G7 kuamua juu ya Crimea
24 Machi 2014Wawakilishi wa mataifa 53 wanahudhuria mkutano huo wa usalama wa nyuklia, akiwemo Rais Barack Obama wa Marekani, Rais Xi Jinping wa China na viongozi wa Ujerumani, Japan, Uingereza, Canada na Ufaransa.
Lakini badala ya usalama wenyewe wa nyuklia, macho zaidi yanaelelekezwa kwenye mkutano maalum wa mataifa ya G7, ambao utaijadili hatua ya Urusi kwenye Rasi ya Crimea.
Obama, aliyewasili mjini Amsterdam asubuhi ya leo, hakuficha dhamira yake ya kutumia kila nafasi aipatayo kuishinikiza Urusi.
"Ulaya na Marekani zimeungana katika kuiunga kwetu mkono serikali na watu wa Ukraine. Tumeaungana katika kuifanya Urusi ipate na machungu ya matendo yake hadi sasa." Alisema Obama.
Uingereza yaitishia Urusi
Kabla ya kuondoka nyumbani, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, aliliweka pia suala la Urusi na Crimea kwenye nafasi ya juu, ingawa aliondosha kabisa uwezekano wa kupeleka wanajeshi kwenye eneo hilo kujibu operesheni za kijeshi za Urusi nchini Ukraine.
"Sifikirii ikiwa ni muhimu kubadilisha mipango yetu ya kuwaweka wanajeshi wa Kiingereza nchini Uingereza, lakini nadhani ni muhimu kwamba tutume ujumbe wa wazi kwa washirika wetu kwamba tuniamini NATO na tunaamini kwenye usalama wao." Alisema Cameron.
Licha ya kwamba Uholanzi si mwanachama wa kundi hilo la G7, lakini ilikubali kuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo maalum juu ya Crimea.
Viongozi hao wa G7 wanaweza pia kutumia mazungumzo yao haya kuamua hatima ya kundi la G8 - ambalo linaijumuisha pia Urusi tangu mwaka 1998.
Tayari viongozi hao wameshasitisha matayarisho kwa ajili ya mkutano wa kilele wa G8 uliokuwa ufanyike kwenye mji wa Olimpiki wa Sochi nchini Urusi, hapo mwezi Juni.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf