kushuka wakati ambapo mizozo ya kibishara ikiendelea," Abe aliuambia mkutano wa habari. "Viongozi wa G20 wamekubaliana juu ya haja kwa nchi wanachama kuongoza ukuaji imara wa kiuchumi duniani," huku wakiwa tayari kuchukuwa hatua zaidi ikihitajika," alisema.
Abe aliongeza kuwa alimuambia rais wa Marekani Donald Trump na rais wa China Xi Jinping kwamba ilikuwa muhimu zaidi kushiriki katika majadiliano ya tija kutatua mzozo wao wa kibiashara.
Baada ya mazungumzo yao, Trump na Abe walisema Marekani na China zimekubaliana kurejea mazungumzo ya biashara, na Washington haitaweka ushuru zaidi kwenye bidhaa za China kwa sasa.
Vyanzo: Mashirika