G7, Marekani yatakiwa kueleza msimamo dhidi ya Syria
10 Aprili 2017Mkutano huo unafanyika katika mji wa Lucca nchini Italia, Jumatatu. Taharuki imetanda tangu Marekani iishambulie kambi ya kijeshi ya Syria wiki iliyopita huku Urusi inayomuunga mkono rais wa Syria Bashar al-Assad ikilalamika kuhusu shambulizi hilo.
Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye nchi yake iliondolewa kutoka kwenye kundi la G8 baada ya kuitwaa kimabavu rasi ya Crimea kutoka kwa Ukraine mwaka 2014, alilikemea shambulizi hilo akisema ni uvamizi dhidi ya nchi huru. Vita hivyo vya maneno vimepata jawabu kutoka eneo la Magharibi kwani waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson aliifutilia mbali ziara aliyokuwa ameipanga kuelekea Moscow, huku Uingereza ikiituhumu Urusi kwa kuhusika katika mauaji kwenye lile shambulizi la kemikali lililofanywa katika mji wa Syria wa Khan Sheikhoun, jambo lililopelekea Marekani kushambulia.
Korea Kaskazini kuiadhibu vikali Marekani
Korea Kaskazini kama Urusi, imeikosoa Marekani kwa shambulizi lake la wiki iliyopita huko Syria, katika taarifa ya wizara ya mambo ya nje iliyosomwa katika kituo cha habari cha KRT nchini humo.
"Shambulizi la Marekani nchini Syria haliwezi kusameheka kwani ni uvamizi dhidi ya nchi huru na tutawaadhibu vikali," ilisema taarifa hiyo, "kuna wale wanaosema kwamba lile shambulizi la Marekani huko Syria ni hatua ya kutuonya, lakini sisi hatuogopeshwi nalo."
Mkutano huo utazipatia Italia, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Canada na Japan fursa ya kwanza nzuri ya kumdadisi waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson, iwapo Marekani sasa imejitolea kumuondoa madarakani rais wa Syria Bashar al-Assad. Rais Donald Trump alikuwa amedokeza kwamba, hatoingilia sana masuala ya Syria kama wale waliomtangulia na kwamba atapuuza ukiukwaji wa haki za kibinadamu iwapo hilo litainufaisha Marekani.
Shambulizi hilo dhidi ya Syria liliwashangaza wanadiplomasia wengi. Lakini kuna ati ati kuhusiana na iwapo Marekani inamtaka Assad aondoke uongozini sasa kama vile raia wengi wa Ulaya wanavyoshinikiza au mashambulizi hayo ya wiki iliyopita yalikuwa ni kama onyo tu.
Ulaya yaghadhabishwa na tofauti iliyojitokeza kuhusu lengo la Marekani huko Syria
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley, alisema mwishoni mwa juma kwamba, kubadilishwa kwa uongozi nchini Syria ndilo jambo la muhimu kwa rais Trump huku Tillerson akisema, suala wanalolipa kipau mbele ni kulishinda kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS.
Ujumbe huo wa kukanganya kutoka Marekani umeyaghadhabisha mataifa ya Ulaya ambayo yanataka uungaji mkono wa Marekani kwa suluhu la kisiasa litakaloletwa na kubadilishwa kwa madaraka nchini Syria.
Lakini Masuala mengine yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni taifa la Libya ambapo Italia inataraji kuwepo na uungwaji mkono kwa serikali ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli.
Mazungumzo hayo ya mawaziri hao wa mambo ya nje yatatayarisha njia ya mkutano wa viongozi utakaoandaliwa katika mji wa Sicily huko huko Italia mwishoni mwa mwezi Mei.
Mwandishi: Jacob Safari/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga